Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Catherine Ruge amehoji leo Alhamisi Oktoba 26,2017 ni kwa nini Tanesco inadai zaidi ya Sh19 bilioni lakini bado inaendelea kuilinda hospitali hiyo kwa kutoiondoa katika jengo hilo.
Amehoji hilo wakati kamati ilipokutana na watendaji wa Tanesco waliowasilisha taarifa na mipango yake, ambayo pia imekataliwa na wajumbe wakisema haina jipya.
Mbali ya hilo, mbunge Ruge amehoji kuhusu deni kubwa la Sh850 bilioni ambalo amesema haliwezi kulipika kutokana na mipango aliyoiita kuwa mibovu.
Mhasibu wa Tanesco, Renata Ndege amesema ni kweli shirika hilo limeelemewa na madeni ambayo kuyalipa yote kwa fedha za kutegemea mapato yake ni jambo lisilowezekana.
Ndege aliwaeleza wabunge kuwa shirika limepanga kukopa fedha katika benki kubwa zenye masharti nafuu ili kulipa deni hilo.
Kuhusu deni la pango, mwanasheria wa Tanesco, Mwesiga Mwesigwa amesema wamiliki wa hospitali hiyo waliweka zuio mahakamani kuomba kuendelea kulitumia majengo hayo lakini hawalipi kodi.
Katika hatua nyingine, wajumbe wa kamati wameikataa taarifa na mipango ya Tanesco wakisema haina jipya zaidi ya kulindana.
Kamati ya PAC chini ya Mwenyekiti Naghenjwa Kaboyoka imevutana na Tanesco kuhusu mipango yake wakieleza ina upungufu.
No comments:
Post a Comment