Saturday, October 21

PUMA, TIPER ZATAKIWA KUWASILISHA TAARIFA ZA UTEKELEZAJI KILA BAADA YA MIEZI MITATU


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (mbele kushoto) pamoja na Watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Puma Energy wakiendelea na ziara katika sehemu ya kampuni hiyo Kurasini, jijini Dar es Salaam tarehe 19 Oktoba, 2017. 

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameziagiza kampuni za Puma Energy na Tiper Tanzania kuwa kuanzia mwisho wa mwezi huu ziwasilishe mara moja taarifa ya shughuli zake za kila baada ya miezi mitatu Serikalini, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya kampuni hizo.

Pamoja na hayo Waziri Kalemani amesema kuanzia sasa ni marufuku mafuta kupotea kwenye vituo vya kupokelea mafuta na kubainisha kuwa anatarajia kuchukua hatua kwa kushirikiana Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ili kudhibiti tatizo hilo.

Dkt. Kalemani aliyasema hayo Dar es Salaam tarehe 19 Oktoba, 2017 alipofanya ziara katika kampuni hizo na kutembelea Bohari za kuhifadhia mafuta, pamoja na kufanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha kupokelea mafuta ya dizeli kilichopo Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Alisema Serikali kama mbia mwenye asilimia 50 kwenye hisa za kampuni hizo inatakiwa kushiriki ipasavyo ikiwa ni pamoja na kupata taarifa za kila baada ya miezi mitatu kuhusu utendaji, faida, hasara pamoja na changamoto zinazokabili kampuni

“Nataka mtambue kuwa ninyi kama kampuni ni sehemu ya serikali na kuanzia sasa jicho la serikali litakuwa linawaangazia kila mnachokifanya, huu sio wakati wa kufanya kazi kwa mazoea,” alisema Dkt. Kalemani.

Akiwa katika kampuni ya Puma Energy yenye vituo 49 nchi nzima, Dk. Kalemani aliagiza kampuni hiyo kupanua shughuli zake kwa kufungua vituo zaidi kwenye mikoa kwa kuwa hadi sasa mikoa sita nchini bado haijafikiwa na vituo vya Puma Energy.

Aidha aliitaka kampuni hiyo yenye matanki manne ya kuhifadhia mafuta huku moja likiwa ni bovu kuhakikisha matengenezo yanafanyika mara moja ndani ya wiki moja ili kuhakikisha kuwa mafuta ya kutosha yanapatikana. Akiwa katika kampuni ya Tiper, Dkt. Kalemani aliagiza kampuni hiyo kuanza kuwasilisha taarifa ya utendaji kazi wake kuanzia mwisho mwa mwezi huu pamoja na taarifa ya matumizi ya shilingi bilioni nane ambazo zilitolewa na serikali kwa ajili ya ukarabati wa tanki moja la kampuni hiyo lililokuwa limeharibika.

Aidha, aliitaka kampuni hiyo kuyafufufua matanki manne ya kuhifadhia mafuta ambayo hayafanyi kazi kwa sasa ndani ya kipindi cha miezi minne kuanzia sasa ili kuongeza kiwango cha kuhifadhi mafuta.

Katika hatua nyingine Dkt. Kalemani alifanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha kupima mafuta aina ya dizeli kutoka kwenye meli kilichopo chini ya Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA) kilichopo Kigamboni na kukagua mashine mbili za flow meters zilizofungwa kituoni hapo. Waziri Kalemani aliagiza ukarabati wa mashine hizo kufanyika kwa haraka ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha hakuna upotevu wa mafuta kabisa.
Meneja Bohari kutoka Kampuni ya Puma Energy, Auni Yateri (kulia) akielezea shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo kwa Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani(katikati).
Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani (kulia) akizungumza na vyombo vya habari katika Kituo cha Puma Energy, Kurasini jijini Dar es Salaam mara baada ya kutembelea kituo hicho.
Sehemu ya Kituo cha Puma Energy, Kurasini jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani (kulia) akitoa maelekezo katika kituo cha kupima mafuta aina ya dizeli kutoka kwenye meli kilichopo chini ya Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA) kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment