Hilo ni eneo ambalo watafiti wa Kijerumani waliondoka na visukuku (mabaki) vya mijusi mikubwa (dinosaria) wanaodaiwa kuishi duniani kati ya miaka milioni 1.3 hadi milioni 65 iliyopita.
Mabaki ya visukuku hivyo yalichukuliwa na watafiti hao katika kitongoji cha Tendaguru (wenyeji huita Tendegeru) baada ya mhandisi wao, Bernhard Sattler kubaini uwapo wa mabaki hayo ya mifupa ya mijusi waliokuwa na urefu wa zaidi ya futi 100 wanaokadiriwa kuwa na uzito wa tani zaidi ya 80 kila mmoja.
Hata hivyo, kabla na baada ya kufika katika eneo lenyewe kuna mambo zaidi ya matano yatakayokushangaza ikizingatiwa kwamba dunia ya sasa inaongozwa na uchumi unaotegemea sekta mbalimbali ikiwamo ile ya utalii.
Mmoja wa vijana wanaopeleka watafiti eneo la Tendaguru akionyesha mabaki ya mijusi yaliyogeuka vijiwe vidogo vidogo katika sehemu hiyo.
Kutoka Lindi mjini hadi Mkwajuni ni umbali wa takriban kilomita 70 ndipo unapoikuta barabara ya changarawe inayokupeleka mpaka kilipo kijiji hicho ambacho kwa usafiri wa pikipiki (maana hakuna mabasi yaendayo huko) ni mwendo wa takriban dakika 45.
Kisha, kutoka kijijini hapo hadi mlima Tendaguru mahala yalipogunduliwa mabaki ya mijusi hao na Sattler na wenzake kati ya mwaka 1907 hadi 1913 ni umbali wa kilomita 38 kukiwa hakuna barabara isipokuwa njia za waokota kuni na wanyama wa porini.
Baada ya kugundulika kwa mabaki hayo, Wajerumani hao waliyachukua na kuyasafirisha hadi nchini mwao ambako yaliunganishwa na kuhifadhiwa kwenye makumbusho maarufu ya vivutio vya kale inayoitwa Naturkunde iliyopo Berlin nchini humo.
Hata hivyo ukiwauliza wenyeji wa kijiji hicho mara zote jibu lao ni jepesi, “tumesahaulika” wakimaanisha kwamba hakuna juhudi zozote zilizofanywa na mamlaka za kiserikali kuhakikisha kwamba Tendaguru inapata barabara ya maana ikilinganishwa na umaarufu wa mijusi waliochukuliwa eneo hilo.
Kutokana na umuhimu wa eneo la Tendaguru katika utafiti wa mambo kale na utalii wa vivutio vya asili kunakotokana na uvumbuzi uliofanywa na watafiti wa Kijerumani, barabara ya kutoka kijijini hadi eneo husika (yalipogunduliwa mabaki ya mijusi hao), zahanati na alama au jengo katika eneo husika vilipaswa kuwapo miaka mingi.
Chungu kilichotumika kwa tambiko kilichotelekezwa Tendaguru
Unafikaje Tendaguru?
Hakuna barabara inayokwenda Tendaguru kutoka kijijini umbali wa kilomita zaidi ya 38. Kinachoweza kumfikisha mgeni anayetaka kwenda sehemu hiyo ni ama kuuliza kwa wenyeji anapowakuta mashambani wakiwajibika au kuwaomba msaada ili wampeleke.
Katika umbali wa kilomita 38 ambao ni mwendo wa nusu saa kwa mujibu wa mwendesha pikipiki wa sehemu hiyo Said Kiwingo, utatumia saa nzima na nusu au saa mbili ukipita katika mashamba, vichaka na mapori yenye miti minene inayodaiwa kuwa na wanyama wakali.
Kwa mujibu wa Kiwingo, nyakati za mvua za masika eneo la Tendaguru halifikiki mpaka mvua zinapokwisha, hata baiskeli haiwezi kupita sehemu hiyo kutokana na baadhi ya maeneo (ya mashamba na vichaka) kuwa na udongo wa mfinyanzi.
“Kama kuna mahala kusikojulikana basi ni huku. Leo (siku aliyompeleka mwandishi wa makala haya sehemu hiyo) ni zaidi ya miezi miwili hakuna mtu aliyekuja huku, mara ya mwisho tuliwaleta watafiti fulani hivi Wazungu na Mwafrika,” anasema Kiwingo.
Kiwingo anasema mara nyingi watu wasiokuwa na usafiri hutumia siku nzima wanapokwenda Tendaguru eneo ambalo pia wenyeji hulitumia kwa matambiko na ukataji miti na nyasi za kuezekea nyumba na mabanda ya mifugo pamoja na maghala ya vyakula.
