Monday, October 2

Tukemee vikao vya CCM kufanyika ofisi za Serikali


Zipo sababu za msingi za kuandika makala haya. Ni katika malengo yaleyale ya kujenga jamii yenye kufikiri na inayolitizama Taifa letu kwa ajili ya siku zijazo.
Suala la Chama cha Mapinduzi (CCM) kuanzisha utaratibu mpya wa kufanyia vikao vya kikatiba vya chama hicho katika Ikulu ya Tanzania linapaswa kujadiliwa na kukemewa bila woga.
Sina uzoefu sana na siasa za chama kimoja kwa sababu nilikuwa kijana mdogo mno, lakini nafahamu kuwa kulikuwa na utaratibu uliokuwa unazingatiwa chini ya chama kimoja.
Tumeona utawala wa Mwalimu Nyerere ukiondoka madarakani mwaka 1985, akaja Mzee Ali Mwinyi aliyeongoza vipindi vyake viwili na mwanzoni mwa kipindi cha pili mfumo wa vyama vingi ulirudishwa.
Tangu mwaka 1992 isingelitegemewa tena shughuli za chama kinachoongoza dola zifanyikie Ikulu kwa sababu utawala wa chama kimoja ulifika mwishoni, na ndivyo ilivyokuwa.
Alikuja Mkapa na kisha Kikwete, (mbali na vikao vya Kamati Kuu) shughuli nyingine za CCM zimekuwa zikifanyikia Lumumba ambako kuna Ofisi ndogo za chama hicho au kwenye ukumbi wa makao makuu ya CCM Dodoma.
Wakati Rais Kikwete akiwa na kofia ya Mwenyekiti wa CCM ngazi ya Taifa, alijenga majengo mapya ya kisasa ya CCM ambayo baadaye yalifunguliwa rasmi na mrithi wale, Rais Magufuli.
Mwinyi, Mkapa, JK
Wengi wetu tuliipongeza CCM kwa ujenzi ule mkubwa na hatukutaka kuhoji waliwezaje kujenga majengo ya maana namna ile, hatukuhoji kwa sababu tulidhani lile ni jambo jema, ni jambo la maendeleo.
Hatukuhoji kwa sababu tulidhani kuwa vyama vingine walau vitajifunza kutoka kwa CCM juu ya umuhimu wa kuwa na ofisi zake za kudumu sehemu mbalimbali katika nchi yetu.
Wakati wa Mwinyi, Mkapa na wa Kikwete CCM iliendelea kuwa na ofisi zilezile za zamani Lumumba Dar es Salaam na Dodoma. Pamoja na uzamani na ukuu kuu wa ofisi hizo bado walizitumia kufanya vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama na shughuli zingine isipokuwa vikao vya Kamati Kuu ambavyo mara nyingi vilifanyika Ikulu.
Tofauti na marais hao waliopita, uongozi wa sasa wa CCM chini ya Rais John Magufuli mbali na vikao vya Kamati Kuu hivi sasa umeongeza kikao kingine cha Halmashauri Kuu ya Tifa ambacho kinafanyika kwa mara ya pili Ikulu. Mara ya kwanza ilikuwa Desemba mwaka jana.
Hayo yanafanyika wakati ambapo CCM ina ofisi ya kisasa kabisa Dodoma na ina ofisi yake ya Lumumba Dar es Salaam ambayo inakidhi mahitaji ya idadi ya wajumbe ambao bado wanakutanishwa Ikulu.
Ikulu ni ya nani?
Ikulu ni mahali pa Watanzania wote, ni mahali pa vyama vyote na inaendeshwa kwa kodi za wananchi wote bila kujali vyama vyao.
Kitendo cha Rais ambaye ni mwenyekiti wa CCM kuhamishia shughuli za vikao vya chama chake katika Ikulu ya Taifa letu, si kitendo sahihi na kinapaswa kuhojiwa kwa nia njema kabisa.
CCM ni chama cha siasa kama vilivyo vyama vingine na ina haki zilezile chini ya Katiba na sheria za nchi yetu kama vilivyo vyama vingine.
