Friday, October 27

Vifaatiba vyakwamisha madaktari bingwa Ligula

Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara
Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara waliojitokeza katika Hospitali ya Rufaa ya  Ligula ili kupata huduma za matibabu zilizokuwazikitolewa na madaktari bingwa mwezi uliopita. Picha na HaikaKimaro 
Afya ni hali ya kujisikia vizuri kimwili, kiakili, kiroho na kiutu. Binadamu asipokuwa na afya njema, hawezi kutekeleza majukumu yake ya kila siku ipasavyo.
Kutokana na umuhimu wa afya kwa mwanadamu, baadhi ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) waliamua kuweka kambi ya wiki moja Mkoani Mtwara kwa lengo la kutoa huduma kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na matatizo mbalimbali.
Pamoja na kuwatibu, kambi hiyo ilienga kuwapunguzia wagonjwa gharama za usafiri na malazi wanapoenda kutafuta huduma za kibingwa nje ya Mkoa wa Mtwara.
Mpango huo ulibuniwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali za rufaa za kanda, ili kufikisha huduma za matibabu kwa wanachama wake na wananchi kwa ujumla.
Hata hivyo, baadhi ya wataalamu walishindwa kuutekeleza mpango huo kutokana na Hospitali ya Rufaa ya Ligula kukosa vifaatiba.
Mmoja wa madaktari bingwa wa dharura, mahututi na usingizi (Anesthesiologist) wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Albert Ulimali anasema waliamua kutoka nje ya Dar es Salaam kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi wa mikoa ya pembezoni yenye changamoto ya kupata wataalamu wa afya na kupunguza msongamano katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Si wananchi wote wanaweza kusafiri kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kupata huduma, lazima kutakuwa na changamoto za usafiri na malazi, hivyo kuleta huduma huku inakuwa rahisi kuwahudumia wagonjwa wengi kwa wakati mmoja,” anasema Dk Ulimali.
Uhaba wa vifaa Hospitali ya Rufaa Ligula
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Ligula ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji, Kariamel Wandi anasema daktari bingwa wa maradhi ya koo na masikio ameshindwa kufanya kazi yake baada ya kukosekana kwa vifaa vya upasuaji na kwamba, huduma hiyo haijawahi kutolewa katika hospitali hiyo kwa miaka ya karibuni.
“Vifaatiba vya kutibu koo na masikio karibu vyote vikiwa ni vya upasuaji hatuna hospitalini hapa na huduma hiyo haijawahi kutolewa hapa hospitalini, kama ilishawahi kutolewa nafikiri ni miaka ya nyuma sana,” anasema Dk Wandi.
Anavitaja baadhi ya vifaa vya upasuaji vilivyokosekana kuwa ni vya kushikia tishu na nyama. Pia, baadhi ya vipimo kwenye maabara havifanyi kazi kutokana na baadhi ya mashine kuchakaa.
Anasema kutokana na changamoto hiyo, wanakusudia kuzungumza na ofisi ya NHIF kama wanaweza kuwakopesha vifaatiba kusudi wataalamu watakaporudi tena wavikute.
Pia, anasema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto ya madaktari bingwa licha ya kuhudumia wagonjwa wengi. “Niiombe Serikali iangalie namna gani itazisaida hizi hospitali za pembezoni, zinatibu watu wengi lakini zina uhaba mkubwa wa baadhi ya vifaa na hata rasilimali watu wakiwamo wauguzi na madaktari,” anasema.
Dk Wandi anasema hilo ni tatizo sugu tangu 1964 hospitali hiyo ilipofunguliwa, anaiomba Serikali isaidie kutatua tatizo hilo.
Wagonjwa wengi waliojitokeza katika mpango huo ni wale wenye kusumbuliwa na maradhi ya ndani yakiwamo macho, maradhi ya kina mama, kisukari, presha na yenye kuhitaji upasuaji likiwamo tenzi dume.
