Na MWANDISHI WETU-DODOMA
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema kuwa wapiga kura waliopoteza vitambulisho vya kupigia kura watapata fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani wa kata 43 unaotarajiwa kufanyika Novemba 26, mwaka huu.
Hayo yalisemwa jana mjini hapa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhani Kailima, katika mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi na wasimamizi wasiadizi wa uchaguzi yanayoratibiwa na kuendeshwa na NEC.
Alisema wapigakura hao wataruhusiwa kutumia leseni ya udereva, vitambulisho vya uraia vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na hati ya kusafiria.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia kifungu namba 62 (a) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambacho kinasema mpigakura aliyeandikishwa kwenye daftari atakwenda mwenyewe kwenye kata aliyojiandikisha, kwenye kituo alichopangiwa, kumridhisha msimamizi wa kituo au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kwamba yeye ndiye mpiga kura kwa kumuonyesha kadi ya kupigia kura lakini kinasema kwamba Tume inaweza ikaelekeza utambulisho mwingine wowote utakaomsaidia mpiga kura kuweza kupiga kura iwapo kadi hana.
“Tume kwa kuzingatia kifungu hicho, kuanzia uchaguzi huu imetoa maelekezo kwenye mafunzo haya kwamba Tume imekubali vitambulisho vifuatavyo vitumike, moja ni pasi ya kusafiria, pili ni kitambulisho cha taifa kilichotolewa na NIDA na mwisho ni leseni ya udereva,” alisema
Alisema ruhusa hiyo imetolewa kwa sharti moja kwamba majina na herufi yaliyopo kwenye kitambulisho hicho yafanane na majina na herufi zilizopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Aliongeza kusema kwamba NEC itakutana na vyama vya siasa hivi karibuni kuwajulisha juu ya maagizo hayo, lakini akasisitiza kwamba tofauti yoyote itakayo kuwepo kwenye majina itamnyima mpigakura fursa ya kupigakura.
Alisema maamuzi hayo yamefikiwa kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ambalo kwa mara ya mwisho liliboreshwa mwaka 2015.
“…..katika kipindi chote hichi (2015-2017) inawezekana kwa namna moja ama nyingine, kuna baadhi ya wapigakura wamepoteza kadi zao za kupigia kura na kwa sababu hatujaboresha na sheria inasema watapata hizo kadi baada ya daftari kuboreshwa, wanaweza wakakosa fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi wa madiwani wa kata 43.
“Lakini wengine kadi zao zimeharibika kiasi kwamba haziwezi kusomeka na wengine kadi zao zimechakaa kabisa kwa sababu moja ama nyingine kutokana na mazingira yaliyopo,” alisema Kailima.
Wakitoa maoni yao juu ya agizo hilo la NEC, washiriki wa mafunzo hayo wamepongeza hatua hiyo na kusema kwamba itakuza wigo wa demokrasia nchini kwa kuwapa fursa wapigakura halali ambao kwa sababu zilizoko nje ya uwezo wao wamejikuta hawana kadi za kupigia kura licha ya kwamba ni wapiga kura halali waliojiandikisha.
No comments:
Post a Comment