Lulu ambaye yupo nje kwa dhamana anakabiliwa na kesi katika Mahakama Kuu akishtakiwa kwa kumuua Kanumba bila kukusudia.
Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 7, 2012, nyumbani kwa marehemu Kanumba, Sinza Vatican jijini Dar es Salaam.
Seth akitoa ushahidi mahakamani leo Alhamisi Oktoba 19,2017 amedai Aprili 7, 2012 Lulu alifika nyumbani kwa Kanumba saa sita kasoro dakika kadhaa usiku.
Amesema alimsikia Kanumba akimlaumu kwa kuzungumza na wanaume wengine kwenye simu mbele yake.
Shahidi huyo amedai wakati ndugu yake akimlalamikia Lulu, wawili hao walikuwa wakielekea chumbani kwa Kanumba.
Amedai baadaye wakaanza kuvutana, huku Lulu akiwa anataka kutoka na Kanumba akiwa anamvuta kuingia ndani.
Seth amesema Kanumba na Lulu waliingia chumbani na kufunga mlango lakini baadaye akiwa chumbani kwake alisikia kelele za ugomvi kati ya wawili hao.
Amesema baadaye Lulu alitoka chumbani na alimweleza kuwa Kanumba ameanguka.
Shahidi huyo amesema alikwenda chumbani kwa Kanumba ambako alikuta amekaa chini ameegemea ukuta, akiwa katika hali ya kukosa pumzi.
Seth amedai alimpigia simu daktari wao, Dk Paplas Kageiya ambaye alimtaka amfuate, hivyo wakati akielekea kwa daktari alimwambia Lulu abaki na Kanumba.
Amesema akiwa njiani, Lulu alimpigia simu akamweleza amemmwagia maji Kanumba lakini haamki, hivyo yeye anaondoka.
Shahidi huyo amesema walipofika na daktari hawakumkuta Lulu na kwamba, Dk Kageiya alishauri wampeleke Kanumba katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako baada ya daktari kumchunguza aliwaeleza alikuwa ameshafariki dunia.
Baada ya ushahidi huo, Jaji Sam Rumanyika anayesikiliza kesi hiyo aliiahirisha hadi kesho itakapoendelea kwa kusikiliza shahidi mwingine wa upande wa mashtaka.
Hilo linatokana na Wakili wa Serikali, Faraja George kuieleza Mahakama hakuwa na shahidi mwingine.
Awali, Wakili George aliieleza Mahakama kuwa walikuwa na mashahidi wawili akiwemo Dk Kageiya lakini wakati wakifanya mazungumzo na shahidi huyo, aliwaeleza asingeweza kutoa ushahidi kwa kuwa hajisikii vizuri na ameomba autoe kesho.
Wakili George ameileza Mahakama awali walikuwa na mashahidi wanne lakini kulingana na maelezo ya kesi, wataomba kuongeza shahidi mwingine mmoja.
No comments:
Post a Comment