Meli hiyo yenye uwezo wa kubeba lita 400,000 za mafuta, itakuwa ikifanya safari zake kutoka Kigoma, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mv Sangara ilisimama kufanya kazi tangu Februari 2016 kutokana na hitilafu kwenye injini.
Akizungumza ofisini kwake juzi, Kaimu Meneja wa MSCL, Eric Hamissi alisema matengenezo ya meli hiyo ya mizigo yamegharimu Sh97.9 milioni.
“Kuanzia wiki ijayo, Mv Sangara itakuwa imeanza kazi rasmi, kwa kuwa tayari tumeanza kupata wateja wa kuikodi kwa ajili ya kubebea mizigo,” alisema.
Licha ya Mv Sangara, meli nyingine ambazo zinatarajiwa kuanza kukarabatiwa kabla ya Novemba ni Mv Serengeti na Mv Clarias za jijini Mwanza.
“Kufikia Januari hali itakuwa tofauti na sasa. Baada ya kukamilisha meli hizo, kuna ujenzi wa meli mpya itakayogharimu Sh50 bilioni itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo,” alisema.
Tayari, makandarasi wamepatikana kutoka Korea Kusini ambazo ni kampuni za STX na KTMI.
Naye mfanyabiashara wa mkoani Kagera, Alphonce Maturu alisema ufufuaji wa meli hizo utawasaidia katika kufanikisha shughuli zao kiuchumi.
“Naamini baada ya kukamilika kwa matengenezo tutaendelea na harakati zetu za kiuchumi kwa kutumia Ziwa Victoria kama ilivyokuwa awali,” alisema.
No comments:
Post a Comment