Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe ameshinda kwa kishindo uchaguzi ulioitishwa kabla ya wakati wake leo Jumapili (22.10.2017),na kumpatia mamlaka yanayoimarisha msimamo wake ambao tayari ni wa vita dhidi ya Korea kaskazini.
Muungano wa kihafidhina wa waziri mkuu Abe unaelekea kupata ushindi wa viti 311 katika bunge lenye viti 465 , kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyochapishwa na kituo cha televisheni cha binafsi cha TBS, na kumfanya kiongozi huyo wa Japan kuwa kiongozi aliyeshika madarakani kwa muda mrefu zaidi nchini humo.
Ushindi huo wa kishindo bila shaka utaweza kutia nguvu dhamira ya Abe kupambana na hatari ya kinyuklia inayoletwa na Korea Kaskazini , wakati mshirika huyo muhumi wa Marekani katika kanda hiyo akiongeza mbinyo dhidi ya utawala wa Pyongyang baada ya kufyatua makombora mawili juu ya anga ya Japan katika muda wa mwezi mmoja.
Abe alikuwa anaelekea kupata "ushindi wa kishindo," gazeti la kila siku la Yomiuri limesema katika tovuti yake.
Mamilioni ya Wajapan walijitokeza kupiga kura licha ya mvua kubwa na upepo mkali , wakati kimbunga kiliposhambulia taifa hilo na wengi wakipiga kura zao mapema baada ya kutolewa tahadhari kutokana na kimbunga hicho.
"Naunga mkono msimamo wa Abe katika kuipa Korea kaskazini mbinyo," alisema mpiga kura mmoja, Yoshihisa Lemori, wakati akipiga kura yake huku mvua kubwa ikinyesha mjini Tokyo.
Upinzani dhaifu
Chama cha waziri mkuu Abe cha Liberal Democratic , LDP , kimefaidika kutokana na upinzani uliodhaifu na uliogawika, wakati vyama vikuu viwili vilivyokuwa vikipambana nae vikiwa vimeundwa wiki kadhaa tu zilizopita.
Uungwaji mkono kwa chama cha Matumaini , Hope kilichoasisiwa na gavana maarufu wa mjini Tokyo Yuriko Koike uliyeyuka baada ya kupata nguvu kubwa mwanzoni na kilikuwa kikielekea kushinda kiasi ya viti 50 bungeni, matokeo yaliyotolewa na televisheni ya TBS yameonesha.
Akizungumza kutoka mjini Paris ambako alikuwa akihudhuria tukio fulani akiwa kama kiongozi wa mji mkubwa duniani, Koike aliliambia shirika la habari la NHK kwamba anahofia , "matokeo mabaya sana".
Chama kipya cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Constitutional Democratic kimepata matokeo kidogo mazuri kuliko ilivyotarajiwa lakini hata hivyo kiko nyuma sana ya Abe.
"Ushindi wa chama cha LDP ni kutokana na upande wa upinzani kutoweza kuunda umoja," mtaalamu wa masuala ya kisiasa Mikitaka Maysuyama kutoka taasisi ya taifa ya mitaala ya stadi za sera , ameliambia shirika la habari la AFP.
Haijafahamika mara moja baada ya uchaguzi huo iwapo muungano wa vyama vinavyomuunga mkono Abe utabaki na wingi wake wa theluthi mbili."
Wingi wa aina hiyo utamruhusu Abe kupendekeza mabadiliko katika katiba ya Japan iliyowekwa na Marekani ambayo inayalazimisha majeshi yake "kukataa vita" na kuyaweka majeshi yake kuwa ni ya kujilinda tu.
Muda mfupi wa kampeni wa siku mbili ulitawaliwa na masuala ya uchumi na mzozo wa kimataifa kuhusiana na Korea Kaskazini , ambayo imetishia "kuizamisha "Japan ndani ya bahari.
No comments:
Post a Comment