Wakati mtandao huu ulipoanza kukua na kushika hatamu, ndipo taasisi binafsi na kampuni za kibiashara zilipoanza kuwekeza kwenye usalama ili kulinda maslahi yao mbalimbali kwa njia ya mtandao kwa kutengeneza vifaa, programu, mafunzo na mengine mengi .
Unaweza kukuta uwekezaji mkubwa wa usalama kwenye taasisi za kiserikali na zile binafsi ili kulinda maslahi Fulani, lakini hili unaweza usilikute katika idara moja tu ya chuo kikuu ambayo pengine ina kazi muhimu ya kutoa wanataaluma.
Katika taasisi kama za kiserikali na kwingine, binafsi ni vigumu kukuta mtu akiingia na kifaa binafsi kama simu, kompyuta na vinginevyo na kutumia huduma za mawasiliano, lakini hili ni jambo la kawaida kwenye vyuo vikuu vingi ambapo wanafunzi na wadau wengine utawakuta na vifaa kila eneo wakivitumia bila shida wala hofu yoyote .
Hali hii ya kulegalega kwa taasisi za elimu ya juu kuwekeza kwenye eneo hili, ndio matokeo ya uhalifu mwingi wa njia ya mtandao unaotokea ndani ya vyuo vikuu sehemu mbalimbali dunani.
Wiki iliyopita kulikuwa na taarifa za kuingiliwa kwa tovuti ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, tukio lililofanywa na watu wanaojiita “ Tanzania hackers “ kwa lengo la kulazimisha kupatiwa ajira.
Binafsi sijajua kama uhalifu wa aina hii katika tovuti za vyuo nchini Tanzania ni wa kwanza au la, sina takwimu sahihi lakini kwa ufupi uhalifu huu unaitwa kitaalamu kwa jina la ‘Hijacking ‘ yaani mtu au kundi la watu kuteka na kushikilia tovuti au mtandao wa taasisi nyingine kwa nia ya kulazimisha kutimiziwa mambo fulani.
Hata hivyo, ni vizuri tukio kama hili lililotokea ndani ya taasisi ya elimu ya juu litushitue Watanzania.
Kwa mtu wa kawaida, akiangalia taasisi kama chuo anaweza kudhani ni sehemu ya watu kwenda kupata mafunzo na kujiondokea.
Kuna mengi zaidi ambayo kama wahalifu wakifanikiwa kuyafikia yanaweza kuleta madhara kwa taasisi, mtu mmoja mmoja, Taifa na wadau wengine wanaoshirikiana na chuo husika.
Pia, ni vizuri kuwa makini kusambaza udhaifu unaojitokeza katika vyuo vyetu kwa sababu wahalifu wa kimataifa hutumia fursa kama hizi kuingilia taasisi za elimu kwa lengo la kufanya uhalifu kwingine.
Kilichopo ni kuwa wanaweza kutumia taasisi hizi kama madaraja ya kushambulia maeneo mengine mbalimbali yenye maslahi kwa Taifa moja kwa moja.
Naomba nieleweke kwamba ninapoongelea uhalifu kwa njia ya mtandao sio ule unaohusu fedha pekee. Kuna aina nyingi kama vile kuvujisha siri, kuiba kazi za wanafunzi au wanataaluma, kuiba nywila, kuiba rekodi za watu kama ni za afya au chochote.
Tunaweza kufanya nini kudhibiti uhalifu huu kama ulivyotokea katika chuo hiki?
Kwanza, taasisi zote za elimu ya juu ziwe na miongozo ya matumizi sahihi ya vyombo vya mawasiliano. Hii inaanzia kwa mwanafunzi na mtumishi mmoja mmoja
Mwongozo huu hata kama utatofautiana kutoka idara moja hadi nyingine, ni lazima kwa upande mwingine uendane na Sheria ya Ulinzi wa Mawasiliano nchini.
Kwa mfano, wanafunzi na watumishi wote walazimishwe kuchukua programu za matumizi kupitia tovuti za chuo na masuala yote yanayohusu Tehama wawatumie wataalamu wa chuo.
Aidha, vyuo vyote viwe na ‘backup’ ambayo itawezesha huduma kurudi kama kawaida ndani ya muda mfupi kama ikitokea mtandao wa chuo umevamiwa au kumetokea hitilafu yoyote. Mara nyingi hii huweza kurudisha huduma chini ya dakika 30.
Huduma nzuri za ‘backup’ ni kuwekeza katika kuhifadhi vitu kwa njia ya mtandao inayoitwa CLOUD. Hii hii itawezesha shughuli mbalimbali kuendelea kutokea popote duniani.
Uhalifu huu uliotokea Chuo Kikuu Huria, uwe changamoto kwa taasisi za elimu ya juu na wadau wengine kuanza kufikiria sasa kufanya uwekezaji mkubwa katika idara zao za Tehama na hata kutumia wataalamu wa ndani kama wale wa BUNI au KINU ili kupata programu bora zaidi.
Tuna vijana wengi walioiva katika uwanja huu wa Tehama chini ya ulezi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech). Tuwatumie ili kilichotokea Chuo Kikuu Huria kisijirudie katika taasisi nyingine za elimu.
No comments:
Post a Comment