Jaji Salma Maghimbi kutoka Mahakama Kuu jijini Arusha anayesikiliza kesi hiyo mjini Moshi, alilazimika kuahirisha kesi hiyo saa 4:40 hadi saa 4:50 asubuhi na baadaye saa 5:00 hadi saa 5:10 asubuhi.
Alipoahirisha kesi hiyo saa 4:40 asubuhi ilitokana na hoja ya mawakili wa Serikali kuhusu umri wa mzee mshauri wa mahakama, Marry John kuvuka miaka 60 unaotajwa na sheria.
Hali hiyo ilimlazimu Jaji Maghimbi kuahirisha kesi kwa dakika 10 ili kuteta faragha na mawakili wa Serikali na wa utetezi.
Hata hivyo, mahakama iliporejea na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula na kuanza kuwasilisha hoja ya umri, mshtakiwa wa pili, Shaibu Jumanne alijisikia vibaya na kuanza kutapika.
Jumanne maarufu Mredii alitapika kwa sekunde kadhaa akiwa kizimbani, hali iliyomlazimisha Jaji kukubaliana na mawakili wa pande zote kuahirisha kesi kwa dakika 10 kutokana na hali hiyo.
Licha ya mshtakiwa baadaye kusisitiza anaweza kuendelea, Jaji Maghimbi alisema anaahirisha kesi hiyo kwa dakika 10 ili kuanzia saa 5:00 hadi saa 5:10 pamoja na mambo mengine, kizimba kifanywe usafi.
Mahakama iliahirishwa na kufanyiwa usafi na iliporejea tena, Jaji Maghimbi alimuuliza mshtakiwa kama wakati huo anajisikia vizuri na yupo tayari kuendelea na kesi na akakubali yupo tayari.
Hoja ya umri
Akiwasilisha hoja ya umri ya mzee mshauri wa mahakama kwa niaba ya mawakili wengine wa Jamhuri, Wakili Chavula alielezakuwa amevuka miaka 60 inayotakiwa kisheria.
Wakili Chavula anayesaidiana na mawakili Omary Kibwana, Kassim Nassir na Lucy Kyusa alisema kifungu cha 266 (1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) kimeweka ukomo huo.
Alisema kifungu hicho kinachozungumzia umri wa wazee hao kinataka mtu anayeteuliwa awe na miaka kati ya 21 na 60.
“Kwa kuzingatia mwenendo wa shauri hili washtakiwa mbele ya mahakama yako walikamatwa tangu 2013, hivi sasa wana miaka minne mahabusu na hawajui hatima ya shauri lao,” alisema Wakili Chavula na kuongeza:
“Kwa mazingira hayo ya kesi kuwa ya muda mrefu na assessor (mzee) mmoja ameshatangulia mbele ya haki, mahakama ikimuondoa kwa kigezo cha umri itabidi itafute mzee mwingine.
“Akiteuliwa mwingine maana yake shauri zima lazima lianze upya na tulipotoka ni mbali. Tunaiomba mahakama yako itumie mamlaka yako kuongeza muda wa mzee huyu,” alisisitiza.
Akizungumza kwa niaba ya jopo la mawakili wa utetezi, Wakili Majura Magafu alisema baaada ya kushauriana na wateja wao wanaona ni vyema shauri hilo liendelee kwa kumtumia mzee huyo.
Wakili Magafu alisema kifungu namba 264 cha CPA kinaruhusu mahakama kujiwekea taratibu zake kila wakati za namna ya kuendesha mashauri ya jinai kunapotokea mazingira kama hayo.
“Kwa kumruhusu huyu mzee aendelee kutoa huduma hakuwezi kufanya mwenendo wa shauri hili uwe batili kama upande wa Jamhuri ulivyoeleza,” alisema.
Uamuzi wa mahakama
Katika uamuzi wake mdogo, Jaji Maghimbi alisema mahakama imeamua mzee huyo aendelee kuwapo katika kesi hiyo ili haki itendeke, hasa ikizingatiwa washtakiwa wapo mahabusu tangu 2013.
Hoja nyingine ambayo Jaji aliizingatia katika kufikia uamuzi huo ni kuwa tangu kesi hiyo ianze kusikilizwa mwaka 2015 ni mashahidi tisa tu wametoa ushahidi na inaweza kuleta usumbufu.
Baada ya uamuzi huo, shahidi wa tisa wa upande wa mashtaka, Inspekta Samwel Maimu aliendelea na ushahidi wake kuanzia alipoishia Machi 21 kesi hiyo iliposimama.
Katika ushahidi wake huo wa Machi 21, Inspekta Maimu alieleza namna Oktoba 5, 2013 alivyomkamata mshtakiwa wa saba, Ally Mussa maarufu Mjeshi mkoani Kigoma na kumrejesha Kilimanjaro.
Jana, shahidi huyo aliendelea kutoa ushahidi wake kwa kuongozwa na Wakili Chavula na mahojiano kati ya wawili hao yalikuwa kama ifuatavyo:-
Wakili Chavula: Baada ya kumkamata Ally Mussa Mjeshi mkoani Kigoma, nini kilifuata?
Shahidi: Tulimpeleka Polisi Kigoma na akaandika maelezo yake.
Wakili Chavula: Baada ya kuandika maelezo yake nini kingine ulifanya?
Shahidi: Jioni niliondoka naye kwa ajili ya safari ya kumleta Kilimanjaro.
Wakili Chavula: Ulifika Moshi na mshtakiwa lini?
Shahidi: Oktoba 7, 2013
Wakili Chavula: Baada ya kumkabidhi kwa RCO (mkuu wa upelelezi) nini ulifanya kuhusiana na mshtakiwa?
Shahidi: Baada ya kumkabidhi kwa RCO aliendelea na utaratibu wake.
Wakili Chavula: Hebu Agosti 7, 2013 ikumbushe mahakama kwenye lile eneo la tukio ulikusanya nini?
Shahidi: Maganda 22 ya SMG au SAR
Wakili Chavula: Haya maganda baada ya kuyakusanya ulifanya nini nayo?
Shahidi: Niliyaweka kwenye bahasha na nikaandika haya ni maganda 22 yaliyotumika kwenye mauaji.
Wakili Chavula: Kitu gani kingine ulikusanya kwenye eneo la tukio.
Shahidi: Bastola aina ya Glock.
Wakili Chavula: Ilikuwa kwenye mazingira gani?
Shahidi: Niliipata kwenye mwili wa marehemu.
Wakili Chavula: Ulifanya nini baada ya kuipata bastola hiyo?
Shahidi: Nilichomoa magazine na kuhakikisha usalama wake na kuiwekea alama.
Mfanyabiashara huyo aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa, aliuawa kwa kufyatuliwa risasi 22 za bunduki aina ya SMG, 12 ndizo zilizomuua.
Tukio hilo la aina yake, lilitekelezwa Agosti 7, 2013 katika eneo la Mijohoroni wilayani Hai na watu wasiojulikana, lakini polisi inawatuhumu washtakiwa saba kuhusika na mauaji hayo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne au Mredii, Musa Mangu, Jalila Zuberi, Karim Kihundwa, Sadick Mohamed au Msudani au Mnubi na Ally Mussa au Mjeshi.
No comments:
Post a Comment