Upinzani umekataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi wa majimbo uliompa ushindi mkubwa Rais Nicolas Maduro na chama chake kinachoelemea siasa za mrengo wa kushoto, wakiitisha maandamano kudai kuhisabiwa upya kura.
Hata kabla Tume ya Uchaguzi kutangaza matokeo hayo mapema leo, tayari muungano wa upinzani ujiitao Mshikamano wa Kidemokrasia ulishatoa indhari kwamba ulikuwa na taarifa za tume hiyo kuyachezea matokeo halisi ya kura.
Mkuu wa kampeni wa muungano huo, Gerardo Blyde, aliwaambia waandishi wa habari mjini Caracas kwamba si raia wa nchi hiyo wala wenzao duniani kote walio tayari kuukubali kile alichokiita mchezo wa kutunga.
"Tunaionya serikali hii kwamba matokeo hayo hayawiani na tuliyonayo, tunakata kuiambia serikali mambo mengi kwenye tamko hili. Kwanza, wanajuwa kuwa wao sio wengi na nchi hii na watu wa Venezuela na dunia inajuwa hatuyatambui matokeo yaliyotolewa leo na Tume ya Uchaguzi ya Taifa," alisema Blyde.
Mwenyekiti wa tume hiyo ya uchaguzi, Tibisay Lucena, alitangaza kwamba chama cha kisoshalisti kinachotawala Venezuela kimejizolea majimbo 17 na upinzani ukiwa na sita tu, katika uchaguzi wa jana ambao asilimia 61 ya wapigakura walishiriki.
Ushindi huu mkubwa kwa chama cha Maduro umewashangaza wapinzani na wachunguzi wa maoni, ambao walitabiri kuwa upinzani ungelishinda kwa wingi wa asilimia 44.7 dhidi ya 21.1 za chama tawala.
Maduro awakosoa wapinzani na Marekani
Mara tu baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Rais Maduro aliwahutubia wafuasi wake akizikosoa tafiti za maoni ambazo alisema zilibuniwa na serikali ya Marekani na washirika wake.
"Mahudhurio ya asilimia 61.4 kwenye uchaguzi Washington, data ya pili: katika wakati huu tuna majimbo 17, ushindi wa wazi kabisa. Wafuasi wa Chavez wameukata uchaguzi. Wameyakata majimbo 17. Upinzani wanachukuwa matano, tangu sasa nasema kuwa nayatambua matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa," alisema Maduro.
Viongozi wa upinzani wanalalamikia wizi mkubwa uliofanywa na chama tawala kwa kushirikiana na tume ya uchaguzi na wameitisha maandamano makubwa hivi leo, wakidai kuhisabiwa upya kwa kura. Hata hivyo, hadi sasa, hakuna ushahidi waliotoa kuthibitisha madai yao.
Baada ya kujiona kuwa hawataweza kumuondoa Maduro kwa maandamano ya mitaani, wapinzani wengi nchini humo sasa wanatarajia vikwazo vya kiuchumi kutoka mataifa ya kigeni ndiyo pekee vitakavyomuangusha.
Tayari utawala wa Trump wa Marekani umeshawawekea vikwazo maafisa wa serikali, akiwemo mwenyewe Rais Maduro, huku ikitarajiwa kuwa Umoja wa Ulaya nao huenda ukachukuwa hatua kama hiyo.
No comments:
Post a Comment