Friday, October 13

Polisi yatangaza kuviwajibisha vikundi vya Whats App Tanzania

Viongozi wa makundi ya What's App nchini Tanzania wanatakiwa kutoa taarifa pindi uhalifu unapofanyika kwenye makundi yao.
Kufanya hivyo kutawasaidia polisi kuchukua hatua dhidi ya mhusika aliyefanya uhalifu huo ili kukabiliana na ongezeko la vitendo vya uhalifu mtandaoni.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa na naibu mkuu wa kitengo cha Makosa ya Mtandano, Joshua Mwangasa wakati wa semina iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano(TCRA) na kuwakutanisha viongozi wa dini wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa za jeshi la polisi makosa ya kimtandao yameendelea kuongezeka kwa kasi kubwa huku makundi ya What's App yakionekana kuwa kichocheo kikubwa.

Viongozi wa makundi hayo wametakiwa kutowavumilia wahalifu hao na mara moja wametakiwa watoe taarifa polisi.

"Usikubali umeanzisha kundi kwa nia nyingine halafu mtu au watu wanaweka mambo yasiyofaa, toa taarifa hatua zichukuliwe kinyume na hapo hata wewe utahusika," Amesema Mwangasa.

Uchunguzi wa polisi unaonyesha kuwa kwa kiasi kikubwa makundi hayo yamekuwa yakitumika kusambaza taarifa za uongo na uchochezi.

Mwangasa ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini kuwahubiria waumini wao juu ya matumizi sahihi ya mitandao ili kujiweka mbali na uhalifu.

"Ukosefu wa maadili ndio unachangia haya yote haya, ndiyo sababu narudi kwenu viongozi wa dini wasisitizeni waumini wenu watumie mitandao kwa maendeleo," amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TCRA, Mhandisi James Kilaba amesema mamlaka hiyo inaendelea kuchukua hatua kuimarisha ulinzi wa mawasiliano mtandaoni.

Amesema simu za mkononi kwa sasa zimekuwa kama silaha hivyo matumizi yake yanapaswa kuangaliwa kwa umakini zaidi.

No comments:

Post a Comment