Mabalozi wa nchi za Magharibi wamewashutumu viongozi wa upinzani na viongozi wa serikali nchini Kenya huku nchi hiyo ikiendelea kujiandaa kwa maruduo ya uchaguzi wa urais baadaye mwezi huu.
Wawakilishi hao wa nchi 13 pamoja na Umoja wa Ulaya wamesisitiza kwamba uchaguzi mpya unafaa kuwa "bora kuliko uliofanyika awali (mwezi Agosti) - uwe huru, wa kuaminika na wa Amani".
Taarifa yao ya pamoja imetolewa baada ya mkutano kati yao na maafisa wakuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC).
Kwenye taarifa hiyo, mabalozi hao wakiwemo Robert Godec wa Marekani, Susie Kitchens wa Uingereza na Jutta Jardfelt wa Ujerumani, wametoa wito kwa wadau kuheshimu uhuru wa tume hiyo ya uchaguzi na kuiacha ifanye kazi yake bila kuingiliwa.
Mapema leo, wafuasi wa muungano wa upinzani National Super Alliance walitawanywa na polisi walipojaribu kuandamana nje ya afisi kuu za IEBC, Nairobi kushinikiza mabadiliko katika tume hiyo.
Balozi wa Marekani nchini Kenya Bob Godec amesema juhudi za chama tawala kutaka kurekebisha sheria za uchaguzi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo "zinazidisha wasiwasi na uhasama wa kisiasa".
Kadhalika, ameushutumu upinzani kwa kutishia kususia uchaguzi huo.
Mgombea wa upinzani Raila Odinga amesisitiza kwamba "hakutakuwa na uchaguzi" iwapo maafisa ambao anadai walihusika katika kuvuruga uchaguzi uliopita hawataondolewa kwenye tume hiyo.
"Hii ni fursa kwa pande zote mbili kuonyesha sifa za uongozi bora, kuimarisha demokrasia ya Kenya na kuinua hadhi ya taifa hili kimataifa. Inasikitisha kwamba kwa sasa mambo yanaonekana kutokea kinyume," alisema Bw Godec.
Majaji wa Mahakama ya Juu walipokuwa wakifuta matokeo ya uchaguzi wa awali walisema haukuwa wa wazi na kwamba ilikuwa vigumu kubaini nani alishinda kwa njia halali.
Waliiamuru IEBC kuandaa uchaguzi wa marudio na kufuata kikamilifu katiba na sheria za uchaguzi.
Majaji hao walisema hawatasita kufuta tena matokeo ya uchaguzi iwapo uchaguzi mpya hautaandaliwa kwa kufuata katiba na sheria za uchaguzi.
Upinzani Nasa umetishia kuandaa maandamano kila Jumatatu na Ijumaa kushinikiza mageuzi katika IEBC.
No comments:
Post a Comment