Uchunguzi umebaini kuwa gharama za usafiri wa bodaboda na bajaji ni chini kwa asilimia 50 ukilinganisha na teksi, hali ambayo imewafanya madereva teksi kulalamikia ugumu wa biashara.
Mathalani, gharama ya teksi kutoka eneo la KNCU hadi Hospitali ya Rufaa ya KCMC ni Sh5,000 lakini bajaji zimekuwa zikitoza Sh3,000 kwa safari hiyo huku bodaboda zikitoza Sh2,000.
Dereva teksi, Seif Nguzo alisema ujio wa bajaji na bodaboda umeathiri biashara huku akitolea mfano siku ya jana kuwa kuanzia saa moja asubuhi hadi saa sita mchana alikuwa hajapata abiria.
“Tangu asubuhi hadi sasa hivi sijapata abiria hata mmoja. Angalia magari hapa yanavyopigwa jua hakuna biashara. Wenzetu wanatoza nauli rahisi kwa sababu baadhi yao hawalipi kodi.
“Sisi tunalipa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kodi ya Sh150,000 kwa mwaka na Manispaa (Halmashauri) tunawalipa Sh15,000 hebu waulize hao wa bajaji na bodaboda wanalipa nini?,”alihoji Nguzo.
Alidai kuwa tofauti yao na bajaji na bodaboda ni kwamba wao lazima waegeshe magari katika vituo vilivyoidhinishwa lakini bajaji na bodaboda zinachukua abiria kila mahali.
Dereva teksi mwingine anayeegesha gari lake katika kituo kilichopo Barabara ya Stesheni, Kelvine Mfinanga alisema hali ya biashara ni mbaya.
“Bodaboda na bajaji zimevuruga sana biashara ya teksi, yaani tumebakiwa na wale wateja ambao siyo wapenzi wa kutumia pikipiki,” alisema.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki na Waendesha Bodaboda na Bajaji Kilimanjaro (CWBK), Bahati Nyakiraria aliwataka madereva teksi kuwa wabunifu badala ya kulalamika.
“Huu usafiri umekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi na sasa hivi tuko katika soko huria maana yake tuko kwenye ushindani. Wakitaka na wao watoze bei sawa na sisi,” alisema Nyakiraria.
Kuhusu suala la kodi, Nyakiraria alisema wamiliki wa bajaji wanalipa Sh 150,000 kwa mwaka.
Mmoja wa wateja wa bodaboda, Scholastica Shao alisema anapendelea usafiri huo kwa vile unafika mahali unapokwenda haraka zaidi na gharama ni rahisi kulinganisha na teksi.
No comments:
Post a Comment