BoT hutoa ripoti hiyo kila mwezi ili kuwataarifu wadau wa uchumi na wananchi kwa ujumla mwenendo wa kiuchumi, lakini haijafanya hivyo kuanzia Juni hivyo kuibua maswali miongoni mwa wadau wanaozitumia taarifa hizo kwa shughuli zao.
Mkurugenzi wa Uchumi wa BoT, Johnson Nyela alisema maandalizi ya kukamilisha ripoti hizo yanaendelea kwa kuzishughulikia changamoto zilizopo.
“Nia yetu haiendani na hali halisi. Tungependa ripoti ya Januari kwa mfano itoke mwishoni mwa mwezi huo lakini hali halisi ni tofauti. Upatikanaji wa taarifa unasumbua,” alisema mkurugenzi huyo.
Nyela alisema taarifa ya Juni inakamilishwa na muda wowote itatoka wakati ile ya Julai bado inaandaliwa.
Ripoti hiyo ya kila mwezi huwekwa kwenye tovuti ya BoT ama mwishoni mwa wiki ya pili au mwanzoni mwa wiki ya tatu ya mwezi unaofuata, yaani ripoti ya Januari inawekwa muda huo Februari.
Lakini ripoti ya mwisho iliyopo kwenye tovuti ya BoT iliwekwa Juni ikitathmini mwenendo wa uchumi ulivyokuwa Mei. Kwa maana nyingine, ripoti ya mwezi wa kufunga mwaka wa fedha 2016/2017 haikutolewa pamoja na miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu wa fedha, 2017/18.
Baadhi ya wakosoaji wanatuhumu kuwa kutotolewa kwa taarifa hiyo kwa muda mrefu ni mwanzo wa uendeshaji uchumi kwa kificho baada ya Tanzania kujiondoa kwenye Mpango wa Uwazi Serikalini (OGP).
Kiongozi mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook, akiituhumu Serikali kuwanyima wananchi taarifa kuhusu uchumi.
“Kwa kuchelewa huku, taarifa itakayotoka lazima itakuwa ya kupikwa,” amedai mbunge huyo wa Kigoma Mjini.
Kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, BoT inalazimika kutoa taarifa za kila mwezi, robo mwaka na mwaka.
No comments:
Post a Comment