MBUNGE mstaafu wa Chama cha Mapinduzi, Omar Mjaka Ali, amesema serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli inahitaji kuokolewa kwa sasa imepotea na kupoteza mwelekeo kutokana na rais kukosa washauri, anaandika Dany Tibason.
Mbunge huyo ambaye alikuwa mbunge wa CCM tangu mwaka 2000 hadi 2005 jimbo la Pemba Vitongoji, amesema kuwa kwa sasa nchi haina mwelekeo kutokana na kuendeshwa kwa matamko na matakwa ya mtu mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari kutoka chama cha waandishi wa habari kutoka mkoa wa Dodoma (CPC) pamoja na wenyeji wa Chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Kusini Pemba (PPC) nje ya ofisi ya mkuu wa wilaya ya Chake Chake mbunge huyo mstaafu amesema kuwa kwa sasa taifa limekosa mwelekeo.
Katika ziara hiyo iliyofadhiliwa na Muungano wa vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) alieleza kuwa yapo mambo mengi ambayo yanafanywa bila kufuata utaratibu na kuminya matakwa ya wananchi likiwemo suala la kutoonyesha vikao vya bunge moja kwa moja.
“Mimi nimekuwa mbunge wa CCM tangu mwaka 2000 hadi 2005 na mimi ni mwana CCM na nitaendelea kuwa CCM lakini yapo mambo mengi ambayo nayaona katika serikali ya Magufuli yakiwa siyo mazuri na hayo yanafanyika kutokana na kiongozi huyo kukosa washauri wazuri.
“Washauri wa rais wanashindwa kumweleza ukweli kuwa serikali ni ya wananchi, yapo mambo mengine ambayo wananchi wanayataka hata kama yeye hayataki mfano kitendo cha serikali kuzuia kuoneshwa kwa vikao vya bunge moja kwa moja, hiyo ni kuwaonea wananchi,” amesema mbunge huyo mstaafu.
Katika hatua nyingine, amekemea kitendo cha serikali kuwapora mali zao viongozi wastaafu na kudai kuwa jambo hilo siyo zuri kwani linaweza kusababisha migogoro ambayo siyo sahihi na kujenga chuki kati ya jamii na serikali.
Akizungumzia wajibu wa wabunge, amesema wote ni sawa wakiwa bungeni, awe CCM au Upinzani, hivyo wanatakiwa kutambua wajibu wao hususani katika kuisaidia serikali pale ambapo inaonekana kwenda tofauti.
Amesema kuwa wabunge wengi wamekuwa hawajui wajibu wao badala ya kuisimamania serikali wamekuwa ni watu wa kuijibia serikali au kujifanya wao ni sehemu ya serikali katika mambo ambayo ni ya msingi kwa maslahi ya jamii.
Aidha ameitaka serikali pamoja na bunge kuacha tabia ya kubeza maoni ya wapinzani badala yake maoni na ushauri wa wabunge wa upinzani yanatakiwa kufanyiwa kazi kwani kazi kubwa ya mbunge ni kuikosoa serikali ili iweze kukaa katika mstari.
“Mbunge ni mtu wa heshima iwe wa upinzani au wa chama tawala siyo jambo zuri kumtoa mbunge bungeni kwa kutumia jeshi la polisi kwa kufanya hivyo ni kumvunjia heshima mbunge na kulivunjia heshima bunge kwa ujumla hivyo washauri wanaomshauri rais na vyombo vyake wanatakiwa kutokuwa na hofu na badala yake wampe rais ushauri ambao ni sahihi
zaidi,” alisema Ali.
zaidi,” alisema Ali.
No comments:
Post a Comment