Mwananchi huyo anasema kuwa, kijijini wanaamini kwamba haitajengwa barabara iendayo Tendaguru kwa sababu hata viongozi wa wilaya na mkoa kutembelea eneo husika ni nadra.
“Huku wamepasusa, nakumbuka mbunge tu ndiye alikuja wakati fulani na nasikia na mkuu wa mkoa lakini mimi sikuwapo. Ila sijawahi kuwasikia wakubwa wengine ikilinganishwa na umuhimu wa eneo hilo ambalo kama wangekuwa wanakuja barabara ingekuwa tayari ishajengwa,” anasema Kiwingo.
Nelson Ndelitete (71) anasema hoja ya barabara haijawahi kutatuliwa licha ya kwamba siku za nyuma walikuwa wakiizungumza kila walipopata ugeni wa viongozi wa kiserikali.
“Hili (la barabara) ni kama kichefuchefu, hakuna hata kiongozi aliyekuja hapa akaahidi na kutekeleza. Hiyo (barabara-isiyokuwapo) uliyoiona ndiyo inatumiwa na kila mtu, kufika kwenyewe ni shida. Kama huna nia ya dhati huwezi kwenda huko,” anasema.
Ndelitete anasema wakazi wa kijiji hicho wanaokwenda Tendaguru mara nyingi ni watu wa matambiko ambao hata hivyo katika miaka ya karibuni wamepungua kwa kiwango kikubwa.
Ni vichaka na misitu
Wakati ukishangaa kutokuwapo barabara inayotoka kijijini kwenda lilipo eneo alilopatikana dinosaria zaidi ya miaka 110 iliyopita, hata ukifika katika sehemu hiyo hakuna alama yoyote iliyowekwa kuonyesha kuwa ndipo mabaki ya mjusi mkubwa yaligunduliwa na watafiti. Viashiria pekee vilivyopo ni vyungu na mabaki ya vitu kama masufuria na nguo zilizochanika ambazo kwa mujibu wa wenyeji vinaachwa na watambikaji.
“Hivyo vyungu wazee wetu huenda huko wanapojisikia kwenda kufanya matambiko yao, lakini hakuna kitu pale kilichowekwa kama alama. Hata sisi hapa kijijini tumepakariri kwa sababu tumerithishwa kizazi na kizazi na wazee wetu kuwa hapo ndipo huyo mjusi aliokotwa,” anasema Ndelitete.
Anasema misitu na vichaka vinavyozunguka eneo hilo vinaashiria namna eneo lilivyotelekezwa na mamlaka husika, huku uchache wa wananchi wanaofika sehemu hiyo ukichangia kulifanya lionekane kama lililohamwa miaka mingi.
Ndelitete anasema licha ya wananchi wachache wa kijiji hicho wanaokwenda kwa matambiko, waokota kuni na wakata nyasi, mara moja moja watafiti huenda na kukaa kwa siku kadhaa wakiweka mahema na vifaa mbalimbali vya kitafiti. Anasema wamekwishawaambia mara nyingi watu hao kuweka alama ama kujenga mnara utakaokuwa ishara ya kudumu kuonyesha uthamani wa eneo husika, ikizingatiwa kwamba shughuli za utafiti bado zinaendelea.
“Hawa watu bado tunawaona, wanakuja hata kama ni mara moja moja wakiwamo Wazungu. Tunachojiuliza ni je wao hawaoni umuhimu wa kuweka alama pale? Au wanataka kila wanapokuja tuwapeleke kisha waweke mahema yao wafanye kazi zao na kuondoka?” Anahoji mkazi huyo.
Wakati unashangaa kutokuwapo alama ya sehemu hiyo licha ya utafiti mwingi ukiwamo wa kimataifa kufanyika, kando ya mlima ndimo kuna mashimo ambamo wenyeji hudai ndimo ufukuaji wa mabaki ya mjusi ulifanyika.
Mashimo hayo takriban matatu yapo karibu na mlima, lakini pembezoni kuna bwawa la maji ambalo linaelezwa na wenyeji kuwa huwa halikauki hata kipindi cha kiangazi, licha ya mito mingi ya sehemu hiyo kukauka.
“Bwawa hili pia lina heshima yake katika matambiko, licha ya kwamba wazee wetu huwa hawalifikii, lakini maji yake ni masafi na tunayanywa bila shida tunapokuja huku,” anasema Mahmoud Mpili, mkazi wa Mipingo.
Maji nayo ni shida
Licha ya kuwapo kwa bwawa hilo, lakini wakazi wa Tendaguru wanalilia maji wakitaja kilio hicho kuwa cha enzi na enzi, lakini wao wanaona kuwa wanaonewa na mamlaka za Serikali kwa kutopatiwa huduma hiyo kijijini kwao.
Wanasema bwawa hilo la maji liko mbali na makazi yao, na hakuna mwanachi anayeweza kufuata maji umbali wa kilomita 38 kutoka kijijini, hivyo wanachotaka ni kupatiwa huduma hiyo karibu na makazi yao.
Wao wanasema kuwa shida hiyo ya maji haipaswi kuwaandama, ilhali ‘mjusi wao’ anachangia pato Ujerumani kupitia utalii. Mabaki ya dinosaria huyo ambayo yapo katika jumba la makumbusho la Naturkunde jijini Berlin yanatumiwa kuvutia watalii kutoka ndani na nje wanaokwenda kuyaangalia.
Hata hivyo jambo la kushangaza ni namna gani wananchi hao wanajua mjusi huyo anaiingizia fedha nyingi Ujerumani, lakini ukiwauliza majibu yao ni mepesi, lakini yaliyobeba uzito wa aina yake.
“Kaka hatuna maji hapa, tunakunywa maji ya mifereji na vidimbwi ambayo wanyama wa porini wanajisaidia humo, lakini tunajua sana yule mjusi anawatajirisha Wazungu. Tunaingia hata mtandaoni kwa kutumia simu tunaona walivyomrembeshea nyumba yake,” anasema mwenyekiti wa kitongoji wa Nyamapaya kilichopo katika kijiji hicho, Mohamed Mayuni (31).
Mayuni anasema akikutana na kiongozi yeyote wa kitaifa akiwataja Rais John Magufuli; makamu wake, Samia Suluhu Hassan na au Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atawafikishia kilio hicho kwa hisia kali na kwamba, hata machozi yatamtoka.
Anasema akinamama wamekuwa wakipata shida kutafuta maji nyakati za kiangazi, huku wakipoteza muda mwingi kusaka huduma hiyo badala ya kujielekeza katika uzalishaji mali shambani jambo ambalo wameeleza mara nyingi kwa viongozi waliowahi kuwatembelea siku za nyuma.
“Nikikutana na mmoja kati ya hao, nina mambo matatu; kilio cha barabara ya kwenda Tendaguru kutoka hapa (kijijini), zanahati na maji. Kwa kweli hivi ndivyo vilio vikubwa wakati mjusi wetu yupo Ulaya na wanapata pesa nyingi tu. Hivi kweli wanashindwa hata kutupatia mgawo kidogo wa fedha tujengee hivi vitu - barabara, zahanati na kisima cha maji?” Anahoji.
Mawe yaliyowekwa juu ya kilima cha Tendaguru na wananchi. (Picha zote na Kulwa Magwa)
Wasemavyo wadau
Mtendaji mkuu wa shirika lisilokuwa la kiserikali la South Human Empowerment, Rajab Kilindo anasema jamii zinazoishi katika maeneo yenye historia au mambo ya asili hazina budi kutazamwa kwa jicho la kipekee kwa kuwa walinzi na wahifadhi wa maeneo husika.
Anasema malalamiko ya wananchi wa kijiji cha Mnyangala kuhusu miundombinu na hali ya maisha vilipaswa kuwa ni historia, badala yake jamii ingekuwa inazungumzia uboreshaji zaidi wa miundombinu hiyo.
“Nasikia hata zahanati hakuna, maji shida, barabara kwenda eneo alipoishi huyo mjusi haipo. Sasa haya yote ni mambo ambayo Serikali ingekuwa ilishayamaliza miaka mingi na sasa ingekuwa labda tunazungumzia lami kujengwa,” anasema Kilindo.
“Kwa sasa tungekuwa hatuzungumzii zahanati tu, bali kuzungumzia zahanati kuboreshwa na kuwa kituo cha afya, kungekuwa na maji ya uhakika na vijiji jirani vingekuwa vinakitegemea zaidi kijiji hicho,” anasema.
Mtafiti wa mambo ya kale kutoka Zanzibar, Ibrahim Hussein anasema zipo malikale nyingi katika maeneo mbalimbali nchini ambazo Serikali haijaziendeleza ili ziweze kuchangia katika uchumi wa Taifa kupitia utalii.
Anasema, Tendaguru ni eneo mojawapo muhimu ambalo halijaendelezwa muda mrefu na kwamba, kitendo cha kuendelea kulisahau ni kulifanya lisahaulike na hivyo kuwapa fursa Wajerumani kunufaika nalo huko huko kwao.
“Hivi yule mjusi si alitoka Tendaguru? Sasa kama hata Tendaguru huiendelezi, lakini wale (Wajerumani) wanae mjusi waliyemtoa pale na wamem-lable (wamemtambulisha) kuwa walimtoa pale unategemea nini kama huwapi fusa ya kuendelea kupiga fedha?” Anahoji mtafiti huyo.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bakari Meno anasema vilio vilivyopo kijijini hapo ni vingi, lakini wamekosekana wanaoweza kuwasaidia kuvitatua.
