Sunday, October 15

Ripoti yaibua mapya kuhusu gesi Mtwara


Ripoti ya Mtandao wa mashirika yasio ya kiserikali mkoani Mtwara (Mrengo), imedai kuwa wakazi wa Lindi na Mtwara walipotoshwa namna wanavyoweza kufaidika na uchumi wa gesi asilia inayovunwa katika maeneo yao.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Januari hadi Juni 2017, viongozi wa umma wanatajwa kuhusika katika upotoshaji huo hasa kwenye utekelezaji wa mradi shirikishi jamii wa kudhibiti athari za uendelezaji wa sekta ya mafuta na gesi asilia kwa binadamu, mazingira na hali ya hewa nchini.
“Kupitia mradi huu tumebaini kuwa wananchi walipotoshwa dhidi ya uchumi wa gesi asilia, wakajazwa matumaini makubwa ya kuwa matajiri ndani ya muda mfupi kuliko uhalisia, hali hiyo ilichagia vurugu za kupinga mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Madimba hadi Dar es Salaam mwaka 2013,” inaeleza ripoti hiyo.
Mratibu wa mradi huo, Mustafa Kwiyunga alisema Taifa halikujiandaa dhidi uchumi za gesi.
“Kwa kweli ilikuwa ni sekta ngeni kwa kila mmoja, wakati jamii inahitaji kuelimishwa, waelimishaji nao hawakuwa na taarifa sahihi hivyo wakalazimika kutoa taarifa walizonazo bila ya kujali usahihi wake,” alisema kwiyunga.
“Mradi huu umejikita zaidi katika kuwashirikisha wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kujua athari za kibinadamu, mazingira na namna ambavyo jamii inaweza kufaidika moja kwa moja na uchumi wa gesi, tunatoa elimu kwa njia ya vyombo vya habari, mikutano, semina na warsha kwa makundi mbalimbali ya jamii.”
Taarifa hii inatolewa ikiwa ni miaka minne sasa tangu kutokea kwa vurugu za kupinga mradi wa ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Madimba hadi jijini Dar es Salaam kwa madai kuwa mradi huo ungeweza kuondoa matarajio yao ya kuondokana na umaskini kupitia sekta ya gesi asilia.
Vurugu hizo zilisababisha vifo, ulemavu wa kudumu kwa baadhi ya watu na uharibifu wa mali.
Wakazi wa mikoa hiyo walisema elimu waliyopata kupitia mradi huo, imewapa mwanga wa kujua namna wanavyoweza kufaidika na gesi na kuondokana na dhana potofu waliojengewa hapo awali.
“Tulijazwa matumaini makubwa kwamba uchumi wa gesi utamaliza matatizo yetu yote, ila kwa sasa tunaelewa kuwa ili tufaidike ni lazima tujishughulishe na kazi zingine ambazo soko la gesi zitatengeneza uhitaji, kama kazi za kilimo na ususi au sanaa,” alisema mkazi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Ismail Amir.
“Tuliambiwa Mtwara itakuwa kama Dubai, tukaaminishwa kila mmoja atakuwa tajiri, lakini hizo fikra hazipo tena, hakuna mtu atakwenda barabarani kuandamana au kufanya vurugu akidai kufaidika na gesi asilia.
“Hii elimu ingetolewa mapema kabla ya utekelezaji wa mradi sidhani kama tungepitia kwenye historia ile ya vurugu, viongozi wajifunze kutokana na hili, ni muhimu kutoa elimu sahihi kwa jamii kabla ya utekelezaji wa mradi katika eneo husika,” alisema.

No comments:

Post a Comment