Kupungua kwa vipengele hivyo kunatokana na sababu kadhaa ikiwemo rasilimali fedha za kuendeshea tuzo hizo na zawadi.
Vipengele vilivyopunguzwa ni tuzo za habari za kodi, ununuzi wa umma, Ukimwi na VVU, habari za uchambuzi na matukio, na habari za afya ya uzazi wa mpango.
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga ameeleza hayo leo Ijumaa wakati wa uzinduzi wa tuzo za Ejat za mwaka 2017 mbele ya wanahabari.
Mukajanga amesema mbali na changamoto ya rasilimali fedha, pia wameamua kupunguza vipengele hivyo ili mashindano hayo yafanyike kwa ufanisi zaidi.
Amesema vipengele vilivyobaki ni uandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha; habari za michezo na utamaduni; habari za afya na uandishi wa habari za biashara na kilimo.
Tuzo zingine ni za uandishi wa habari za elimu, utalii na uhifadhi, uchunguzi, data, haki za binadamu na utawala bora, mpiga picha bora wa magazeti na runinga, mchoraji katuni bora, habari za jinsia, wazee na watoto na kundi la wazi.
Mukajanga amesema washindi katika makundi hayo watazawadiwa vyeti, tuzo na zawadi nyingine.
Amesema tuzo ya Mshindi wa Maisha katika Uandishi wa Habari itashindaniwa kwa mara ya sita.
"Tuzo hii hutolewa kwa mwandishi aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari na uhuru wa vyombo vya habari," amesema.
Mukajanga amesema tuzo za Ejat zitatolewa Aprili 27 mwakani na waandishi wametakiwa kuwasilisha kazi zao kuanzia sasa hadi Februari 16 mwakani.
Amesema kazi zinazotakiwa kushindanishwa ni zilizochapishwa na kutangazwa kati ya Januari Mosi hadi Desemba 31 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment