Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Francis Mwanaisi alisema mwaka jana wanawake 63,123 walipimwa saratani ya matiti na kati yao, 422, sawa na asilimia 0.7, walikutwa na ugonjwa huo.
“Kati ya Januari hadi Septemba, mwaka huu wanawake 48,610 wamepimwa na 47 kati yao, sawa na asilimia 0.7 wamegundulika kuwa na ugonjwa huo,” alisema Dk Mwanaisi.
Alifafanua kuwa uelewa mdogo wa jamii kuhusu upimaji wa afya umebainika kuwa miongoni mwa sababu za ugonjwa huo na kuwataka wananchi kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara ili kupata tiba mapema.
Hivi sasa, wanaogundulika kuwa na ugonjwa huo hupewa rufaa kwenda kutibiwa katika hospitali za rufaa za Bugando jijini Mwanza, Muhimbili na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, zote za jijini Dar es salaam.
“Kwa wale wagonjwa ambao hawajaathirika na ugonjwa sana, hospitali yetu inao uwezo wa kuwafanyia upasuaji na tayari tumefanikiwa kuwafanyia upasuaji wanawake wanne kati ya Januari hadi Septemba mwaka huu,” alisema Dk Mwanaisi.
Mkazi wa Manispaa ya Musoma, Felix Kalisa aliiomba Serikali kuboresha huduma na tiba ya saratani katika ngazi ya wilaya na mikoa ili kutoa fursa kwa wananchi wengi kufikiwa badala ya huduma hiyo kutolewa ngazi ya hospitali za rufaa.
No comments:
Post a Comment