Mlowola ametoa tahadhari hiyo kwa Nassari leo Jumanne, Oktoba 17, 2017 alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amesema endapo Nassari ataendelea kuingiza siasa kwenye suala hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mlowola amesema kitendo cha mwanasiasa huyo kuweka hadharani taarifa za uchunguzi ni kinyume cha sheria kwa kuwa kazi hiyo inatakiwa kufanyika kwa siri na Mahakama ndiyo yenye jukumu la kuchukua hatua.
Amesema Takukuru ina wajibu wa kumlinda mtoa taarifa lakini jukumu hilo linakuwa tofauti kwa Nassari ambaye ameamua kujitokeza hadharani.
"Alicholeta Nassari kwetu ni taarifa si ushahidi. Ameleta tumezipokea na tunazifanyia kazi, inashangaza anapozungumza na vyombo vya habari na kutuelekeza namna ya kufanya kazi," amesema.
Mlowola amesema, "Tulishampa angalizo kuwa mambo tunayoongea ni siri lakini mwenzetu inaonekana anafanya siasa kama anavyosema mwenyewe kuwa ataendelea kuleta ushahidi kama series ya Isidingo."
Mkurugenzi mkuu huyo amemtaka Nassari kuacha kukiingiza chombo hicho kwenye siasa ili kifanye kazi kwa uhuru kama sheria inavyoelekeza.
"Nitoe rai kwa Nassari na wengine wote, ukishaleta taarifa kwenye chombo husika kama hiki kiache kifanye kazi. Hakuna sababu ya kukishinikiza au kukiingiza kwenye malumbano ya kisiasa. Ukweli wa mambo utajulikana mahakamani," amesema.
No comments:
Post a Comment