Monday, October 2

Mwinyi ashangaa kuendelea mauaji yaliyomfanya ajiuzulu


Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amesema hakuna sababu ya kiongozi kujiuzulu baada ya kuona mauaji yanaendelea licha ya kusababisha yeye ajiuzulu wakati alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Mwinyi alimuandikia Rais wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere barua ya kujiuzulu uwaziri huo Julai, 1976 baada ya kutokea mauaji mkoani Shinyanga.
Uamuzi wake ulimjengea heshima kiasi cha kupata nafasi ya kuongoza nchi mwaka 1985 na kuwa Rais wa Awamu ya Pili.
Lakini, pamoja na kujiuzulu kwake mauaji hayajakoma zaidi ya kuchukua sura tofauti; mauaji ya vikongwe, watu wenye ulemavu wa ngozi, uchunaji ngozi na hivi sasa yanafanyika kwa kutumia silaha kali.
Rais huyo mstaafu anaona njia ya kukabiliana na mauaji ni kuyashughulikia badala ya viongozi kuwajibika kwa kujiuzulu.
Akizungumza jana katika kilele cha siku ya wazee duniani, Mwinyi alisema bado inasikitisha kuona jambo lililomfanya aachie ngazi linaendelea katika dunia ya leo, akisema ni aibu na fedheha kwa Taifa kama Tanzania.
Alisema hayo wakati Taifa likipitia kipindi ambacho wananchi wanauawa na watu ambao hawajaweza kupatikana na wala kujua lengo lao kiasi cha kupata jina la “watu wasiojulikana”.
Mwinyi aliitaka Serikali kupambana na wauaji ikiwamo wanaowaua vikongwe kwa sababu za macho yao mekundu kwa kuwa mkono wake ni mrefu na ikiamua inawezekana.
Pia, alivitaka vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu kwa Watanzania ili waache mtindo wa kuwaua watu wasiokuwa na hatia, hasa vikongwe.
Vilevile, aliitaka Serikali kutunga sheria ya wazee haraka ili iwalinde badala ya kutegemea sera na kauli katika utoaji huduma ambazo mwisho wa siku huishia kwenye makaratasi.
Awali, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ambaye pia anahusika na masuala ya wazee, alisema Serikali imeweka kipaumbele kwa wazee na haitasita kuwahudumia kila inapobidi ikiwamo kuwapatia matibabu ya bure.
Ummy alisema kwamba hadi sasa wazee wapatao 135,415 wameshatambuliwa na zaidi ya 200,000 wamepatiwa vitambulisho vya bima kwa ajili ya matibabu hayo.
Alisema Serikali inapeleka fedha kila mwezi katika kambi 17 za wazee pamoja na kuwanunulia bajaji 10 kwa ajili ya kuwahudumia. Pia, alisema Serikali imenunua majiko matano ya kupikia ili kupunguza matumizi ya kuni.
Waziri huyo alisema kambi hizo zina wazee 489 ambao hawana ndugu wa kuwatunza.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa mtandao wa mashirika ya wazee, Sebastian Bulegi alimuomba Mzee Mwinyi kufikisha maombi yao kwa Rais Magufuli, akisisitiza kilio kikubwa cha wazee ni kutaka uwakilishi katika vyombo vya uamuzi kama Bunge.
Bulegi aliyataja mambo mengine kuwa ni sheria itakayoendana na Sera ya Wazee ya mwaka 2003, huduma bora bila malipo kwa kuwa bado wanasumbuliwa, mauaji ya kikatili na malipo ya pensheni kwa wazee kwa kuwa wanaolipwa ni asilimia nne tu ya wazee ambao walikuwa watumishi.
Aliongeza kwamba hadi sasa Tanzania ina wazee wanaokadiriwa kuwa milioni 2.5 huku wengi wao wakiwa katika hali duni ya maisha.

No comments:

Post a Comment