Tuesday, October 17

MADEREVA WA BODABODA ACHENI HARAKA - MAKAMU WA RAIS

Madereva wa Pikipiki (bodaboda) nchini wametakiwa kutii sheria za Usalama Barabarani bila shuruti kwani ajali nyingi zinazotokea barabarani zimekuwa zikisababishwa na uzembe unaofanywa na madereva hao.
Akizungumza leo katika maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama kitaifa mkoani Kilimanjaro Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa chanzo kikuu cha ajali hizo ni uharaka walionao madereva hao na ukosefu wa mafunzo ya usalama barabarani kwa baadhi ya madereva.
“Madereva wa bodaboda naomba mbadilike, muwe na tabia ya kutii sharia za usalama barabarani bila shuruti kwani ajali nyingi nchini zimekuwa zikisababishwa na nyinyi kutokana na haraka haraka zenu”, amesema Makamu Rais.
Aidha, amefafanua kuwa Tathmini iliyofanywa na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani kuanzia mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu katika mkoa wa Kilimanjaro imebaini kuwa kuna ajali za Pikipiki 84 zilizojitokeza ambazo kati ya hizo, 61 zimesababisha vifo na zilizobaki majeruhi.
Kuhusu ajali za mabasi ya abiria Mheshimiwa Makamu wa Rais amesema kuwa zimepungua kutokana na uwepo wa mbinu za udhibiti wa mabasi hayo kama vile upigaji picha kwa magari yanayozidisha spidi yakiwa barabarani (Tochi),  na ukaguzi wa mara kwa mara unaofanywa na Jeshi la polisi kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani katika magari ya abiria nchini.
Makamu wa Rais amefurahishwa na mkakati wa Serikali wa uandaaji wa mfumo mpya na wa kisasa wa kuweka kamera zitakazorekodi makosa ya usalama barabarani yanayofanywa na madereva nchini.
Ametoa rai kwa Askari wa Usalama Barabarani kutotumia kigezo cha kupiga Tochi kwa kuwaonea, kuwanyanyasa madereva na kudai rushwa kwani vitendo havikubaliki kisheria na hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo.
“Taswira tunayoitaka ni kuwa wananchi wawaone askari  kama walinzi wa mali zao na maisha yao na si vinginevyo”, amesisitiza Makamu wa Rais.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amelitka Baraza la Taifa la Usalama Barabarani na wadau wake kuhakikisha wanabadilisha mbinu za namna ya kukabiliana na tatizo la ajali nchini na kuongeza nguvu katika kudhibiti mwendo kasi, ulevi kwa madereva, kutovaa kofia ngumu kwa waendesha bodaboda, kutofunga mkanda kwa baadhi ya abiria na ukosefu wa vifaa vya kuwalinda watoto wadogo wakiwa kwenye gari.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba (Mb), amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa wataboresha na kuunda mbinu mbalimbali ili kudhibiti ajali za barabarani zinazoweza kuepukika.
Amewataka wananchi kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika kupunguza ajali za Barabarani na kuwasisitiza madereva kuzingatia sheria za usalama Barabarani kwani hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote anayekiuka sheria hizo.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa (Mb), amesema kuwa Baraza limekuwa likifanya jitihada mbalimbali ili kudhibiti ajali za barabarani kama utoaji wa elimu kwa umma kupitia vyombo vya Habari kama Televisheni na Redio pamoja na uandaaji wa viperushi na majarida.
Maadhimisho ya Wiki ya nenda kwa Usalama Barabarani Kitaifa yaliyobeba kauli mbiu “Zuia ajali, Tii Sheria – Okoa maisha”, kwa mwaka huu yameadhimishwa mkoani Kilimanjaro amabapo yameshirikisha wadau mbalimbali wa usalama nchini.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro katika maadhimisho ya Wiki ya nenda kwa Usalama Barabarani kitaifa yaliyofanyika mkoani humo
Wananchi wakimsikiliza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, katika maadhimisho ya Wiki ya nenda kwa Usalama Barabarani kitaifa yaliyofanyika mkoani humo, leo.
 Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usalama Barabarani na Mazingira kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joyce Mbunju, akieleza mikakati inayofanywa na Serikali katika kudhibiti ajali za barabarnia kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, alipotembelea Banda la Wizara hiyo katika maadhimisho ya Wiki ya nenda kwa Usalama Barabarani kitaifa yaliyofanyika mkoani Kilimanjaro
 Mpima magari kutoka mzani wa Himo, mkoani Kilimanjaro kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani humo Mhandisi Adam Labay, akifafanua jambo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, alipotembelea Banda la Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), katika maadhimisho ya Wiki ya nenda kwa Usalama Barabarani kitaifa yaliyofanyika mkoani Kilimanjaro
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kwenye maadhimisho ya Wiki ya nenda kwa Usalama Barabarani kitaifa yaliyofanyika mkoani Kilimanjaro
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiungana na kikundi cha ngoma za asili cha Msanja, kutoka Mkoani Kilimanjaro kucheza   ngoma hiyo katika maadhimisho ya Wiki ya nenda kwa Usalama Barabarani kitaifa yaliyofanyika mkoani humo, leo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, 
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment