Wakati akichora katuni hizo, Tumusiime ambaye amepata kuwa Waziri wa Kilimo wa Uganda, hivi sasa akiwa mmoja wa Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo Afrika Mashariki (EADB), alimtengeneza Bogi Benda kwa uhusika wa ubishi usio na sababu.
Hata mahali ambapo alitakiwa tu kukubali kwa sababu hoja ilikuwa wazi, Bogi Benda alibisha. Mathalan, Bogi Benda aliambiwa na mzungu kuwa alipotembelea Afrika kwa mara ya kwanza alionywa kunywa maji hovyo kwa sababu si salama.
Ni kweli kuwa Afrika ya miaka ya tisini haikuwa na utaratibu wa kuchemsha maji ili kuyatibu yawe salama kwa kunywa. Utamaduni huo haukuwa umesambaa, lakini Bogi Benda kwa vile anaona mzungu anajidai, naye akamjibu: “Hata mimi nilipotembelea Ulaya mara ya kwanza nilionywa kuhusu kuvuta hewa ya Ulaya.”
Alichomaanisha Bogi Benda ni kuwa hewa ya Ulaya ni chafu, kwa hiyo alionywa asiivute. Swali ni angeishi vipi bila kuvuta hewa? Unakuja kubaini kuwa ilikuwa ni ujuaji tu wa Bogi Benda ili aonekane naye amemshinda mzungu na hoja yake kuhusu maji.
Akili ya Bogi Benda alikuwa anaijua mwenyewe. Siku moja yupo baa analalamika anazidiwa na wategemezi wakati kipato chake ni kidogo. Rafiki yake anamkumbusha mbona nyumbani kwake ana mke na mtoto wake mdogo peke yake? Akajibu: “Unaisahau vipi Idara ya Kodi ya Mapato?”
Alichomaanisha Bogi Benda ni sawa na wewe hapo ulalamike kuwa mshahara wako ni mdogo kwa sababu una wategemezi wengi, unaulizwa wategemezi hao akina nani wakati una mke na mtoto peke yake? Unajibu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwamba ni moja ya wategemezi wako.
Bogi Benda Tanzania
Ile sifa ya kutotaka kukubali ukweli hata katika maeneo ambayo hayahitaji ubishi aliyokuwa nayo Bogi Benda, ndiyo ambayo naitumia kama mfano, kulinganisha malumbano ya Serikali ya Tanzania na vyama vya upinzani. Jinsi pande hizo mbili zisivyotaka kuelewana kwenye masuala yaliyo wazi kabisa.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alipigwa risasi Septemba 7, mwaka huu akiwa kwenye gari lililoegeshwa nje ya makazi yake, muda mfupi baada ya kutoka kuhudhuria kikao cha asubuhi bungeni mjini Dodoma.
Suala ni Lissu kupata matibabu bora na kupona. Hilo linafahamika kwa kila mtu, kwa hiyo haitakiwi kuwepo kususiana, kukomoana, kutengana wala kupeana masharti. Muhimu kwa kila mtu ni kwamba Lissu apone.
Malumbano yanayoendelea wakati huu ambao Lissu yuko kitandani, yanadhihirisha kuwa Serikali na wapinzani, wanapenda kutofautiana hata mahali ambapo inaonekana wazi kuwa tofauti hazipaswi kuwepo kama ile tabia ya Bogi Benda.
Mtu ameshambuliwa kwa risasi na inaelezwa ameumizwa kwa kiwango kikubwa, sasa inashindikana nini wakati huu kujenga mshikamano wa pamoja, kufanya mashauriano ya namna bora ya kumpa huduma za kiwango cha juu ili apone kabisa?
Picha ambayo wahusika wanaitengeneza ni kama Chadema inamshikilia Lissu kuwa ni mgonjwa wao, halafu Serikali wanamuona Lissu kuwa mgonjwa wa jirani, kwa hiyo kumhudumia hakuna ulazima.
Hoja ya Serikali inakuwa: ‘Ninyi si mlikataa kufuata utaratibu tuliouweka?’ Kwamba kosa la Chadema ni kumuondoa Lissu kwenye mnyororo wa Hospitali ya Taifa, Muhimbili ambao ndiyo rasmi wenye kutambuliwa na Serikali, vilevile Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF).
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, siku Lissu alipopigwa risasi, wakati Lissu alipokuwa akitibiwa mjini Dodoma kabla ya kupelekwa Nairobi, walifanya kikao kujadili matibabu ya kiongozi huyo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba. Katika kikao hicho uamuzi wa Serikali ulikuwa kwamba haiwezi kuhusika na matibabu ya Lissu kwa sababu yametoka nje ya mnyororo wa Muhimbili.
Maelezo hapo ni kuwa Lissu alitakiwa kuhamishwa kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kupelekwa Muhimbili ambako kama kungekuwa na ulazima wa kupelekwa nje, rufaa ingetolewa na Muhimbili kisha moja kwa moja angepelekwa India katika Hospitali ya Apollo.
Maswali kila upande
Chadema walipoambiwa kuwa Serikali haiwezi kumhudumia Lissu nje ya mfumo wa Muhimbili walikubali. Wakaamua kumsafirisha kwenda Nairobi kwa gharama zao. Wakachukua uamuzi wa kuchangishana gharama za matibabu.
Sasa manung’uniko ya nini ikiwa walichagua kufuata njia ambayo wao waliamini ni bora zaidi lakini haina baraka za Serikali? Tangu Lissu anaondolewa Dodoma kwenda Nairobi, Chadema walifahamu fika kwamba Serikali haitahusika na matibabu ya Lissu, kwa nini isijikite kumhudumia mgonjwa na kuachana na malumbano na Serikali?
Septemba 8, Spika Ndugai alisema bungeni kuwa familia ya Lissu iliuchagua kuwa matibabu ya mbunge huyo yapo nje ya mfumo wa Serikali na NHIF. Alichokieleza ndicho ambacho kilirejewa na Mbowe. Tafsiri ni moja ingawa uwasilishaji ni tofauti.
Wakati Spika Ndugai akisema hivyo, Bunge analoliongoza pamoja na Serikali, wanatambua umaalumu wa matibabu ya Lissu kwa namna yalivyo. Chadema na familia ya Lissu walikuwa na hofu kuhusu usalama wa mbunge huyo, endapo angeendelea kutibiwa nchini.
Ukitazama pia mazingira ya shambulio, unaona dhahiri kuwa ilikuwa lazima kwa mtu yeyote anayempenda Lissu kutilia shaka usalama wake, siyo tu akiwa anatibiwa nchini, bali popote pale duniani.
Waliomshambulia Lissu bila shaka walitaka roho yake. Na kwa vile wameishia kumjeruhi, ni wazi kazi waliyoikusudia hawajayakamilisha. Kwa maana hiyo, popote pale duniani, wakiweza kumfikia basi maisha ya Lissu yatakuwa hatarini. Hivyo, ulinzi si chaguo bali lazima.
Bunge na Serikali walitakiwa kufahamu hofu ya Chadema na familia ya Lissu, ukizingatia kwamba haukuwa umepita muda mrefu tangu mbunge huyo aviambie vyombo vya habari kuwa anafuatiliwa na watu ambao alidai ama ni polisi au maofisa Usalama wa Taifa.
Ni kwa jicho hilo, Serikali ilitakiwa kufahamu kuwa Chadema na familia ya Lissu hawana imani na ulinzi wa Serikali. Hata hoja yao ya kumpeleka Lissu Nairobi si kwa sababu za ubora wa matibabu, bali usalama. Hivyo, Serikali ilitakiwa kutumia busara ili Lissu atibiwe katika mazingira yenye radhi ya familia na chama chake.
Baada ya Lissu kusafirishwa kwenda Nairobi, hazikuonekana jitihada zozote za Serikali kujishirikisha kwa namna yoyote kumtibu Lissu. Ni kama walisema ‘mmeamua kumpeleka huko mgonjwa wenu, basi mtamtibu wenyewe. Sisi hatuhusiki’.
Kwa vile uamuzi ulikuwa ni huo, kwamba Serikali haitahusika kwa sababu Chadema na familia ya Lissu walichagua mfumo nje ya Muhimbili, je, hata viongozi binafsi wa Serikali kujitoa na kujishirikisha ilishindikana nini?
Tunaweza kubaki hapo kuwa Serikali ilishatangaza kutohusika na matibabu, sasa kauli mpya za Waziri Ummy kuwa familia ya Lissu iandike barua ni ya nini? Kipi ambacho Serikali haikitambui kuhusu matatizo ya Lissu mpaka iandikiwe barua?
Serikali imeshajieleza na imesikika, sasa maneno mengine ya nini? Kama imeona upo mwanya wa kumhudumia Lissu katika hospitali yoyote hata zilizo nje ya mfumo wa Muhimbili, kwa nini isikae chini na familia yake pamoja na Chadema ili kujadili na kuangalia namna bora ya kushirikiana?
Kurushiana maneno, mara Chadema wanasema hawawezi kuiandikia barua Serikali, familia ya Lissu nayo inasema Lissu kakataa barua isiandikwe, huku Serikali ikisisitiza inahitaji barua, ni kuzalisha malumbano ambayo hayatakiwi.
Kipaumbele ni kumhudumia Lissu tu.
No comments:
Post a Comment