Sunday, October 15

TRA inakusanya mapato kutoka kwa nani?


Wacha niseme ukweli halisi, kama ulivyo. Kwanza aliyeiibua TRA ni Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini. Katika utoaji maoni kwenye mitandao ya kijamii, Zitto aliandika kuwa uchumi wa Taifa unaanguka akielezea namna makusanyo yanayofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalivyoshuka kutoka makadirio ya trilioni 1.4 kwa mwezi kipindi cha mwaka 2016 na kufikia Sh600-700 Bilioni kwa mwezi kwa mwaka huu 2017, jambo lenye maana kuwa tumeshuka kwa zaidi ya asilimia 60. Zitto alitoa taarifa zingine kadhaa za kiutafiti kushajihisha hoja yake.
Kwa miezi kadhaa iliyopita TRA imekuwa haitangazi hadharani makusanyo ya kila mwezi, Utawala wa Rais John Magufuli ulipoanza kazi Novemba 2015, tuliona TRA ikitangaza hadharani mapato ya nchi kila mwezi lakini baadaye zoezi hilo halikuendelea.
Ukiona mamlaka iliyokuwa inatangaza masuala muhimu kwa wananchi kwa kuonyesha mafanikio makubwa, ghafla mamlaka hiyo haiendelei na zoezi hilo, unajua huenda mafanikio yamekwisha na sasa kuna shida. Ni kawaida kwa Serikali za kiafrika kukwepa sana kutangaza shida zake kwa wananchi wake, Serikali hizo ziko tayari kutumia gharama zozote ili kuwafanya wananchi wasijue linaoendelea.
Baada ya taarifa ya Zitto kusambaa na kuandikwa sana, ndipo TRA ikaamua kuvunja ukimya, ikaja na taarifa muhimu kwa wananchi, ikiwajulisha hali halisi ya ukusanyaji wa mapato nchini Tanzania kwa Julai, Agosti na Septemba. TRA ikaeleza kuwa katika kipindi hicho cha robo ya tatu ya mwaka 2017 ilifanikiwa kukusanya mapato makubwa zaidi kuliko yale ya robo ya tatu ya mwaka 2016.
TRA ikasisitiza kuwa katika kipindi hicho imekusanya juma ya Sh3.65 trilioni kwa mchanganuo wa Julai 2017 Sh1.11 trilioni, Agosti Sh1.21 trilioni, Septemba Sh1.33 trilioni na kwamba jumla ya makusanyo hayo ya miezi mitatu ni sawa na ukuaji wa asilimia 1.2 ukilinganisha na makusanyo ya robo ya tatu ya mwaka 2016.
Bila kumung’unya maneno, taarifa ya TRA inazua maswali makubwa na inatia shaka za kutosha. Ifahamike kuwa lengo la TRA kutoa taarifa hiyo ghafla ni kuonesha kuwa nchi haijayumba kimapato, hapa chini nafanya uchambuzi wa kwa nini taarifa ya TRA imeongeza maswali mengi zaidi kuliko yale yaliyokuwapo awali?
Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetoa viashiria vya kuanguka kwa uchumi kwa tafsiri ya wataalamu wa uchumi, kuwa uchumi unaporomoka na kama si kuanguka lakini mbaya zaidi ni kwamba thamani ya shilingi inashuka kwa kasi huku mfumuko wa bei ukikimbilia juu.
Inafahamika kwamba tangu utawala wa awamu ya tano uanze kazi kumekuwa na mabadiliko mengi chanya na hasi ya kiuchumi na kwa vyovyote vile hasi yakionekana kuelemea chanya kwa nguvu mno. Mfumuko wa bei unaokua kwa kasi umeathiri sana bidhaa ambazo zinatumiwa sana na wananchi ikiwamo bidhaa za chakula na mazao muhimu.Kwa hali hii ni wazi kuwa wananchi wanatumia fedha nyingi kununua chakula kuliko kulipa kodi.
Kwa maana nyingine wananchi wanatumia pesa nyingi kutafuta chakula cha kila siku kuliko kuwekeza kwenye biashara ambazo hawana uhakika nazo kutokana na kutotabirika kwa uchumi, kwa hiyo TRA wanapotangaza mapato ya kila mwezi yanaongezeka sijui wanamaanisha kodi au mapato hayo yanakusanywa kutoka kwenye biashara zipi wakati wananchi wengi wanawekeza kwenye mapambano dhidi ya bei za vyakula.
Hali halisi mtaani
Hali halisi ya kiuchumi mtaani ni ngumu. Wananchi wanajua tunaposema hakuna pesa mtaani ina maana hazipo kweli! Ina maana hakuna wepesi wa mzunguko wa pesa kuwezesha raia wajishughulishe na kuendelea na maisha. Ndiyo kusema kuwa kama mama wa kijijini alitumia siku nzima kuuza vitumbua 100 na kupata Sh10,000 leo hii akiweka vitumbua 100 katika eneo lile lile huenda anaishia kuuza vitumbua 50 kwa sababu wanunuzi wa vitumbua wamebadilisha bajeti zao ili kuendana na hali halisi ya uchumi ambao umekuwa mgumu.
