Juzi, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema Serikali ina mpango wa kununua vichwa 13 vya treni vilivyoko bandarini ikiwa vitathibitika kuwa vina ubora unaostahili.
Alisema hayo ikiwa ni miezi kadhaa tangu Rais John Magufuli aseme kuwa amepata habari ya kuwapo kwa vichwa vya treni vilivyowasili Bandari ya Dar es Salaam bila ya mwenyewe kujulikana.
Lakini Mamlaka ya Bandari ilisema siku hiyo kuwa vichwa hivyo vina nembo ya Shirika la Reli (TRL) na kwamba vilinunuliwa na shirika hilo la umma, lakini kukatokea mzozo katika mchakato wa ununuzi.
Machi 23, TRL ilitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuwa imepokea vichwa viwili kati ya 13 ilivyonunua kwa Sh70.9 bilioni kutoka kampuni ya EMD ya Marekani ambayo ilikasimu DCD ya Afrika Kusini.
Habari hizo mbili za kuwasili kwa vichwa vya treni ambavyo mmiliki wake hajulikani na TRL kununua vichwa 13 zimekuwa zikihusishwa kwamba injini hizo zilizopo bandarini ambazo Rais anasema mmiliki wake hajulikani ndizo ambazo ziliagizwa na TRL.
Kwa hiyo, kauli ya Profesa Mbarawa imechanganya watu kwamba Serikali itanunuaje vichwa vya treni kwa mtu aliyeagiza vichwa kwa kificho hadi vikafika bandarini? Pia, kwa nini Serikali inasita kumtaja mtu ambaye aliagiza vichwa hivyo kama inaweza kufanya naye mazungumzo?
Swali jingine ni kwamba inawezekanaje mtu binafsi au kampuni binafsi kuagiza injini za treni katika nchi hii ambayo usafiri wa aina hiyo bado unaendeshwa na Serikali, yaani haujabinafsishwa? Hadi sasa ni mashirika mawili tu yanayoendesha huduma hiyo yaani TRL na Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara), ambayo pia yanatumia mifumo tofauti ya reli.
Taarifa kwamba injini hizo zina nembo ya TRL inazidi kuchanganya watu wanaofuatilia habari hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa shirika hilo linaendeshwa kwa kodi za wananchi na hivyo ni lazima ununuzi wa mali zake ufanyike kwa njia ambayo haitakuwa na usiri wowote kuepuka ufisadi.
Kwa maana hiyo, taarifa kuhusu vichwa hivyo vya treni zinachanganya kutokana na ukweli kwamba mkuu wa nchi anasema aliyeviagiza hajulikani na waziri anasema watafanya naye mazungumzo.
Ni muhimu kwa wahusika kuzingatia kuwa mali wanazozungumzia zinatakiwa kununuliwa kwa kodi wanazokatwa wananchi na hivyo wanastahili kupewa taarifa ambazo zinaeleweka na zitakazowapa picha kuwa jasho lao linatumiwa vizuri na si kwamba linaliwa na wajanja wachache ambao hawawezi kutajwa hadharani. Vita dhidi ya ubadhirifu, ufisadi, rushwa na mambo mengine haiwezi kufanikiwa iwapo Serikali itakuwa inatoa taarifa zisizokamilika kwa baadhi ya mambo na zilizokamilika kwa mambo mengine.
Suala la usafiri wa treni ni nyeti na muhimu sana kwa kuwa ni usafiri unaotegemewa na wengi ikizingatiwa kwamba ni nafuu na hivyo kupunguza gharama za maisha, hasa inapofikia suala la usafirishaji mizigo.
Wito wetu ni kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuchukulia kwa uzito taarifa za injini hizo za treni, kufanya uchunguzi wa kutosha na kutoa taarifa yenye majibu ya maswali yote ambayo yaliibuka baada ya Rais kueleza kuwa mmiliki hajulikani.
Bila ya kuweka wazi mchakato mzima wa ununuzi wa injini hizo na jinsi suala hilo lilivyomalizwa, maswali yaliyoibuka yatawafanya watu waamini kuwa vita dhidi ya rushwa na ufisadi ni dhidi ya watu fulani tu na sio wote.
Tuongeze imani kwa wananchi katika vita hii kwa kuwa wawazi zaidi na kutoa taarifa zinazokidhi kiu na si zinazoacha maswali.
No comments:
Post a Comment