Wabunge hao wamesema hayo leo muda mfupi baada ya kuwasilisha ushahidi wa tuhuma hizo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola.
"Tumepokelewa vizuri sana na Kamisha wa Takukuru na timu yake...tumewapa ushahidi na wamesema wameshaanza kuufanyia kazi," amesema Lema.
Amesema Mlowola amewahakikishia taasisi hiyo ni huru na wataufanyia kazi bila kujali kwamba umewasilishwa na upinzani.
Lema amesema Rais John Magufuli anapaswa kuliona hilo na kuchukua hatua ili uchunguzi uweze kufanyika vizuri.
Kwa upande wake Nassari amesema amemkabidhi flash ya kile alichokisema jana Arusha na nyongeza huku akisisitiza kwamba watatoa ushahidi zaidi.
"Tumesema tuna ushahidi, kama hawaamini na wakiendelea kujibu tutatoa zaidi ya hapa na mimi kesho nitakuja kufungua jalada hapa Takukuru," amesema Nassari
Kuhusu mkanganyiko wa tarehe katika video yenye ushahidi, Nassari amesema: "Hiyo ni ‘setting’ tu lakini anayebisha aseme huyo si DC, si ofisi yake na wakibisha tutatoa ushahidi zaidi ya huu."
Kwa upande wake, Mchungaji Msigwa amesema kilichotokea Arusha kinafanana na Iringa.
"Nami nitakuja kuandika maelezo ya kilichotokea Iringa kwani ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wilaya zinahusika," amesema Mchungaji Msigwa.
Mwananchi imezungumza kwa njia ya simu na Mlowola kuhusu ujio wa wabunge hao ambapo amesema: 'Nipo kikaoni, mtafute msemaji kwa suala hilo."
Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba amesema alipoulizwa amesema, “Sipo ofisini, kwani nilikuwa safari, kesho nitakuwa ofisini hivyo nitaweza kuongelea hilo."
Wabunge hao waliwasili Takukuru saa 8.39 mchana na ilipofika saa 10.04 jioni walitoka ndani na kuzungumza na waandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment