Umri wake wa miaka 62 haumzuii Anna Pallagyo mkazi wa kijiji cha Mulala, wilaya ya Meru mkoani Arusha kutabasamu na kuonyesha umahiri wa kuimba na kucheza ngoma ya kabila la Wameru, anapopata wageni nyumbani kwake.
Wakati wengine wanaona vitu vya asili ni vya kawaida, Anna vinamuongezea heshima na hivyo kupokea watalii wa ndani na nje ya nchi wanaotamani kuviona.
Wakati wote uso wake umejaa tabasamu huku sauti nyororo ya nyimbo za asili ikiwa ndiyo inayosikika kinywani mwake. Namna anavyocheza wakati akiwakaribisha wageni kunamfanya aendelee kutajirika kwa sababu, wakiondoka watarudi tena.
Mwanamke huyo mjane anadhihirisha kuwa katika maisha hakuna jambo linaloshindikana kama ukiweka nia na malengo. Utalii wa Utamaduni ndio ulioinua maisha yake. Mama huyu ambaye elimu yake ni darasa la saba, hakuwa kupata ujuzi wowote zaidi ya kujihusisha na kilimo duni ili aweze kuhudumia familia yake yenye watoto sita.
Kwa sasa anaongoza kikundi cha utalii wa utamaduni, Agape Mulala Cultrual Toursim chenye jumla ya wanachama kumi, amefanikiwa kujenga nyumba ya ghorofa yenye vyumba saba na pia yupo kwenye mchakato wa kumalizia ujenzi wa mradi wa shule ya sekondari.
Anna alianza harakati za kujikomboa kutoka kwenye wimbi la umaskini mwaka 1996 alipopata mitaji wa Sh50, 000 kutoka taaisisi ya mikopo ya Pride.
Alianzisha mradi ya kununua maziwa mtaani na kuuza pamoja na kusindika kwa ajili ya kutengeneza jibini.
Baada ya muda alikutana na mradi wa Haifer International ambao ulimpatia mtaji wa ng’ombe wa maziwa, ndio ukawa mwanzo wa mafanikio.
“Ilipofika mwaka 1998 kuna Waholanzi walikuja kwenye maeneo ya Meru wakiangalia maeneo yanayoweza kuwa sehemu ya kivutio cha utalii wa asali.
Wakati akiendelea na shughuli zake, alihamasisha kina mama na wanakijiji kupanda miti ili kufanya mazinmgira yawe mazuri.
“Mwaka 1998, Waholanzi wakishirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) walifija kwenye maeneo yetu wakiangalia sehemu ambayo inaweza kuwa kivutio cha utalii wa utamaduni, ndipo wakasikia habari kuhusu mimi na yule ng’ombe wa maziwa wakaamua kunichagua ili nianzishe kikundi.”
Kilichowavutia zaidi ni namna alivyotengeneza jibini kwa kutumia vifaa duni, ndipo wakamshauri kuanzisha kikundi.
“Tutaanza kikundi cha watu watano na ilikuwa chini TTB ambao walinipatia mafunzo ya namna ya kupokea watalii.”
Kuanzia miaka ya 2000 na kuendelea, kikundi kilianza kupokea wageni mbalimbali ambao walikuwa wanafika kwa lengo la kujua utamaduni wetu na historia ya kabila la wameru.
“Lile shirika liliIonipa mtaji wa ng’ombe na wenyewe wakawa ni sehemu ya kunitangaza kwa hiyo watalii wakawa wanakuja kwa lengo la kumwona yule ng’ombe kwa kweli maisha yaliianza kubadilika kwangu na kina mama wenzangu,” Anasema Mama Pallangyo akiwa na uso wa tabasamu, huku akicheza ngoma ya kabila la Wameru.
Agape Cultural Group wanafanya nini
Pamoja na utalii wa utamaduni kikundi kinajihusisha na shughuli mbalimbali za usindikaji maziwa na kutengeneza jibini ya aina tofauti, ufugaji wa nyuki kwa kutumia mizinga ya asili, kahawa, batiki, shanga za kimasai na kuchora picha.
Anasema wageni wakifika pamoja na kupata huduma za utamaduni wa utalii asili, pia baadhi yao hununua vitu vinavyotengenezwa na wanachama kwa kutumia zana za asili hivyo wana kikundi hujipatia fedha ya ziada.
Kwa siku mtalii analipa kati ya dola za kimarekani 20 hadi 30 ili kuweza kupata huduma zao ikiwemo chakula na mahitaji mengine.
Kikundi pia kimewanufaisha zaidi ya watu 2,500 ambao wanaishi maeneo ya jirani kwa njia mbalimbali, mfano imesaidia ujenzi wa zahanati, shule ya msingi na sekondari.
Kwa sasa wapo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha ujenzi wa shule ya sekondari wakishirikiana na mfadhili mmoja kutoka Ujerumani ambaye alifurahishwa na jitihada zao na kuamua kuwekeza kwao.
Anasema mwanzo watalii walikuwa wakija wanaondoka kutokana na uhaba wa vyumba vya kulalaza, labda mtalii aje na tenti lake ndio atalala. Kutokana na hilo kikundi kilikuwa kinakosa mapato kwani badala ya mtalii kulala siku mbili au tatu analazimika kuondoka.
Ila baada ya mafanikio na mtaji kuongezeka kwa sasa kikundi kinamalizia ujenzi wa ghorofa ya nyumba saba, ambapo tayari vyumba vinne vimekamilika na wageni wameanza kuvitumia.
Alisema, vyumba vina uwezo wa kulaza watalii wanne hadi sita na itakapomalizika itakuwa na uwezo wa kulaza watu zaidi ya 20 kwa siku.
No comments:
Post a Comment