Kuna wenye blogu (mitandao binafsi ya intaneti) wanaoandika na kushiriki mijadala. Mmoja anasema, “Nimechapisha makala kwenye blogu yangu lakini kiu yangu haijakatwa; ni mpaka nipate fursa ya kufanya kazi nikiwa mwandishi wa habari katika kampuni ya magazeti.”
Mwingine alitaka kujua “…unaanzia wapi ili uwe mwandishi wa habari? Uwe na nini na uweje? Mhariri wa Jamii aliongeza hapo kwamba, wanaotoa majibu wasiishie kwenye hisia na utashi, unyofu na udadisi au utafiti.
Pamoja na yote hayo, waeleze kwa ukamilifu sifa walizotakiwa kuwa nazo na walizokuwa nazo; na wanazofikiri zilisababisha wawe chaguo la mwajiri.
Hapa ninawaletea majibu kutoka kwa waandishi wanne (4) walioko kazini. Wanatoa ushauri lakini pia wanaeleza kipi kinahitajika ili uwe mwandishi.
Mwandishi wa kwanza: Ni muhimu kuwa na utashi tangu mwanzo; kama wewe Mhariri wa Jamii ulivyosema ulitaka kuwa mwandishi au mwalimu tangu ukiwa madarasa ya chini shuleni.
Lakini kwa mazingira ya sasa inabidi utafute elimu itakayochonga utashi na ndoto yako. Hizi ni enzi za vyeti; siyo kutaka tu. Vyuo vya habari vipo vingi nchini. Uliza wanaofahamu watakuelekeza ni kipi bora. Usome. Ufanye mazoezi. Ukihitimu utafute kazi.
Hivyo ndivyo nilivyofanya. Lakini sipo magazetini. Ninafanya kazi katika kituo cha redio ambako uandishi ni uandishi tu; tofauti ni katika mfumo wa kuwasilisha.
Mwandishi wa pili: Nilichukua gazeti nililokuwa nikipenda kusoma. Nikawa ninafuatilia majina ya waandishi na kile wanachoandika. Nikaona wawili wananikosha. Nikasema: Nitakufa na hawa.
Unafahamu, uandishi wa habari una mdundo. Ni kama ngoma. Unasoma habari huku ukisikia mdundo kifuani wa hiki na kile. Vitu vipya. Unarejea jina la mwandishi na kujisemea moyoni, ‘huyu bwana ananifaa. Ningeandika kama huyu?’
Nilitaka kuwa mwandishi nikiwa Kidato cha Sita. Kwa utaratibu wangu huo, nikajikuta ninaendelea kuzama katika ndoto na wakati wote nikichochewa hasa na habari za uchunguzi; vile vitu visivyofahamika kwa watu wengi. Nilishindwa kwenda Chuo Kikuu. Wakati huo hakukuwa na vyuo vikuu nchini vinavyofundisha uandishi wa habari. Nikasema siendi huko. Nikajiunga na chuo cha uandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Nilipohitimu nikaomba na kupata kazi katika magazeti ya serikali. Nikawa mwandishi. Nilikwenda chuo kikuu miaka sita baadaye na wakati huo nikiwa ninaanza kuitwa ‘mwandishi mzuri.’ Nilipomaliza chuo nikarejea kazini. Ukitaka, inawezekana.
Mwandishi wa tatu: Tangu shule ya msingi nilikuwa na tabia ya kushindana katika kuandika insha. Nilishinda mara nne. Nikawa ninajiuliza: Hii si kama uandishi wa habari? Baada ya kuhitimu Kidato cha Sita nikajiunga na Chuo cha Ualimu.
Nikiwa mwalimu nikawa nasoma magazeti mpaka wenzangu wakawa wananitania kwa kuniita mwandishi. Ni hapo nilipoanza kuandika na kupeleka maandishi yangu kwa wahariri. Niliandika lakini hakuna hata moja iliyochapishwa.
Baada ya miezi sita, andishi langu moja likatoka kwenye gazeti la Uhuru. Machozi yalinitoka. Nilikuwa ninaandika kwa lugha ya Kiingereza pia. Nyingine mbili zikatoka Daily News. Nikasema Mungu akupe nini. Nikawa ninaandika na maandishi yangu yanachapishwa huku nikilipwa.
Siku moja nikaletewa barua kuwa ninaitwa na mhariri. Nilipokwenda akaniuliza ninafanya kazi gani. Nikasema ualimu. Akasema ninaonekana ninaweza kufundishika; anataka kuniajiri. Nikaacha kazi na kwenda kufanya kazi hiyo. Miaka minne baadaye nikateuliwa kwenda kusomea uandishi nchini Hungary. Bado niko katika uandishi wa habari.
Mwandishi wa nne: Ninachoweza kuchangia ni kwamba, waelewe kuwa mwandishi wa magazeti si kitu kikubwa kama kuwa mwandishi wa Injili. Injili iliandikwa na waandishi wa habari wanne kutoka maeneo tofauti wakiripoti maisha ya Yesu Kristo.
Lakini ajabu ni walichoandika wote kilifanana. Cha ajabu zaidi hakukuwa na chuo cha uandishi wa habari enzi hizo. Naona hata wewe umeduwaa kwa jibu lililohusisha Injili.
Kifupi, hao wanaotaka kuwa waandishi wa habari tayari ni waandishi. Kuandika katika blogu ni sawa na kuandika katika Biblia, Newsweek, MCL, The Guardian nk.
Wanachoandika ndicho kitafanya vyombo viwe na majina makubwa kama MCL na ndipo kiu yao itakapoisha. Dk John Haule (Health Writer).
Majibu haya na mengine saba ambayo yametufikia na namba za simu za watoa majibu, yatapelekwa kwa waliouliza maswali ili wapate fursa ya kuwasiliana nao.
No comments:
Post a Comment