Thursday, October 19

Majeruhi washikiliwa kwa tuhuma za kusafirisha bangi


Kibaha. Majeruhi wawili wa ajali ya gari wanashikiliwa na polisi mkoani Pwani wakituhumiwa kuhusika na usafirishaji na biashara ya bangi kilo 7,500.
Majeruhi hao ni Gudluck Kundaeli maarufu Mbowe (24) mkazi wa Kiwalani na Ally Gebra maarufu Mtena (28) wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jonathan Shanna amesema leo Alhamisi Oktoba 19,2017 kuwa watuhumiwa walikamatwa jana eneo la Kwa Mathias mjini Kibaha baada ya upekuzi kufanyika kwenye gari walilokuwa wakisafiria aina ya Toyota IST lililopata ajali.
Amesema gari hilo lilipata ajali eneo hilo saa tatu usiku na askari walifika kutoa msaada ikiwemo kuwaokoa majeruhi ambao walipelekwa Hospitali ya Tumbi kwa matibabu.
Kamanda Shanna amesema baada ya kuwaokoa majeruhi na askari kufanya upekuzi kwenye gari walikuta magunia saba yenye bangi.
"Tulipata taarifa ya ajali kutokea eneo la Kwa Mathias, askari wakaenda kwa ajili ya uokoaji na waliwaokoa vijana hawa.  Baadaye walifanya upekuzi kwenye gari na kukuta bangi hiyo. Tumepima ina kilogramu 7,500 kwa hiyo tunawashikilia watusaidie katika uchunguzi," amesema Kamanda Shanna.

No comments:

Post a Comment