“Watu wengi waliojitokeza na daktari alinieleza ukanda huu una watu wanaougua presha ya kupanda hadi 300 wanatembea nayo bila wasiwasi na wagonjwa wa aina hiyo walikuwa wengi, lakini pia maradhi wanawake yameongezeka wakati mwingine daktari alikuwa anaondoka saa 3 usiku,” Dk Wandi.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Nathaniel Minangi anasema matatizo yaliyojitokeza zaidi kwa kina mama ni pamoja na ya kijamii.
Anasema wengi wao wamebainika kuwa na tatizo la kutobeba mimba kutokana na kuugua tezi la kizazi maarufu bomu kwa wakazi wa mkoani Mtwara.
“Matatizo yaliyojitokeza zaidi kwa kina mama tunayaita ya kijamii kwa sababu si ugonjwa unaoweza kuhatarisha maisha yao, lakini ni suala la kijamii, yaani kama mwanamke hapati mtoto kwenye familia yake hutengwa, kwa hiyo mtoto kwake ni muhimu sana, tatizo lingine ni tezi kwenye uvimbe ambalo wananchi wanaita bomu,” anasema Dk Minangi.
Daktari bingwa wa maradhi ya macho, Judith Mwende anasema wagonjwa wengi wa aina hiyo walikuwa na presha ya macho inayosababisha kupoteza uwezo wa kuona, ugonjwa mwingine ni mtoto wa jicho ambao wengine imeshindikana kuwafanyia upasuaji baada ya kubainika wanatatizo la kubwa la shinikizo la damu.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na madaktari bingwa hao ulibaini wagonjwa wengi wanatumia dawa za macho bila kufuata maelezo sahihi ya daktari au wataalamu wa afya.
“Wengi wana shida ya presha ya macho, lakini wanatumia dawa za maji bila utaratibu na si kwa Mtwara pekee, ni nchi nzima, hizi dawa zina utaratibu wake, unaweza ukazitoa lakini siyo kwa kila mgonjwa anayewashwa macho, mwingine anaenda duka la dawa anasema anawashwa macho anapewa dawa, Serikali waliangalie hili,” anasema Dk Mwenda.
Daktari wa maradhi ya wanawake, Dk Nathaniel Minangi anasema mpango huo unaotekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ni mzuri na unalenga kusaidia wananchi, lakini ni vyema kama ungebebwa na Serikali kwa kutengeneza sera ya afya ili kuwapa wananchi wa kipato cha chini unafuu wa matibabu, lakini pia kuwapo na maandalizi ya mazingira mazuri ya kazi na vitendea kazi ili kutoa huduma bora zaidi.
“Kwa mpango huu unaofanywa na NHIF ningependekeza pia serikali iuweke kama mpango wake, kwa sababu changamoto kubwa ni kipato cha wananchi wengine waliokuwa na uwezo, wamepata huduma na waliokuwa hawana uwezo wamekosa huduma. Kwa sababu gharama inaweze kuonekana ndogo kulingana na tatizo la mtu, lakini kwa mfuko wa mtu ni gharama kubwa, watunga sera wangeliweka katika mpango wa serikali,” anasema Dk Nathaniel Minangi na kuongeza;
“Wataalamu bado ni wachache, hospitali ya rufaa inakuwa na daktari mmoja, ni upungufu ambao unatakiwa kufanyiwa kazi. Lakini pamoja na yote, inatakiwa kuwa na maandalizi utakapokwenda kufanyia kazi, kunahitaji nyumba, mazingira mazuri ya kazi na vifaa kwa sababu hata sisi madaktari wa maradhi ya wanawake na maradhi ya kike kuna upungufu wa vifaatiba, Serikali washirikiane na NHIF ili kuboresha huduma hizi zaidi.”
Daktari wa Macho na upasuaji wa mtoto wa jicho wa Hospitali ya Ligula, Upendo Abeid anashauri wananchi kujijengea mazoea ya kupima afya za macho mara kwa mara ili kugundua matatizo yanayoanza taratibu na kusababisha upofu.
