NCHI wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), leo zinasherehekea miaka 72 tangu kuanzishwa kwa umoja huo mwaka 1945 muda mfupi baada ya vita ya pili ya dunia.
Wakati UN inaadhimisha umri huo, bado ina deni kubwa la kuhakikisha uwiano chanya wa kiuchumi baina ya mataifa yaliyoendelea na yanayoendelea.
Pamoja na kutekeleza baadhi ya maazimio yake yaliyosababishwa kwa kuundwa kwa umoja huo kama vile kupinga ukandamizaji ulipokuwa ukitekelezwa na mataifa makubwa yaliyoyatawala mataifa machanga hususani mataifa ya Afrika, bado kumeendelea kuwapo na pengo kubwa baina ya mataifa hayo ikiwamo kuendelea ukoloni mamboleo.
Tatizo la umasikini limeendelea kuyatafuna mataifa machanga hasa yale ya bara la Asia na Afrika ikiwamo Tanzania.
Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watu wanaoishi katika umasikini uliokithiri imepungua kutoka watu bilioni 1.9 mwaka 1990 hadi kufikia milioni 836.
Wastani wa umasikini katika nchi zinazoendelea unaonesha kuwa mtu mmoja kati ya watano anaishi kwa chini ya Dola 1.25 (sawa na Sh 2,500) kwa siku na wale wanaoishi chini ya Dola mbili wakiwa ni takribani bilioni 2.2.
Nchi zilizo Kusini mwa Bara la Asia na Kusini mwa Jangwa la Sahara ndiyo zimekuwa waathirika wakuu wa janga la umasikini.
Umasikini huu uliokithiri umechangiwa na mambo mengi ikiwamo ukosefu wa chakula cha uhakika katika maeneo mengi ambapo hadi kufikia mwaka 2016 asilimia 12.9 ya watu wote duniani walikabiliwa na lishe duni ikiwa ni sawa na wastani wa mtu mmoja kati ya tisa.
Hii inamaanisha kuwa jumla ya watu milioni 795 wanakabiliwa na lishe duni duniani kote hali inayochangia kutoshiriki katika shughuli mbalimbali hususani za uchumi.
Bara la Asia ndilo linalokabiliwa na idadi kubwa ya watu wenye njaa likiwa na theluthi mbili ya watu wote wenye njaa duniani, huku nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara zikiwa na wastani mkubwa wa watu wenye lishe duni ambapo kati ya watu wanne mmoja anakabiliwa na tatizo hilo.
UN inapaswa kuhakikisha inapunguza tatizo hili kwa kuwezesha kilimo bora ili kupunguza idadi ya wakulima wanaotumia njia duni za kilimo.
Hadi sasa wakulima wadogo wanaotegemea mvua kuzalisha mazao ya kilimo wanachangia asilimia 80 ya chakula chote duniani zaidi katika nchi zinazoendelea.
Katika malengo 17 ya UN miongoni mwa mambo yaliyoorodheshwa ni pamoja na kuwekeza kwa wakulima wadogo kama moja ya njia bora za kuhakikisha kuwapo kwa usalama wa chakula na lishe kwa watu masikini na uzalishaji wa chakula kwa mahitaji ya ndani na soko la dunia.
Ukosefu wa nishati ya uhakika ni miongoni mwa vikwazo si tu katika maisha ya kawaida bali hata kwa shughuli za kiuchumi, zaidi ya watu bilioni 1.3 duniani kote hawana huduma ya umeme.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali zinaonesha kuwa watu bilioni tatu wanategemea kuni, mkaa, makaa ya mawe au kinyesi cha wanyama kama nishati kuu.
Ukosefu wa ajira ni janga la dunia na limekuwa likiongezeka kote duniani ambapo kiasi cha watu milioni 202 wenye umri wa kufanya kazi hawana ajira kati yao vijana wakiwa milioni 75.
Sekta ya viwanda ambayo ni miongoni mwa waajiri wakuu bado imeendelea kusuasua katika nchi nyingi hususani za Afrika kutokana na vikwazo vya ukosefu wa miundombinu na nishati ya uhakika, wakati nchi zilizoendelea asilimia 98 ya bidhaa zake hupitia viwandani hali ni tofauti kabisa kwa nchi zinazoendelea ambapo bidhaa za viwandani ni chini ya asilimia 30.
Taarifa zinaonesha kuwa wastani wa kipato kwa nchi zinazoendelea kati ya mtu na mtu kimekuwa ni kikubwa ambapo pengo kati ya walionacho na wasionacho limeongezeka kwa asilimia 11 kati ya mwaka 1990 na 2010.
Ushiriki wa watu katika shughuli mbalimbali za maendeleo umekuwa ukitatizwa na migororo ya vita hususani kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Hadi mwaka 2014 kulikuwa na jumla ya wakimbizi milioni 13 wanaohudumiwa na Shirika la Wakimbizi (UNHCR).
Migogoro hii imesababisha madhara makubwa sehemu mbalimbali hadi mwaka 2011 kiasi cha watoto milioni 28.5 waliacha shule kutokana na migogoro mbalimbali, licha ya kuwa hakuna takwimu zilizotolewa hivi karibuni ni wazi kuwa idadi hiyo imeongezeka maradufu kutokana na kuongezeka kwa machafuko katika maeneo ambayo wakati huo yalikuwa na usalama kama vile Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali na Syria.
Pamoja na matatizo hayo lukuki, bila shaka UN wanaadhimisha miaka 72 wakifahamu fika kuwa dunia inakabiliwa na tishio la ugaidi kutokana na kuongezeka kwa makundi kama vile Al Shaabab, Boko Haram na mengine mengi.
No comments:
Post a Comment