Uamuzi wa kupokea pikipiki hiyo kama kielelezo cha kesi hiyo, ulitolewa jana na Jaji Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, anayesikiliza kesi hiyo inayowakabili washtakiwa saba.
Jaji Maghimbi alilazimika kutoa uamuzi mdogo baada ya kutokea mabishano ya kisheria wakati mawakili wa utetezi wakiongozwa na wakili Emanuel Safari kupinga kupokewa kwa kielelezo hicho.
Katika hoja zake, wakili Safari alisema shahidi wa tisa, Samwel Maimu hakuwa shahidi sahihi kutoa kielelezo kwa vile hakueleza namna alivyoipata hiyo pikipiki.
Maimu ambaye alikuwa mkuu wa operesheni katika tukio hilo, alitoa ushahidi wake akisema pikipiki hiyo ni moja ya vitu alivyovikusanya siku ya tukio na kuvitunza katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi (RCO).
Hata hivyo, katika hoja yake, wakili Safari alisema shahidi huyo kwa sasa sio mtunzaji wa vielelezo hivyo kisheria, ilitakiwa ionekane mnyororo wa tangu alipovihifadhi na alipokabidhiwa hiyo jana.
Jaji Maghimbi alikataa pingamizi hilo akisema shahidi huyo ni sahihi kwa kuwa aliweza kutambua na kuzitaja alama za kipekee zilizopo katika pikipiki hiyo aina ya Toyo yenye nambaT.316 CLG.
Baada ya kupokewa kwa kielelezo hicho, shahidi huyo aliendelea kutoa ushahidi wake kwa kuongozwa na Wakili mwandamizi wa Serikali, Omary Kibwana na mahojiano yalikuwa kama ifutavyo:-
Wakili Kibwana: Umeeleza kuwa tarehe 7.8.2013 ulipofika eneo la tukio ulikusanya pia maganda ya risasi, yalikuwa mangapi?
Shahidi: Yalikuwa 22.
Wakili Kibwana: Yalikuwa vipi kama ukiyaelezea?
Shahidi: Yana rangi ya grey (kijivu) na mengine yalikuwa na namba. Ninaweza kukumbuka chache kama 77 na 61 lakini siwezi kukumbuka namba zote.
Wakili Kibwana: Ulivyoyakusanya, uliyarudisha kuyahifadhi wapi?
Shahidi: Nilikwenda kuyahifadhi kwenye kasiki iliyopo ofisi ya RCO Kilimanjaro.
Wakili Kibwana: Ulimkabidhi nani ayahifadhi?
Shahidi: Kwa kipindi hicho mimi ndiyo nilikuwa mtunza stoo.
Wakili Kibwana: Hebu tueleze, ulitunzaje?
Shahidi: Niliyaweka kwenye bahasha nyeupe nikaandika exhibit (kielelezo), maganda 22 ya SMG au SAR yaliyokutwa eneo la tukio.
Wakili Kibwana: Kingine ulichoandika?
Shahidi: Niliandika namba ya kesi BMG/IR2786/2013
Wakili Kibwana: Hiyo bahasha uliyohifadhia hayo maganda ya risasi, ukipewa nafasi unaweza kuitambua?
Shahidi:Ndiyo
Wakili Kibwana: Vitu gani vitakufanya uitambue?
Shahidi:Ni kutokana na mwandiko wangu, jinsi nilivyoifunga na rangi ya bahasha.
Wakili Kibwana: (akimpa shahidi bahasha) Naomba uiangalie.
Shahidi: Ndiyo bahasha yenyewe niliyoweka maganda 22.
Wakili Kibwana: Naomba ionyeshe Mahakama hayo maandishi unayosema uliandika?
Shahidi: (akatoka kizimbani na kwenda kumuonyesha Jaji)
Wakili Kibwana: Ulisema bahasha hii uliiweka kwenye kasiki?
Shahidi: Ndiyo
Wakili Kibwana: Na kipindi hicho wewe ulikuwa mtunzaji wa stoo?
Shahidi: Ndiyo
Wakili Kibwana: Baada ya kuyaweka kuna wakati yaliwahi kupelekwa mahali pengine?
Shahidi: Sikumbuki kama yaliwahi kupelekwa sehemu nyingine.
Wakili Kibwana: Umesema ulikusanya pia bastola eneo la tukio?
Shahidi: Ndiyo
Wakili Kibwana: Ulikusanya bastola na nini?
Shahidi: Bastola moja na magazini mbili
Wakili Kibwana: Hiyo bastola ukipewa nafasi ya kuitambua utaweza?
Shahidi: Ndiyo nitaweza.
Wakili Kibwana: Utaitambuaje?
Shahidi: Kwa rangi yake, aina yake na namba zake
Wakili Kibwana: Ilikuwa na namba gani?
Shahidi: ELS 417
Wakili Kibwana: Kitu kingine unachoweza kukitambua?
Shahidi: Ni kwamba ilitengenezwa Australia
Wakili Kibwana: Hizo magazini mbili unaweza kuzitambua?
Shahidi: Zina rangi nyeusi, moja ni ndefu na moja ni fupi na zote zina namba.
Wakili Kibwana: Zina namba gani?
