Moja wa maafisa wa Benki ya Dunia,ambaye pia huratibu shughuli za TASAF (TTL) katika benki hiyo , bw. Muderis Mohamed (aliyesimama) akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa maendeleo na serikali mjini Dar es salaam.
Mtaalamu wa Habari na Mawasiliano wa TASAF ,Bi. Zuhura Mdungi (aliyesimama) akitoa maelezo ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini- PSSN- kwenye mkutano wa wadau na serikali kwenye ukumbi wa mikutano wa TASAF ,mjini Dar es salaam.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa wadau wa maendeleo, serikali na watumishi wa TASAF –wakiwa katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo kupata maelezo ya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini kabla ya kuanza ziara ya kikazi katika maeneo mbalimbali nchini kukutana na walengwa na viongozi.
Na Estom Sanga-TASAF
Baadhi ya watendaji wa Serikali na Wadau wa Maendeleo wanaanza ziara katika maeneo mbalimbali ya Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF- kukutana na walengwa wa Mpango huo na kuona mafanikio na changamoto za utekelezaji wake.
Akitoa maelezo kabla ya kuanza kwa ziara hizo zitakazofanyika katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Kigoma, Tabora, Singida, Kilimanjaro ,Morogoro na Zanzibar ,Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bw. Ladislaus Mwamanga ameishukuru serikali na wadau wa maendeleo kwa mchango mkubwa wa kufanikisha shughuli za Mpango huo unaohudumia zaidi ya kaya masikini MILIONI MOJA na Laki MOJA nchini kote.
Hata hivyo Bwana Mwamanga amesema licha ya kuweko kwa mafanikio makubwa ya utekelezaji wa Mpango, bado kuna asilimia 30 ya vijiji nchini ambavyo havijafikiwa na huduma za Mpango jambo linaloendelea kulalamikiwa na wananchi ambao hawajafikiwa na Mpango huo na hivyo amesema serikali kupitia TASAF inalifanyia kazi kwa karibu suala hilo.
Aidha katika maelezo ya utekelezaji wa Mpango huo yaliyowasilishwa na Mtaalamu wa Habari na Mawasiliano wa TASAF,Bi. Zuhura Mdungi imeonyeshwa kumekuwa na mafanikio katika kubadili fikra na za kaya za walengwa katika kupambana na umasikini kwa kutumia huduma za Mpango huo mkubwa kupata kutekelezwa nchini .
Shughuli za ziara na majadiliano kati ya serikali,wadau wa maendeleo na maafisa wa TASAF hufanyika kila baada ya miezi sita kuona namna utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya masikini unavyoendelea kwa kukutana na walengwa ,viongozi,wataalam na kuwasikiliza namna huduma za Mpango huo zinavyosaidia jitihada za serikali za kupunguza adha ya umaskini kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment