Friday, October 6

Uzazi wa mpango waponza wanawake wa Singida vijini


Singida. Nilihisi nimefika dunia nyingine nilipokanyaga ardhi ya Kata ya Kinyeto iliyopo Wilaya ya Singida Vijijini. Kwani ukosefu wa elimu kuhusu afya ya uzazi imewafanya wakazi wa maeneo hayo kuwa vipofu.
Hili ninalitambua baada ya kukutana na Arafa Juma (24) ambaye ana simulizi ya kisa cha maisha yake, baada ya kushindwa kupewa haki yake ya msingi ya kuchagua kuhusu watoto wangapi atawazaa na kwa wakati gani.
Nyumba ya Arafa iliyo pembezoni mwa kijiji cha Ntunduu, imezungukwa na uzio wa miti ya Minyaa ambayo inazuia baadhi ya wadudu na wanyama wakali kutopenya kutokana na utomvu unaotoka kwenye miti hiyo.
Kwa mara ya kwanza nilipokutana naye ana kwa ana, nilishtuka baada ya kuuona uso wake ukiwa na majeraha makubwa.
Jicho lake la upande wa kushoto lilikuwa limeviria damu, kwa mtazamo likuwa jeusi na kufumba kabisa kutokana na uvimbe uliolizunguka. Ananikaribisha na kutoa mkeka ili tuketi nje, bado alionekana ni aliyeumizwa zaidi kwani hata kuketi kwake chini kulikuwa ni kwa tabu, alikuwa akiegemea zaidi upande wake wa kulia, ishara iliyonionyesha alikuwa na maumivu makali maeneo ya kiunoni na mapajani.
Baada ya mazungumzo, nililazimika kumuhoji nini kimempata, Arafa alishindwa kuwa muwazi ila baada ya kumshawishi sana alizungumza;
“Mume wangu alinipa kipigo cha mbwa mwizi juzi eti nimueleze kwanini sishiki mimba. Niliweka vipandikizi baada ya kuamua kutumia njia za uzazi wa mpango ili niweze kufanya biashara zangu vizuri na kulinda afya yangu,” anaanza kwa kusema mama huyo mwenye watoto watatu, wa mwisho akiwa na mwaka mmoja na nusu.
Arafa anasema aliwahi kumshirikisha mumewe kuhusu jambo hilo lakini hakumsikiliza na aliambulia kipigo. Hiyo ndiyo sababu ya watoto wake kupishana mwaka mmoja na miezi michache, kwani mtoto wake wa kwanza ana miaka mitano.
Anasema alianza kumhoji kwanini hashiki mimba mtoto wake alipofikisha mwaka mmoja, lakini aliendelea kumficha kuwa anatumia uzazi wa mpango.
“Juzi aliporudi nyumbani nilipika chakula tukala, usiku aliniita na kuanza kuifikicha mikono yangu kuanzia kwenye viganja mpaka kwapani, aliposhika mkono huu (wa kushoto), akakutana na hivi vijiti, hapo hapo alianza kunipa,” anasimulia.
Arafa ni miongoni mwa wanawake kadhaa waliopigwa na waume zao baada ya kugundulika wanatumia njia za uzazi wa mpango ili wasibebe mimba za mapema kabla ya watoto wao kukua na kushindwa kupangilia uzazi wao.
Tatu Kisaka (32) alitalikiwa na mumewe miaka miwili iliyopita baada ya kutumia njia za uzazi wa mpango. “Nilikuwa natumia kwa kipindi kirefu kidogo, nilipoamua kuzaa nilifanya hivyo, sasa ilifikia hatua nikasema wanne wametosha kama nilivyoshauriwa hospitali, kilichotokea mume wangu akajua na aliamua kuoa mke mwingine.”
Anasema hata baada ya kuoa aliamua kumuacha kwa talaka tatu na miezi michache baadaye akaoa mke mwingine.
Wanaume wanasema kuhusiana na matumizi ya uzazi wa mpango
Mwandishi wa makala haya alizungumza na Issa Nyamsati mwenye wake wawili na watoto 15 ambaye anasema; “mke wangu akitumia uzazi wa mpango manuacha siku hiyohiyo, mimi nahitaji watoto wengi.” Anasisitiza kuwa kwake haoni kama uzazi wa mpango una faida kwa madi taarifa azipatazo, mpango huo si salama kwa afya mama.
Majibu haya yanaonyesha ni kwa jinsi gani elimu ya uzazi wa mpango imeshindwa kuwafikia wanaume wengi katika eneo hilo.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kinyeto, Romana Haule anasema uongozi unajitahidi kutoa elimu kwa wananchi lakini bado wanaume wengi wagumu kubadilika kifikra.
Romana anasema mwanamke aliyepata elimu kuhusu afya ya uzazi anapodiriki kutumia njia za uzazi wa mpango huambulia kipigo na wakati mwingine hupatiwa talaka na mumewe.
“Huku hakuna lenye afadhali, hata wanaozaa watoto wengi baadhi yao hutelekezwa na waume zao, hizi ndiyo kesi ninazozipokea mara kwa mara katika ofisi yangu,” anasema Romana.
Hata hivyo, anasema kesi zingine zinazoambatana na tatizo hilo ni za wanaume kutelekeza wake zao kutokana na kushindwa kuhudumia familia kubwa. Licha ya hulka waliyonayo ya kutaka kuzaa watoto bila mpangilio, bado hawataki wake zao watumie njia za uzazi wa mpango.
Anasema wapo wanaume wanaofika zahanati kulalamika wake zao hawataki kuhudhuria kliniki na hawataki kutumia njia za uzazi wa mpango, lakini hao ni asilimia tano tu.
“Wanaume watano kati ya 100 ndiyo wanaoafiki matumizi ya njia za uzazi wa mpango, hapa ofisini aliletwa mama mmoja n mumewe kutoka Kijiji cha Mkimbii, anasema ana watoto watano lakini bado mkewe huyo anang’ang’ania kuzaa,” anasema Romana.
Daktari anasemaje
Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kinyeto iliyo pekee katika kata hiyo, Joyce Temu anasema licha ya wanaume kuwa kikwazo, wanajitahidi kutoa elimu ya afya ya uzazi wa mpango kwa wanawake, lakini wengi hawataki kufuata njia hizo na hawahudhurii kliniki.
“Siku hizi kuna mashirika mbalimbali kama Maria Stopes, Familia, PSI hawa wanatuletea huduma za uzazi wa mpango karibu kila mwezi na sisi wenyewe tunazo dawa hizo tunazozitoa mara kwa mara, angalau wameanza kupata uelewa baadhi yao,” anasema Temu.
Hata hivyo anasema bado wanakumbana na vikwazo kutoka kwa wanaume ambao wakiona mke amechelewa kubeba ujauzito, wanawakagua kwa kuwashika shika mkononi wakiona vijiti inakuwa shida.
Anasema uelewa kwa baadhi ya wanaume ni mdogo na wanaamini kwamba kila mtoto anakuja na baraka yake, hivyo wanaona kuzaa ni moja ya mambo muhimu kwa wakati uliopo kwao.
Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto Wilayani Singida, Juliana Ndosi anasema suala la uzazi wa mpango kwa wanawake wengi bado hawajalikubali hasa vijijini.
Lakini wanafanya jitihada ya kutoa elimu kwa kutumia vyombo mbalimbali vya mawasiliano kama redio ili kuweza kuwafikia kwa urahisi.
Singida Vijijini ambayo imeshirikishwa na mashirika mengi ya kutoa elimu juu ya uzazi wa mpango ikiwemo PSI, Maria Stopes na mengineyo, Ndosi anasema wanakabiliana na uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi kuhusu kupanga uzazi.
Alipoulizwa sababu ya idadi kubwa ya wananchi kukosa uelewa licha ya elimu wanayoitoa, Ndosi anasema; “tatizo wakazi wengi bado wanaendekeza mila na desturi zilizopitwa na wakati, mwanaume akizaa watoto wachache anaonekana si rijali.”
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Singida, Sungwa Kabissi anasema wilaya hiyo ina mikakati ya kuhakikisha inasambaza elimu kuhusu afya ya uzazi ili kuepukana na familia nyingi kuwa na watoto ambao haiwezi kuwahudumia.
“Tunaendelea kuelimisha wananchi, ukiangalia familia zenye watoto wengi wanashindwa kuwapa mahitaji yao ya muhimu ikiwamo elimu na hata wapo ambao hawatumii njia za uzazi wa mpango na hawataki hata kuhudhuria zahanati kwa ajili ya huduma muhimu wakati wa kujifungua,” anasema Kabisi.
Mratibu wa Taasisi ya Utepe Mweupe na Uzazi Salama, Rose Mlay anasema asilimia kubwa ya wanawake wa vijijini ambao hawataki kujihusisha na uzazi wa mpango, hawana mwamko wa kuhudhuria kliniki.
Anasema wanaume ndiyo wanapaswa kujihusisha na afya ya mama na mtoto hasa kwa kuongozana na wake zao wanapokwenda kliniki kusudi wanapofundishwa kuhusu uzazi wa mpango na faida zake, waweze kuzijua.
Mlay anatoa wito kwa jamii kuhakikisha mjamzito anajifungulia katika kituo cha afya kwani ni salama na kina wataalamu wengi.
Anasema kutumia uzazi wa mpango pia ni njia muhimu kwa kuwa inamfanya mama apumzike na kutunza afya yake. Pia anakuwa na nafasi ya kuwahudumia watoto aliowazaa kwa nafasi kubwa na anaweza kufanya kazi zingine za kujenga uchumi wa familia na Taifa.
“Mwanamke mwenyewe pia anapaswa kuthamini maisha yake na wanaume wajue mimba ni ya mama na baba,” anasema Mlay.
Kauli ya Waziri wa Afya
Kwa kuwa malalamiko ya wanawake wengi wanashindwa kupata taarifa kuhusu uzazi wa mpango na uzazi salama kutokana na  umbali wa zahanati, hivyo huamua kujifungulia nyumbani na kwa wakunga wa jadi, Mwananchi lilimuuliza Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuhusu hatma ya wananchi hao.
Akizungumzia Sera na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia lengo lake la kujenga zahanati katika kila kijiji, kituo cha afya kila kata na hospitali katika kila wilaya na kuzipatia vifaatiba, dawa na watumishi, kinyume na Kata ya Kinyeto yenye zahanati moja inayohudumia vijiji vinne anasema;
“Kazi ya Wizara ya Afya ni kusimamia utekelezaji wa Sera, kutoa miongozo pamoja na kusimamia ubora wa huduma zinazotolewa.”
“Tutaendelea kushirikiana na tamisemi kupitia kwenye Halmashauri kuhakikisha wananchi wa kata hiyo wanapata huduma bora za afya ikiwamo kupeleka watumishi, fedha za dawa, vifaatiba, fedha za uendeshaji na kuhakikisha elimu inatolewa kuhusu umuhimu wa kupanga uzazi,” anasema Ummy Mwalimu.

No comments:

Post a Comment