MKUU wa Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro, amewataka askari wa usalama barabarani kutumia busara na si tu kuwapiga faini madereva bila kuwapa onyo na kuwa suala hilo si sahihi.
Akizungumza mjini Iringa jana, Sirro alisema pamoja na kuwa kuna dhana potofu miongoni mwa jamii kuwa askari hao wamepangiwa kiasi cha fedha za kukusanya kwa siku, jambo hilo si kweli.
“Hakuna askari wa usalama barabarani anayepangiwa makusanyo ya faini, IGP ni mmoja nchi hii, mimi ndio IGP nasema hakuna IGP anayepangia askari wa usalama barabarani pesa, labda wana IGP wao nyumbani kwao,” alisema.
Alisema kazi ya askari hao ni kusimamia sheria za usalama barabarani na si kila kosa ni la kumpiga mtu faini, na kwamba ni lazima busara itumike ikiwa ni pamoja na kumpa onyo mhusuka pamoja na elimu kabla ya kukimbilia kumpiga faini .
“ Jambo la kwanza la kuzuia uhalifu ni elimu kwanza, siku ya pili onyo na siku ya tatu ni faini, sio unaanza kwa faini pasipo kumpa elimu wala onyo.
Wakati mwingine hawa polisi si malaika yawezekana wametoka nyumbani wakiwa ovyo, hivyo wanahamishia hasira zao kwenye faini, ila naomba muwaelewe hawa ni watoto wetu tuwasamehe bure ila ninachosisitiza elimu kwanza, ukiona dereva kaongeza spidi kwanza mpe elimu,” alisema.
Katika hatua nyingine, alisema haoni changamoto kufanya kazi na wanasiasa kwani wanasiasa ni sehemu ya jamii na wanafanya siasa kwa mujibu wa sheria na kwamba hakuna aliye juu ya sheria.
“Hakuna mwanasiasa aliye juu ya sheria, akikiuka sheria atawajibika kwa mujibu wa sheria na atashughulikiwa kama mtu mwingine yeyote, hivyo hakuna mwanasiasa atakayenisumbua mwanasiasa atakayetoa lugha ya matusi atakamatwa tu kazi yangu ni rahisi sana kwa kuwa nasimamia sheria,” alisema.
Kuhusu uboreshaji wa nyumba za askari polisi nchini alisema kuwa kuna programu maalum ya kuboresha makazi ya askari polisi kupitia fedha wanazopata .
“ Nimefurahi sana kuwafahamu nimekuwa nikisoma tu nondo zenu ila leo nimewafahamu ahsanteni sana ila naombeni jaribuni kuandika kile ambacho nimesema kuna mmoja jana Mbeya ameandika IGP anasema wana Siasa wasiongee hii si kweli mimi siwezi kuwazuia wanasiasa kuongea wazungumze tu ila wasivunje sheria,” alisema.
Kuhusu kauli mbali mbali ambazo amekuwa akiziandika kwenye mitandao ya kijamii Mange Kimambe alisema kuwa kauli zake hizo zimekuwa zikivunja sheria ndani ya nchi ila mpango wa Jeshi la Polisi kuhusu mtu huyo hawezi kusema kwa sasa .
No comments:
Post a Comment