Serikali ya Rwanda imesisitiza uamuzi wake wa kumrudisha nyumbani balozi wake aliyoko nchini Ufaransa, Jack Kabare ikionyesha kukerwa kwake na shutuma zinazoendelea kutolewa na Ufaransa.
Rwanda imesema imechukua hatua hiyo kujibu kile ilichokiita dharau na shutuma za mara kwa mara zinazofanywa na Ufaransa dhidi ya Rwanda.
Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA anaripoti kuwa hii ni hatua mpya kabisa inayo onyesha mustakabali usiofahamika mwisho wake kati ya Ufaransa na Rwanda.
Mapema wiki iliyopita Rwanda ilimrudisha balozi wake kutoka Paris lakini taarifa za serikali wakati huo hazikuzungumzia kiundani zaidi suala hilo.
Hatua hii imekuja baada ya majaji wa Ufaransa kutangaza kuanza upya upelelezi kuhusu aliyeitungua ndege ya Rais wa zamani wa Rwanda Juvenali Habyarimana mwaka 1994, jambo ambalo limekuwa ni mzizi ya sintofahamu unaoendelea kwa zaidi ya miongo miwili sasa baina ya mataifa haya mawili.
Katika hatua isiyotegemewa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Rwanda akiwa pia msemaji wa serikali Louise Mushikiwabo amesema:
"Tumefanya hivi kutokana na mwenendo usiyoridhisha wa serikali ya Ufaransa ambayo imejaa dharau, sisi kama Rwanda tunachokiomba ni haki ya kisheria, sisi kama taifa tunaamini kuwa vita hivi Ufaransa haiwezi kuvishinda hata kidogo, ndiyo unaweza kujitahidi kuficha uovu wako lakini huwezi kuficha kila aina ya uovu ulioutenda, tunafahamu uovu nchi hiyo ya ulaya ilioutenda hapa, na kwa hali hiyo tunasema Ufaransa haiwezi kushinda vita hivi ambavyo vimejaa hila za kila mara na ndiyo maana tumemuita nyumbani balozi wetu Jacques Kabale."
Rwanda imechukua hatua hii baada ya majaji wa Ufaransa kumuita waziri wa ulinzi wa Rwanda Gen James Kabarebe kwenda kutoa maelezo nchini humo kuhusu kuangushwa kwa ndege hiyo ya Rais wa zamani wa Rwanda kitu ambacho serikali imekutupilia mbali.
Katika hatua nyingine Rais Paul Kagame bila kuuma maneno amesema ripoti na madai ya mataifa ya ng’ambo kuhusu Rwanda ni kujitoa kimasomaso kwa sababu mataifa hayo yamekuwa na mkono kwenye mauaji ya Rwanda.
Kagame amesema: "Na ulimwengu huo wanakotoka hao, ndiyo ulimwengu huo huo uliokaa kando wakati ule watu walipokuwa wakiuawa hapa,hao hao walioamua kuondoa vikosi vyao vya jeshi zaidi ya elfu sita waliokuwa hapa,na kuondoka huku watu wakiteketea,kisha unaniambia unayajali maisha ya watu haoa?unanifundisha demokrasia?uhuru wa kusema na ujinga mwingine? Ndiyo waliondoka vikosi vyao na mimi nilikuwa hapa nikipigana!!"
No comments:
Post a Comment