Thursday, October 19

Lissu: Mungu alisema huyu hatakufa -VIDEO

Dar es Salaam. Hatimaye Tundu Lissu ametoa kauli ya kwanza iliyorekodiwa na kuambatanishwa na picha zinazomuonyesha akiwa amekaa na mwenye tabasamu, huku sauti ikiwa imara.
Katika sauti hiyo iliyosambaa mitandaoni jana jioni, mbunge huyo wa Singida Mashariki aliyeshambuliwa kwa risasi takriban 30 Septemba 7 mjini Dodoma, anajitambulisha na kuelezea jinsi watu walivyostushwa na kuwashukuru.
“Watanzania wenzangu, mimi ni Tundu Lissu. Nazungumza kutoka katika kitanda cha Hospitali ya Nairobi,” anasema Lissu katika mkanda huo ulioambatanishwa na picha za watu waliokwenda kumuona na wanaomuombea.
“Kwanza kabisa naomba nitoe shukrani kwa Mungu wetu wa mapenzi, Mungu wetu wa maisha, Mungu wetu wa uponyaji kwa kuniweka hai mpaka hapa nilipo.
“Kama isingekuwa Mwenyezi Mungu, maisha yangu yangeishia Dodoma siku ile. Lakini Mwenyezi Mungu, huyu wa uponyaji, alisema huyu hatakufa. Naomba nishukuru kwa hilo.”
Mkanda na picha hizo zimetolewa siku moja baada ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuelezea maendeleo ya afya yake, gharama za matibabu na hatua zinazofuata, huku akiahidi kutoa video hiyo wakati wowote kuanzia juzi, ahadi iliyoamsha shauku ya kumuona mwanasheria huyo.
Tangu aliposhambuliwa kwa risasi akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake mjini Dodoma, Chadema na watu wengine wamekuwa wakitoa maelezo ya maendeleo ya afya yake bila ya kuonyesha picha.
Lakini jana, picha zake zilitolewa na baadaye kusambaa kwa kasi mitandaoni kabla ya video mkanda wenye sauti yake kusambazwa jioni.
Lissu anasema katika sauti hiyo kuwa Watanzania walipaza sauti kumuomba Mungu maisha yake yaokolewe, akiwemo mama mmoja ambaye hakuweza kukumbuka kama alitokea Iringa au sehemu nyingine aliyeenda kumuombea.
“Nafikiri sitakosea nikisema kuwa niko hai kwa sababu ya maombi ya Watanzania hawa,” anasema Lissu.
Anasema tangu alazwe Nairobi, watu aliosema ni “wengi sana” wamejitokeza kumuombea, wakiwemo wananchi wa kawaida.
Anasema vyama vya kitaaluma kote duniani ambavyo vina ushirika na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), vimesaidia katika matibabu yake na kwamba amepata ujumbe wa kuungwa mkono kutoka mataifa ya Marekani, Uingereza, Australia, New Zealand, Ubelgiji, Ujerumani na Kenya.
“Lakini kuna kundi ambalo sijalisema, ambalo linahitaji kutajwa kipekee kabisa; madaktari, wauguzi na wafanyakazi wa kawaida wa Hospitali ya Nairobi, wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma pamoja na wafanyakazi wa tiba kutoka taasisi nyingine ambao kwa njia mbalimbali walishiriki kuniponya. Nawapa pongezi zangu za dhati kabisa,” anasema Lissu.
Picha zilizotumwa jana alasiri mitandaoni zinamuonyesha Lissu katika mazingira tofauti, lakini zote zinamuonyesha akiwa na tabasamu, huku akipunga mkono ulionyoosha vidole viwili kuashiria alama ya Chadema.
Mwonekano wa Lissu
Katika picha hizo, Lissu anaonekana kwenye kiti cha magurudumu, ambacho kinasukumwa na kaka yake, ambaye yuko na Ally Hemed, ambaye ni mkuu wa Idara ya Uenezi wa Chadema, Simon Mohamed Bakari (dereva wake) na mtu mwingine ambaye hajafahamika.
Picha hiyo inaonyesha mguu wa Lissu wa kulia ukiwa umenyooshwa, lakini umezungushiwa kitu kinachoonekana kigumu, huku mwingine akiwa ameukunja.
Picha nyingine inamuonyesha Lissu akiwa na makamu mwenyekiti wa Chadema wa Kanda ya Kati, Aisha Yusuph wote wakiwa wanatabasamu.
Picha ya kwanza kutoka inamuonyesha akiwa amekaa wodini kando ya kitanda. Anaonekana amenyoosha mkono uliofungwa utepe mwembamba mweupe, kama vile mtu ambaye anaendelea kuongezewa maji au damu.
Katika picha hiyo, nyuma yake kuna mipira ya dripu kama mitatu, mtungi wa gesi, dawa mbalimbali pamoja na chupa mbili za maji.
Mashuka na nguo zote ni nyeupe na ngozi yake ikionekana kung’aa.
Picha zake zatikisa mitandaoni
Picha hizo zilianza kusambaa mitandoni kuanzia saa 10:00 jioni na kuibua mijadala kuhusu Mwanasheria huyo mkuu wa Chadema aliyezaliwa Januari 20, 1968.
Katika kurasa za kijamii za Mwananchi za Facebook, Twitter na Instagram watu mbalimbali walikuwa wakitoa maoni yao.
Mmoja wao alikuwa, Josephat Mwambola aliyesema: ‘‘Watu wasiojulikana watambue kuwa Mungu yupo na anawajua. Ipo siku atawaweka hadharani na kuwaadhibu zaidi ya walivyomuumiza Tundu Lissu ambaye ni mtetezi wa kweli wa wanyonge hapa Tanzania.’’
Naye Babuu Makundi ameandika: “Sifa na utukufu ni kwa Mungu wetu aliye juu. Mungu ana makusudi na uhai wa Lissu.”     

No comments:

Post a Comment