Aina hii ya uchumi inawaumiza wananchi wa kawaida, wafanyakazi wa umma na sekta binafsi pamoja na wafanyabiashara na wajasiriamali. Kwa wale wasiofahamu, maisha yanategemeana sana, ili mama mwenye vitumbua auze anahitaji mwalimu (mnunuzi wa vitumbua) awe na pesa za kununua vitumbua, mama mwenye vitumbua anahitaji fundi wa baiskeli aweze kutengeneza baiskeli na kupata pesa ili zingine anunue vitumbua.
Na ili mwalimu apate pesa za kununua vitumbua anahitaji Serikali imlipe vizuri au iifanye pesa ya mshahara anayolipwa iwe na thamani sokoni. Vivyo hivyo fundi wa baiskeli anahitaji wateja wake wawe na uwezo wa kumudu gharama za matengenezo za mara kwa mara, vinginevyo naye hawezi kununua vitumbua.
Leo ukizunguka mtaani ukazungumza na mwalimu, fundi baiskeli na mama muuza vitumbua na wateja wao, wote watakwambia hali ni mbaya sana, wote watakwambia uwezo wao wa kuuza au kununua umeshuka. Na kumbuka hawa ndiyo walipa kodi, wanapokosa pesa za kununua vitumbua hawawezi kuwa na pesa za kulipa kodi. Ndiyo maana taarifa ya TRA kuwa mapato yanakua bila shida inaleta kigugumizi, mashaka na hofu ya wazi.
Kauli ya Rais JPM
Wakati TRA inatangaza kukusanya kodi nyingi zaidi katika robo ya tatu ya 2017 na kwamba makusanyo hayo ni makubwa; Rais Magufuli juzi ametamka wazi kuwa Serikali yake haitaongeza mishahara ya wafanyakazi na kuwa ataendelea kulipa kama walivyolipwa na awamu ya nne.
Tamko la Magufuli linapingana na kauli nzito alizozitoa Septemba 15, 2015 akiwa mgombea urais wa CCM, bila kusahau Mei Mosi 2016 na Mei Mosi 2017 akiwa Rais ambapo alisisitiza kuwa kati ya watu ambao atawatetea na kuhakikisha wanalipwa vizuri ni wafanyakazi.
Lakini ugeukaji huu wa Rais wetu unatofautiana na maelekezo ya Serikali yake mwenyewe, yaliyotolewa bungeni Dodoma mwaka huu, yakisisitiza kuwa Serikali itapandisha mishahara mara tu ikishamaliza kabisa zoezi la kuondoa wafanyakazi hewa (Zoezi ambalo tokea lianze liligeuzwa kuwa chaka la kujifichia la Serikali katika kila kitu).
Unaweza kujiuliza haraka haraka, kama TRA inasema makusanyo yanaongezeka bila shaka, kwa nini Rais anatoa kauli ya kuzuia ongezeko la mishahara ya wafanyakazi ambao wana hali mbaya sana kimapato? Kama Serikali ilitoa ahadi ya kupandisha mishahara ya wafanyakazi mara tatu katika kipindi ambacho TRA ilikuwa inakusanya mapato kidogo, kwa nini Serikali hiyo hiyo inaisaliti ahadi yake ya kuongeza mishahara ya wafanyakazi wakati huu ambapo TRA inajinasibu kukusanya pesa nyingi zaidi?
Mkopo wa Dola Milioni 500
Kama TRA inajinasibu kuwa inaendelea kukusanya pesa nyingi zaidi kipindi hiki, kwa nini ni wakati huu huu ndipo tunashuhudia Serikali ikichukua mkopo wa damu “ghali” wa Dola za Marekani Milioni 500 na ikiahidi kurejesha dola milioni 900 (Riba ya Dola Milioni 400)? Riba hiyo ni karibia sawa na mkopo wenyewe? Kwa nini Tanzania ikakope mikopo ghali na ya kitumwa namna hii katika kipindi ambacho TRA inajinasibu kukusanya matrilioni kila mwezi?
Serikali na TRA watambue kuwa uchumi hauna propaganda. Uchumi wa Zimbabwe na mapato yake vilipokuwa vinaanguka, Serikali ya Rais Robert Mugabe iliwekeza kwenye propaganda, leo uchumi wa Zimbambwe umeanguka kwa asilimia 100. Kuanguka kwa uchumi ni sawa sawa na ujauzito, ujauzito unazidi kuonekana kila uchao na haufichiki muda mrefu.
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kijamii na Kisiasa, Mtafiti, Mwanasheria na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi CUF. Simu; +255787536759/ Barua Pepe; juliusmtatiro@yahoo.com/ Tovuti; juliusmtatiro.com.

No comments:

Post a Comment