“Serikali inayajua sana matatizo yetu yanayoonekana na hata yasiyoonekana na pia wananchi huwa wanasema kila wanapokuja viongozi, lakini ndiyo kama hivi mpaka sasa tunalilia maji, zahanati, barabara na kule (eneo la Tendaguru) pawekwe alama lakini hakuna kilichofanyika mpaka sasa,” anasema.
Diwani wa Mipingo, Said Naomali anasema wananchi wamechoshwa na ahadi za miaka mingi juu ya eneo hilo na wanachotaka ni matokeo ya kile walichoahidiwa.
“Kweli watu wamechoka mno, wana matatizo mengi tofauti na uhalisia wa eneo ambalo Mwenyezi Mungu amewajalaalia kuwa nalo. Hawana maji ya uhakika, matibabu pia bado maana hawajapata wahudumu wa afya na zahanati yao ilibomoka lakini pia hakuna barabara nzuri inayofika huko,” anasema.
Anasema licha ya kwamba yeye kwa kushirikiana na mbunge wa Mchinga wamepigia kelele suala la miundombinu, lakini bado hakuna kilichofanyika.
“Kuna wakati wananchi (Mnyangala) walifyeka vichaka wakitegemea halmashauri nayo ingepanua barabara inayokwenda kwenye eneo la Tendaguru, lakini hakuna kilichofanyika. Ndiyo maana ukizungumza nao ni kama wamekata tamaa,” anasema.
Serikali inasemaje?
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Lindi, Samuel Warioba anasema changamoto zote zilizopo katika kijiji hicho zinafahamika na Serikali itazitekeleza.
Hata hivyo, anawataka wananchi kuzifanyia kazi wenyewe zile ambazo ziko ndani ya uwezo wao na kwamba, wasiisubiri Serikali kwa kila kitu kwa vile inakabiliwa na mambo mengi ya kuyatekeleza.
“Wananchi nao wana jukumu lao, nalo ni kujiletea maendeleo wenyewe. Nazielewa vizuri changamoto hizi na zipo katika mipango yetu ya utekelezaji,” alisema Warioba.
Hata hivyo, Kaimu Katibu tawala wa mkoa, Greyson Mwaigombe anaitaka halmashauri kuzifanyia kazi changamoto hizo akisisitiza kuwa hilo ni jukumu lao na hawawezi kulikwepa.
“Kwa eneo la pale palipogunduliwa mjusi nadhani ni wajibu wetu sote kama mkoa kwa kushirikiana na Serikali kuu na wizara (ya Maliasili na Utalii) kuweka alama ya utambulisho ili kila mtu anayetaka kwenda kupaona aweze kufika na kupajua,” anasema.
Mwaigombe anasema tayari wamepata maelekezo kutoka ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuhakikisha kuwa wanayatambua maeneo yote yenye vivutio vya utalii kwa ajili ya uendelezwaji.
Hata hivyo, katibu tawala huyo anawataka wananchi wa Tendaguru kuendelea kufanya shughuli zao za matambiko katika eneo hilo kwa kuwa ni sehemu ya utamaduni wao wa asili na pia kielelezo muhimu cha kuenzi mila na desturi.
Alichosema waziri wa zamani
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani anasema kwamba, Serikali ya Awamu ya Tano kwa kushirikiana na ile ya Ujerumani wamedhamiria kuhakikisha kwamba eneo hilo linanufaika na umaarufu wake kutokana na mpango wa kujenga makumbusho ndogo.
Makani aliyezungumza na gazeti hili kabla ya kutenguliwa uteuzi wake alisema mpango huo utatekelezwa kwa kuwatumia watalaamu wa mambo ya kale kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam watakaowezeshwa kufanya utafiti na kuyafukua mabaki ya mijusi yanayoaminika kubakia katika eneo hilo.
“Taarifa za kitafiti zinaonyesha kwamba kuna mabaki (ya mijusi) chini ya ardhi katika eneo hilo baada ya wale wawili kuchukuliwa, hivyo tutakapoyafukua na kujenga makumbusho eneo hilo ndipo tutaangalia ujenzi wa miundombinu mingine kama barabara,” anasema.
Hata hivyo, mhifadhi wa malikale wilayani Kilwa, Aisha Omary anasema kuna athari ya kiuhifadhi inayoendelea katika sehemu hiyo kutokana na ucheleweshaji wa kulitambua eneo hilo ambao unakifanya kizazi kilichopo nchini kutolifahamu vyema.
“Kama wanachelewa kupatambua, kupatengeneza na kupahifadhi unategemea mtoto yupi wa sasa anayesoma atapajua, atapaenzi au atajiona fahari kuwa eneo hilo ni la kujivunia kwake?” anahoji Aisha akiufananisha umuhimu wa Tendaguru na eneo la malikale la Oldupai Gorge lililopo mkoani Arusha.
No comments:
Post a Comment