Aidha, anashauri wenye presha ya mwili na kisukari kupima macho yao walau mara moja kutokana na magonjwa hayo kuwa na uhusiano na macho.
Hospitali ya Ligula inahudumia wagonjwa kutoka Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma na hata nchi jirani ya Msumbuji kwa ajili ya upasuaji wa mtoto wa jicho.
Anasema kwa sasa hufanya kazi hiyo kwa msaada wa Shirika la Heart to Heart Foundation(HtHF) kwa udhamini wa Korea International Cooperation Agency (Koica)
“Mahitaji ni makubwa daktari wa macho kwa Mtwara niko peke yangu na si bingwa, Mkoa wa Mtwara tunapokea wagonjwa wengi hata wa mikoa ya jirani na nchi jirani, ninaelemewa kwa kweli kwa sababu bado natakiwa pia niende wilaya zote za mkoa huu kwa ajili ya kazi ya upasuaji wa macho ambayo nawezeshwa na Shirika la Heart to Heart Foundation, kwa maana hiyo, bila wao hata hiki kidogo tunachokifanya tusingeweza, Serikali itusaidie au iwezeshe vifaatiba kwa hospitali ya Lindi ambayo wanaweza kusaidia kupunguza tatizo hili.
Meneja Uhakiki Ubora wa Madai kutoka NHIF, Dk Anuari Mhina anasema wamekuwa wakitekeleza mpango wa huduma za kibingwa kwa mikoa ya pembezoni kwa lengo la kuhamasisha uelewa wa dhana ya bima za afya kwa jamii, pia kuongeza elimu kwa wataalamu kupitia wataalamu wanaotoka kwenye vituo vikubwa vinavyotoa huduma kwa kushirikiana.
Anasema mpango kupitia mpango huo, tayari wananchi 800 wameshaonana na madaktari bingwa, na 373 kati yao sawa na asilimia 47 walitumia kadi za bima ya afya na wengine 426 sawa na asilimia 53 walikuwa hawana kadi za bima ya afya.
“Asilimia kubwa ya wanaokuja kupata huduma hizi ni wananchi ambao hawajajiunga na huduma ya bima ya afya, na kampeni hii inasaidia kuwaletea huduma karibu na baada ya hapo wanapata elimu ya kujiunga na Mfuko wetu wa Bima ya Afya ili iwasaidie kupata matibabu,” anasema Dk Mhina.
Hata hivyo, anasema mpango huo umesaidia wananchi wengi wa pembezoni kupata huduma na kuna mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa hospitali na kutoa huduma kwa wananchi.
Kwani kwa sasa madai madai ya bima ya afya kwa wakati pamoja na suala la kuzikopesha hospitali nyingi vifaatiba kwa zile zinazotegemewa linatekelezwa kwa kasi.
Hivi karibuni akizungumza wakati wa kupokea msaada wa vitanda na magororo 40 vyenye thamani ya Sh 20 milioni kutoka Benki ya Eximu, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego alisema hospitali hiyo inakabiliwa na uhaba wa vifaatiba na vitendea kazi vya kitabibu.
Aidha, alisema kutokana na hospitali hiyo kuwa ya miaka mingi, baadhi ya miundombinu yake imeanza kuchakaa lakini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya, wanaendelea kutafuta njia nzuri ya kuiboresha.
“Tuna upungufu mkubwa wa vifaatiba na vitendea kazi vya kitabibu, lakini ujio wa Exim umeweka alama hapa, hamjakosea mmekuja katika kipindi muafaka. Hospitali ikiwa imekamilika kwa vifaa tunatakiwa tuwe na vitanda 250 lakini tulikuwa navyo 190 na vingine vimechoka lakini kwa hivi 40 tumebaki na upungufu wa vitanda 20,” alisema Dendego.
Mkoa huo wa Mtwara hivi sasa unaendelea pia na ujenzi wa hospitali ya kanda kwa mujibu wa mkuu huyo wa mmkoa ambaye amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwaunga mkono. 

No comments:

Post a Comment