Ni ujumbe wa kuhamasisha wazazi na walezi kuandikisha watoto wao kujiunga na masomo ya maandalizi ya kidato cha kwanza, maarufu Kiingereza kwa jina la ‘Pre form one courses’.
Unaweza kukiita kipindi hiki kuwa ni kipindi cha kuvuna kwani kila shule na hata vituo vya twisheni, vinajihimu kutangaza masomo hayo ambayo kwa kawaida huanza baada ya wanafunzi kufanya mitihani ya darasa la saba.
Uchunguzi mdogo wa Mwananchi umebaini wanafunzi wamekuwa wakilipa kati ya Sh20,000 hadi 100,000 kusomea masomo hayo kwa kila mwezi. Zipo shule zinazotoza karo ya miezi mitatu kwa mkupuo.
Uchunguzi unaonyesha masomo yanayofundishwa ni pamoja na Hisabati, Jiografia, Kiswahili, Kiingereza , Uraia na masomo ya sayansi.
Shule zinavyochangamkia wanafunzi
Chuo cha mafunzo ya ufundi wilayani Karagwe (KDVTC) ni miongoni mwa vituo vinavyojinadi kuwa vinatoa mafunzo maandalizi ya kidato cha kwanza kwa wahitimu wa darasa la saba mwaka 2017.
Katika tangazo lao lililomo kwenye mtandao Facebook, Mkuu wa chuo Paschal Thomas anaeleza lengo la mafunzo hayo ni kuwaandaa wanafunzi kabla ya kujiunga na kidato cha kwanza.
“Tayari walimu waliobobea katika masomo yote wameandaliwa na kwamba masomo hayo yanatarajiwa kuanza mnamo tarehe 19 Septemba mwaka huu,” inaeleza taarifa.
Taarifa inaendelea kusema kuwa gharama za fomu kwa ajili ya kujiunga ni Sh5,000 na masomo hayo yatachukua kipindi cha miezi minne kwa gharama ya Sh 100,000 kwa kila mwanafunzi.
Kwa upande wake, uongozi wa Shule ya Sekondari Mukombozi iliyopo mkoani Kagera, ukatangaza kupitia mtandao wa facebook ukieleza kuwa kozi hiyo imeanza Septemba 11 na itakamilika Disemba.
Shule hii iliyosajiliwa na Serikali kwa namba S.4961 tofauti na sekondari nyingi, ilitangaza kutoa kozi hiyo bure ikijikita kwenye masomo ya sayansi na kudai kuwa lengo ni kukusanya wanafunzi ili kubaini wenye uwezo wa kusoma masomo hayo.
“ Gharama ambazo mzazi anapaswa kulipia ni Sh 20,000 kwa ajili ya usajili, lakini pia anapaswa kuleta debe mbili za mahindi na maharage debe moja kwa ajili ya chakula cha miezi mitatu kwa mtoto wake atakapokuwa anasoma kozi hiyo,” anasema Makamu Mkuu wa shule hiyo Eladius Novat.
Katika hali iliyoonyesha kuwa uongozi wa shule hiyo unatumia kozi hiyo kusaka wanafunzi wa kidato cha kwanza, tangazo linaeleza kwa kutaja kiwango cha ada na baadhi ya mambo yanayofanyika shuleni hapo.
Wasemavyo wanafunzi
Ibrahim Suleiman aliyehitimu darasa la saba hivi karibuni, anasema masomo ya awali ya kidato cha kwanza yatampa mwanga wa kile atakachojifunza wakati atakapoanza sekondari kuliko kubaki nyumbani miezi minne akisubiri kuchaguliwa.
“Nafurahi kuanza masomo haya kuliko kubaki nyumbani, nimegundua nachojifunza pre form one ni kama kile nilichojifunza shule ya msingi, kwa hiyo najiandaa vizuri,”anasema.
