Saturday, October 21

Radi, moto na maji vyaua watu sita


Watu sita wamefariki dunia katika matukio tofauti likiwamo la mtoto Charles Samson (14), mkazi wa Kijiji cha Iseni wilayani Sengerema kupigwa radi.
Tukio hilo la mtoto Samson kupigwa na radi lilitokea juzi saa tano asubuhi wakati akiwa na wenzake 12 walipokuwa wakijisomea kujiandaa na masomo ya kidato cha kwanza mwakani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema mtoto Claud Mussa alijeruhiwa katika tukio hilo huku wenzao wakitoka salama licha ya kupata mshtuko wa kawaida.
Katika tukio lingine lililotokea wilayani Kwimba, moto ambao chanzo chake hakijajulikana uliteketeza nyumba ya Kaleb Swema iliyoko Mtaa wa Ngumo na kusababisha vifo vya watu wawili na kumjeruhi mmoja.
Waliofariki dunia ni Jackline Machumu (38) na mwanaye Juliana David (4), huku mwingine aliyejulikana kwa jina moja la Jesca akijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Wakati huohuo, mtu mmoja ambaye jina lake halijajulikana amefariki dunia na wengine watatu kunusurika baada ya mtumbwi waliokuwa wakitumia kuvua samaki ndani ya Ziwa Victoria kupinduka kutokana na kupigwa na upepo mkali.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake juzi kuwa tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Nyamagaro.
Huko Igunga mkoani Tabora, wanafunzi wawili wa Shule ya Awali ya Ncheli wamefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye kisima cha maji walipokuwa wakirejea nyumbani kutoka shule.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa alisema kuwa tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Ncheli saa tano asubuhi ya Oktoba 17 na kuwataja marehemu kuwa ni Mwashi Yohana (6) na Wande Shija (6).
“Mwenzao, Kwimba Sanongo (6), waliyekuwa wameongozana alipoona wenzake wamezama kisimani alikimbia kurejea shuleni kutoa taarifa kwa walimu ambao hata hivyo walipofika na kuwaopoa walikuta tayari wamefariki dunia,” alisema Kamanda Mutafungwa.

No comments:

Post a Comment