Maseneta wa Marekani walisema Jumapili kwamba Ikulu ya Marekani-White House haijaeleza kwa kina kuhusu kuwepo kwa jeshi la Marekani nchini Niger baada ya vifo vya wanajeshi wane raia wa Marekani kutokea huko mwanzoni mwa mwezi huu na maseneta hao wanataka majibu zaidi kuhusiana na operesheni za Marekani katika taifa hilo lililopo Afrika magharibi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters seneta wa Republican Lindsey Graham na kiongozi wa chama cha Democrat katika baraza la seneti Chuck Schumer walisema katika mahojiano tofauti kwamba wanaunga mkono juhudi za seneta wa Republican John McCain za kupata majibu kutoka Pentagon juu ya shambulizi la kushtukiza dhidi ya wanajeshi wa Marekani waliokuwa wakipambana na wanamgambo wa ISIS nchini Niger.
Graham na Schumer hawakujua kuhusu kuwepo kwa Marekani huko Niger na alisema Congress inahitaji taarifa zaidi juu ya kile kitakachokuwa uhusishwaji wa muda mrefu na wa wazi. “sikuwa ninafahamu kwamba kulikuwa na wanajeshi 1,000 wa Marekani huko Niger, Graham alisema kwenye kipindi cha Meet the Press cha televisheni ya NBC ya Marekani”. Hii ni vita isiyokwisha bila mipaka na hakuna kidhibiti cha muda na maeneo aliongeza. "Unatakiwa kutueleza mengi sisi na McCain ana haki ya kusema hivyo".
Wakati huo huo waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis alimwambia Graham na McCain ambaye anahudumu kama mwenyekiti wa kamati inayoangalia shughuli za jeshi katika seneti siku ya Ijumaa kwamba jeshi linabadili mkakati wake wa kupambana na ugaidi ili kulenga zaidi kwenye bara la Afrika na kupanua uwezo wa kutumia jeshi dhidi ya washukiwa magaidi.
Shambulizi la mwanzoni mwa mwezi huu ambalo maafisa wa Marekani wanashuku lilifanywa na ushirika wa kundi la Islamic State katika eneo limetoa mwangaza kuhusu kuwepo kwa Marekani kwenye operesheni za kukabiliana na ugaidi huko Niger ambako Marekani ina kiasi cha wanajeshi 800.
No comments:
Post a Comment