Shahidi: Ile ndefu ina namba 7151 na ile fupi namba 3206.
Wakili Kibwana: Kingine kwenye hiyo magazini?
Shahidi: Magazini ndefu ilikuwa na risasi 23 na fupi ilikuwa na risasi saba.
Wakili Kibwana: Hii bastola na magazini ulifanya nazo nini?
Shahidi: Nilizihifadhi kwenye kasiki ofisi ya RCO.
Wakili Kibwana: Ulizihifadhije?
Shahidi: Niliziweka kwenye bahasha nikaandika bastola za marehemu Erasto Msuya na nikaandika namba ya kesi.
Wakili Kibwana: Hiyo bahasha uliyohifadhia bastola na magazini mbili unaweza kuitambua?
Shahidi: Ndiyo ilikuwa na rangi ya kaki na ina mwandiko wangu.
Wakili Kibwana: Mheshimiwa Jaji tunaomba tumuonyeshe hiyo bahasha
Shahidi: (Baada ya kukabidhi na kuitizama) ndiyo bahasha niliyohifadhia bastola na magazini
Wakili Kibwana: Naomba ufungue hiyo bahasha utuonyeshe vilivyopo.
Shahidi: (akifungua na kutoa bastola) Hii ndiyo bastola aina ya Glock19 na namba zake kama nilivyozitaja ni ELS 417, rangi yake ni nyeusi na imetengenezwa Australia.
Wakili Kibwana: Hebu endelea.
Shahidi: (akatoa magazini) Hii ndiyo magazine niliyosema ni nyeusi, ina risasi 23 na namba yake ni 7151.
Wakili Kibwana: Naomba utuhakikishie hizo risasi.
Shahidi: (akizitoa kwenye magazini na kuzihesabu) ziko 23.
Wakili Kibwana: Na magazini ndogo?
Shahidi: (akiionyesha) ndiyo hii namba zake ni 3206, ina risasi saba.
Wakili Kibwana: Naomba utuhakikishie
Shahidi: (akazitoa na kuzihesabu) ziko saba.
Wakili Kibwana: Umetambua bastola kwa namba zake na sehemu ilipotengenezwa na umetambua magazini zote mbili. Naomba ionyeshe Mahakama hizo namba kwa ukaribu.
Shahidi: (akaenda kwa Jaji na baadae kwa wazee washauri wa Mahakama na mawakili wa utetezi na kuwaonyesha kwa ukaribu)
Wakili Kibwana: Baada ya kutambua bastola hii na magazine mbili, uko tayari kuzitoa kama kielelezo?
Shahidi: Ndiyo niko tayari kutoa bastola na magazini mbili zenye jumla ya risasi 30 kama kielelezo.
Hata hivyo, Wakili John Nundu alisimama na kupinga kupokewa kwa bastola na magazini hizo akisema sababu za kupinga zitatolewa na wakili Safari.
Katika hoja zake, wakili Safari alisema shahidi huyo katika ushahidi wake alidai kwa wakati huo alikuwa akifanya kazi kituo cha Himo na alisema vitu hivyo alivihifadhi katika kasiki ya RCO.
“Juzi alituambia badala yake, sasa kuna mtunza stoo mwingine aliyemtaja kwa jina la Hashimu. Kwa kuwa shahidi huyo siyo mtunza stoo, siyo competent (sahihi) kuvitoa kama kielelezo. Wala hajatueleza vielelezo hivi ambavyo havihifadhi tena yeye vilifikaje mikononi mwake leo (jana) hadi avitoe kama kielelezo kwa vile ile chain of custody (mnyororo) hauonekani.”
“Kuna mashaka makubwa na kwa maoni yetu hivi siyo authenticity (sio vyenyewe) na vinaweza kuwa vilichezewa. Katika mazingira haya tunaweza kupokea vitu vya kutunga, kuungaunga na kupandikiza,” alisema wakili Safari.
Hoja hiyo ilipingwa na wakili Kibwana anayesaidiana na Wakili Mwandamizi Abdalah Chavula na mawakili Lucy Kyusa na Kassim Nassiri akisema hazina mashiko.
Wakili Kibwana alisema kulikuwa hakuna haja ya kuwapo kwa mnyororo wa makabidhiano kwa kuwa shahidi wake alitambua vielelezo hivyo kwa alama za kipekee.
Baada ya kusikiliza mabishano hayo, Jaji Maghimbi aliahirisha kesi hiyo kwa muda ili kuandaa uamuzi mdogo na iliporejea, Jaji alitupilia mbali pingamizi hilo na kuvipokea vielelezo hivyo.
Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa ndani na nje ya Arusha, aliuawa kwa bunduki ya kivita ya Sub Machine Gun (SMG) Agosti 7, 2013 katika eneo la Mijohoroni wilayani Hai.
Kesi hiyo inawakabili washtakiwa saba ambao ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne (Mredii), Musa Mangu, Jalila Zuberi, Karim Kihundwa, Sadick Mohamed (Msudani au Mnubi) na Ally Mussa. Jaji Maghimbi aliahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu kwa ajili ya mawakili wa utetezi kumhoji shahidi.
No comments:
Post a Comment