Friday, October 6

Tume ya uchaguzi Kenya yaahirisha vikao vya mashauriano tena

Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya IEBC imeahirisha kikao chake na wawakilishi wa wagombea urais kwenye marudio ya uchaguzi huo utakaofanyika tarehe 26 mwezi ujao.

Kenia Wahlen IEBCWafula Chebukati in Nairobi (Reuters/B. Ratner)
Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya IEBC imeahirisha kikao chake na waakilishi wa waakilishi wa wagombea urais kwenye marudio ya uchaguzi huo utakaofanyika tarehe 26 mwezi ujao. Mkutano huo umeahirishwa baada ya Muungano Mkuu wa upinzani NASA kuibua mswada ambao unajadiliwa bungeni kuhusu marekebisho kwenye sheriza uchaguzi. Mwenyekiti wa Tume hiyo Wafula Chebukati amesema kuwa mkutano huo utaendelea hapo kesho baada ya kufahamu hatma yake bungeni. Hata hivyo matamshi ya vinara wa siasa yanaibua hofu kwa taifa ambalo limegawanyika kwa misingi ya kisiasa. 
Mkutano huo unajiri baada ya kushindwa kufanyika mara tatu wiki kadhaa zilizopita huku zikiwa zimesalia siku 26 kwa uchaguzi mpya wa urais kati ya Uhuru Kenyatta na Raila Odinga. Hata hivyo baada ya mazungumzo kati ya pande zote mbili yaliyofanyika kwa saa mbili hakuna mwafaka ulioafikiwa.
Masuala tata
Mwenyekiti wa Tume huru ya Uchaguzi na mipaka Wafula Chebukati alilazimika kuitisha mapumziko huku pande zote mbili zikielekea kufanya mashauriano zaidi. Chebukati ameelezea umuhimu wa mkutano huo unaolenga kupiga msasa masuala yaliyoibua utata ili kufanyika kwa uchaguzi ambao utakubalika na pande zote.
Wakili wa muungano wa NASA James Orengo (mwisho kushoto) na wawakilishi wengine wakati w amashauriano na IEBC
Wakili wa muungano wa NASA James Orengo (mwisho kushoto) na wawakilishi wengine wakati w amashauriano na IEBC
Chebukati ameongeza kuwa "Hatuwezi kuendelea leo kwa kuwa hakuna aliye na mswada huo, kwa hivyo mkutano huu umeahirishwa hadi kesho saa nne ambapo mswada huo utakuwa sehemu ya mjadala wa kesho.
Upande wa Jubile umewasilisha mswada bungeni ukitaka marekebisho kadhaa kwenye sheria za uchaguzi. Muungano wa NASA umesema kuwa hadi bunge liafikiane kuhusu sheria hizo ndipo utaendelea na mkutano huo. Mkutano wenyewe umefanyika baada ya bunge hapo jana kukataa kushirikishwa kwa shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP.
Msaada wa UNDP katika uchaguzi
Aidha wabunge wa pande mbili za siasa wamekataa Shirika la Umoja wa Mataifa kugharamia ununuzi wa karatasi za Uchaguzi. Hatua hiyo inalemaza mwafaka na kuzidisha vizingiti vinavyostahili kuondolewa kabla ya marudio ya uchaguzi wa urais kuonekana kuwa huru na wa haki. Raphael Tuju ambaye ni katibu katika chama cha Jubilee na aliyekuwa kwenye mkao huo amesema: "Huwa siwachukulii kwa uzito, wameilaumu kampuni ya Safaricom, wameilaumu kampuni ya Morpho, wameilaumu kampuni ya Alghurair, kitu ambacho hawajakilaumu ni ziwa Victoria halina samaki wa kutosha kwa sababu ya propaganda za Jubilee.”
Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa kuna nuru kwenye kiza hasa baada ya mkutano wenyewe. Upande wa NASA unashikilia kuwa kampuni za Al Ghurair na Morpho zisihusishwe tena kwenye uchaguzi mpya huku wakitaka maafisa kadhaa wa Tume ya Uchaguzi kuondolewa afisini.
Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju akiwasili katika ukumbi wa Bomas of Kenya kwa kikao cha mashauriano na IEBC
Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju akiwasili katika ukumbi wa Bomas of Kenya kwa kikao cha mashauriano na IEBC
Bob Mkangi ambaye ni wakili na mchambuzi wa masuala ya siasa amesema pana haja ya suluhu ya kisiasa kutafutwa kwa kuwa tume ya Kusimamia Uchaguzi ina mengi ya kufanya. Mkangi ameendelea kusema "Kwa sababu ni wanasiasa, wanaweza kutafuta njia hata kama ni kufanya marekebisho kwenye katiba ili kama muda utaongezwa ufanyike kwa njia ambazo ama utaratibu wa kisheria.”
Matamshi kinzani ya viongozi
Lakini mbali na mkutano huu, viongozi wa pande za Jubilee na Muungano wa NASA wanahubiri injili tofauti kwenye mihadhara na ile ya mwafaka. Matamshi yao huenda yakawa vizingiti kwa maafikiano ya kuondoa taifa kwenye lindi la kiza. Rais Uhuru Kenyatta anapigia debe chama chake katika kampeni jimbo la Isiolo huku akiwasuta wapinzani wake. Haya ndiyo aliyoyasema rais Kenyatta: "Leo hii nasikia akisema kama safaricom ndio inafanya network hakuna uchaguzi kwani yeye ndiye anapanga uchaguzi, aamue kama yeye ni mgombea ama anataka kuwa mwenyekiti.”
Na sasa kinara wa Muungano wa upinzani amesema kuwa Muungano wao utawataka wafuasi wao kususia baadhi ya bidhaa zinazolishwa na kampuni ambazo zinashirikiana na chama tawala. Hata hivyo hakutaja kampuni zenyewe. Hapo jana Odinga alilaumu kampuni ya simu za mkononi ya Safaricom kwa kushirikiana na tume ya IEBC kuvuruga uchaguzi. Odinga anaongeza kusema: "Hatuendi kwa hiyo uchaguzi kabla hatujafanya marekebisho kwenye hiyo tume. Hadi uwanja uwe sawa, tumesema hadi tungoe visiki, tuzibe mashimo tutoe miiba ili tuonane na Uhuru na Ruto wake."
Huku pande hizo mbili zikishikilia misimamo yao mikali, uchumi unaendelea kudorora kwani wawekezaji wanahofia kuwekeza kwenye taifa ambalo hatma yake haijulikani.

No comments:

Post a Comment