Thursday, October 5

Serikali yataka mfumo kuwatambua walioghushi vyeti

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki 
Dar es Salaam. Serikali imeitaka Bodi ya Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kutayarisha mfumo utakaokuwa na majina ya watumishi wa umma walioghushi vyeti ili iwe rahisi kuwatambua.
Agizo hilo linatokana na kuendelea kuwepo watu wanaojitokeza kwenye usaili wa ajira za umma walioghushi vyeti.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki amesema hayo leo Alhamisi wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo.
Amesema kutokana na umuhimu wa utumishi wa umma, wanaoghushi vyeti wanastahili kutambuliwa popote waendapo.
Kairuki amesema ajira katika utumishi wa umma ni suala nyeti na la msingi, hivyo ni muhimu bodi ikasimamia vizuri na kuhakikisha hakuna anayepenya kwa udanganyifu.
“Tengenezeni mfumo wa data, ukiwa na majina ya wote wanaoghushi na walioghushi vyeti, muyaanike na wachukuliwe hatua zikiwemo za kisheria, wasiachwe,” amesema Kairuki.
Amesema bodi ikifanya kazi ya usimamizi vizuri Taifa litapata nguvu kazi yenye sifa stahiki.
Waziri ameitaka bodi kufuatilia mchakato wa utoaji ajira katika kada zinazoajiri zenyewe, zikiwemo halmashauri za miji, majiji na wilaya.
Amesema licha ya kuwa na ruhusa ya kuajiri, bado bodi ina jukumu la kufuatilia kuhakikisha hakuna anayepita kiujanja ujanja.
Kairuki ameagiza bodi kutumia mfumo wa Tehama kuwafikia wadau ambao ni waomba ajira popote walipo ili kuwapunguzia gharama za nauli ya kufika makao makuu kwa ajili ya usaili.
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira kwa Utumishi wa Umma, Xavier Daudi amesema baada ya ajira kufunguliwa kwa mwaka wa fedha 2017/18 walipokea vibali vya ajira 292 vyenye idadi ya nafasi 2,611.
Amesema hadi Septemba idadi ya waombaji 185 walishapangiwa vituo vya kazi.
“Wiki ijayo tunatarajia kuwapangia vituo vya kazi zaidi ya wasailiwa 400 na kuna vibali vingi ambavyo vipo katika hatua mbalimbali,” amesema.
Daudi amesema bado kuna watu wanaendelea kutumia vyeti feki kuomba ajira na kufika navyo kwenye usaili.
“Licha ya kelele, kuchukuliwa hatua na baadhi ya watu kufukuzwa kazi, bado kuna watu wanakuja kwenye usaili na vyeti vya kughushi, huwa tunavishikilia vyeti vyao na kuvirudisha kwenye vyuo husika,” amesema.
Daudi amesema katika mawasiliano hakuna chuo kilichovitambua vyeti hivyo.
Bodi hiyo ya watu sita inaongozwa na mwenyekiti, Rose Lugembe. Wajumbe ni John Joel, Mbarak Abdulwakil, Aloyce Msigwa, Fanuel Mbonde na Tamika Mwakahesya.

No comments:

Post a Comment