Kwa upande wake, Kulawa Raymond aliyehitimu darasa la saba katika Shule ya Msingi Chemchem ya jijini Dar es Salaam, anasema kwa awali walijifunza masomo kwa lugha ya Kiswahili, kozi hiyo ni muhimu kwake kwa inamwaandaa kuimarisha lugha ya Kiingereza atakayokutana nayo sekondari.
Wazazi nao
Baadhi ya wazazi wanasema pamoja na umuhimu wa masomo hayo, Serikali ingeweka utaratibu wa masomo hayo kujulikana rasmi kuliko ilivyo sasa.
“Miezi minne kwa mtoto ni mingi kubaki nyumbani, bora wangecheleweshwa kufanya mtihani wa darasa la saba au kungekuwa na vituo maalumu vinavyotambuliwa kisheria kuepuka wizi unaofanywa na baadhi kwa kutoza fedha nyingi tofauti na kile kinachofundishwa,” anasema Naomi Michael, mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam.
Naomi haoni tatizo kulipa Sh60,000 kwa kipindi cha miezi mitatu anayosoma mwanawe. Anashukuru kuwa masomo hayo yanampa mtoto huyo fursa ya kuwa mtulivu na makini.
Hamis Mashaka, mkazi wa Mwananyamala, Dar es Salaam, anasema amempeleka mtoto wake kusoma kozi hiyo kwa malengo mawili.
“ Kwanza naamini kwamba inasaidia kumdhibiti asiwe na nafasi ya kuwa na nyendo za ovyo zitakazomtoa nje ya mstari. Lakini, pia masomo yatamsaidia kuwa ma msingi mzuri wa kuanza kidato cha kwanza,” anaeleza.
Vituo feki
Awali, katika maeneo kama vile jiji la Dar es Salaam, masomo ya pre form one yalikuwa yakitolewa katika vituo maarufu kwa jina la twisheni. Vituo hivi havikuwa na sifa ya kutoa taaluma. Baadhi vilikuwa ni vibanda huku walimu wakiwa vijana wahitimu wa kidato cha nne na sita.
‘’ Kilikuwa kama kipindi cha kuvuna kwa baadhi ya walimu wa vituo hivi. Mkazo waliuweka katika masomo hasa Kiingereza, lakini walimu wengi ni wajanja tu wa mjini. Hawakuwa na sifa za ualimu,’’ anasema mdau wa elimu, Bakari Heri.
Ofisa elimu Dar es Salaam azungumza
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hamis Lissu anasema anasema kozi hizo zinatolewa kwa makubaliano ya wazazi na shule au vituo husika.
“ Kozi hizo sisi hatuzisimamii hazitolewi kwa mwongozo ambao unatulazimu sisi kuzifuatilia bali makubaliano ya wazazi, jambo ambalo sioni kama ni baya iwapo elimu inazingatia silabasi husika inasaidia watarajia hao wa kidato cha kwanza kupata mafunzo ya awali,” anasema Lissu.
Mtazamo wa wataalamu wa elimu
Mhadhiri wa masuala ya elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Joviter Katabalo anasema muda unaotumiwa kwa kozi hizo, ulipaswa kutumika kuwafundisha watoto kazi za nyumbani.
Anasema kwa baadhi ya wazazi hasa wa mijini, wanatumia kuwapo kwa masomo haya kama fursa ya kutokuwa karibu nao.
Hiki kwao kilipaswa kuwa kipindi kizuri cha kuwafundisha baadhi ya kazi kama wanavyofanya wazazi kutoka jamii za ufugaji na kilimo.
Kwa upande mwingine, anayatazama masomo hayo kama ‘fasheni’ yaani mtindo wa mazoea kwa wazazi wengi.
“ Naona changamoto ya masomo hayo kuzalisha vijana wavivu, ambao kama wangefundishwa stadi za kazi zaidi, ingewasaidia kuwajengea uwezo wa kujitegemea vizuri hata wanapoendelea na masomo yao,’’ anaongeza.
No comments:
Post a Comment