Yapo mambo ya msingi ambayo CCM inapaswa kuvifundisha vyama vingine katika kulinda usawa na utawala bora katika Taifa letu.
Moja ya mambo hayo ni kutochanganya masuala ya chama na masuala ya Serikali. Japokuwa Serikali zinaundwa na vyama lakini kuna mipaka ya wazi kati yake.
Kama Taifa hatuwezi kuendelea namna hii na lazima tuambizane ukweli kwamba shughuli za vikao vya kitaifa vya CCM zinapaswa kufanyikia Lumumba jijini Dar es Salaam au Dodoma na kwamba shughuli za kitaifa na za taasisi ya Rais ndizo zinapaswa kufanyikia katika Ikulu ya Watanzania wote.
Mwangwi wake
Pamoja na kuwa CCM ndiyo chama kinachoongoza nchi, haina maana kwamba ndiyo inaongoza kila kitongoji, kila mtaa, kila kijiji, kila kata, kila manispaa na kila halmashauri.
Tunazo halmashauri nyingi tu zinazoongozwa na vyama vingine vya siasa na katika halmashauri hizo ofisi za mameya au wenyeviti wa halmashauri hazitumiwi kwa vikao vya chama kinachoongoza katika eneo hilo. Huo ni mpaka muhimu sana ambao hatupaswi kuuondoa.
Kitendo cha vikao vya CCM kufanyikia Ikulu wakati huu kinamaanisha kuwa huko chini ofisi za umma zote zigeuzwe kuwa kumbi za vikao vya vyama vinavyoongoza huko.
Yaani kama kijiji fulani kinaongozwa na CUF, basi mwenyekiti wa kijiji hicho kila akiitisha vikao vya kiutendaji vya CUF vifanyikie kwenye ofisi ya kijiji ambayo imejengwa kwa kodi za wananchi na inahudumiwa na wananchi.
Kwamba kama halmashauri fulani inaongozwa na Chadema basi ofisi za mwenyekiti wa halmashauri hiyo zigeuzwe kuwa kumbi za vikao vya kikatiba vya viongozi wa Chadema ngazi ya wilaya.
Kwamba kama CCM ina diwani katika kata fulani basi ofisi ya diwani huyo iliyojengwa na inahudumiwa na wananchi igeuzwe kuwa ukumbi wa vikao vya CCM vya kikatiba katika ngazi ya kata. Orodha inaweza kuwa ndefu na ndefu na ndefu.
Iliyo sawasawa
Rais Magufuli anaweza kuitumia Ikulu kwa vikao vidogo visivyo rasmi vya CCM. Mathalani, anaweza kumuita Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na akampa maelekezo na wakashauriana masuala ya msingi kuhusu chama chao ndani ya Ikulu. Hiyo haina tofauti na Kinana au Phillip Mangula kumtembelea Rais Magufuli Ikulu na kufanya naye mazungumzo.
Rais anaweza kumuita Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole au kiongozi mwingine wa CCM na kumpa maelekezo, hicho si kikao rasmi na hiyo inafanyika dunia nzima.
Ukienda Marekani kwa mfano, kiongozi wa chama cha Republican anaweza kumtembea Rais Donald Trump Ikulu na wakazungumza masuala ya Republican kwa kina. Lakini, kikao cha kikatiba cha chama cha Republican kamwe hakiwezi kufanyikia Ikulu ya Marekani.
Vivyo hivyo kwa ngazi za vijiji, kata, halmashauri n.k. mwenyekiti wa halmashauri au meya wa eneo fulani anaweza kumuita au kutembelewa na kiongozi wa chama chake wa ngazi yoyote na wakafanya mazungumzo katika ofisi ya meya. 

No comments:

Post a Comment