Umewahi kujaribu kumuua mbu au nzi? Utagundua kwamba huwa vigumu sana. Wadudu hawa huwa na kasi ajabu. Lakini inakuwaje wadudu hawa wadogo - wenye ubongo mdogo hivi - wanaweza kuwazidi binadamu kwa urahisi hivi?
Je, huwa wanaweza kujua kwamba unataka kuwaua hata kabla yako kujaribu kuwaua?
Ni swali ambalo watu wengi wamekuwa wakijiuliza, lakini usishangae tena.
Sababu ya wadudu hawa kuwazidi binadamu na wanyama wengine ni mtazamo wao wa dunia.
Wadudu hawa huitazama dunia kwa mwendopole yaani slowmotion ukilinganisha na tunavyoyatazama matukio.
Kwa kufafanua, hebu utazame mshale wa saa.
Kama binadamu, huwa unauona mshale huo wa saa ukisonga kwa kasi fulani.
Lakini kwa wanyama wengine hali ni tofauti.
Mfano kasa atautazama ukisonga kwa kasi mara mbili zaidi ya kasi anayoiona binadamu.
Kwa mbu, nzi na wadudu wengine wa karibu, mshale huo wa saa watauona ukisonga kwa kasi mara nne chini ya kasi anayoitazama binadamu.
Kimsingi, kasi ya kusonga kwa wakati hubadilika kutoka kwa mnyama hadi mwingine.
Wanyama kimsingi huutazama ulimwengu kama video inayocheza mfululizo.
Kwa kufafanua, huwa wanaunganisha picha nyingi kutoka kwenye sehemu zao nyingi kwenye macho hadi kwenye ubongo kwa kasi ya juu, mara kadha kila sekunde. Kwa binadamu, picha hizi hutumwa mara 60 kila sekunde, kwa kasa mara 15 kila sekunde, na kwa mbu, nzi na wadudu wengine wanaopaa mara 250 kila sekunde.
Tofauti
Kasi ambayo picha hizi husomwa kwenye ubongo wa mnyama huweza kupimwa. Kwa kawaida, wanyama wadogo huwa na kiwango cha juu cha kasi hii, ikiwa ni pamoja na mbu na nzi. Binadamu kwa sababu ni wanyama wakubwa, kiwango chao cha kasi hii kiko chini.
Prof Roger Hardie, wa chuo cha Cambridge, amekuwa akitafiti jinsi mbu na nzi hufanya kazi, na ameandaa hata kipimo cha kupima kiwango hiki cha kasi ya mnyama au mdudu kufasiri picha kwenye ubongo.
"Kiwango hiki kwa ufafanuzi mwingine ni kasi ambayo mwanga unafaa kuwashwa na kuzimwa kabla ya kutambuliwa na ubongo au kuonekana kama mwendelezo wa mwanga," anasema Prof Hardie.
Roger huweka vipande vidogo vya gilasi kwenye sehemu ya macho ambayo huusoma mwanga na kisha kuwasha taa ya LED kwa kasi na kuendelea kuongeza kasi hiyo huku akifanya vipimo vyake. Kila taa inapowashwa, nishati fulani huzalishwa kwenye sehemu hiyo ya jicho inayosoma mwanga na nishati hii inaweza kupimwa na kompyuta na mchoro kuandaliwa.
Vipimo vyake vimebaini kwamba nzi wenye uwezo wa kuona kwa kasi zaidi wanaweza kutenganisha mng'ao wa mwanga mara 400 kwa sekunde.
Uwezo wao ni mara sita zaidi ya uwezo wa binadamu.
Nzi mwenye uwezo wa juu zaidi hufahamika kama "nzi muuaji". Ni nzi mdogo sana mla wadudu ambaye hupatikana maeneo ya Ulaya. Huwa anapaa na kuwanasa nzi wengine wakiwa angani kwa kasi ya juu ajabu.
Kwenye maabara yake ya "nzi" katika chuo kikuu cha Cambridge, Dkt Paloma Gonzales-Bellido anadhihirisha uwezo wa juu wa nzi hao wauaji kwa kumwachilia mdudu mla matunda ndani ya kisanduku maalum ambapo mtu anaweza kupiga picha. Ndani yake kuna nzi muuaji wa kike.
Paloma ananakili wanachofanya nzi hao kwa kupiga video ya fremu (picha) 1,000 kwa sekunde kwa kutumia kamera za video za mwendopole. Nzi anapoanza kusonga, anapiga video ya sekunde 12 na kuhifadhi video hiyo.
Anatumia njia maalum, ya kuhifadhi video fupifupi ambazo zinajifuta kila sekunde 12 na kuhifadhi sekunde 12 za mwisho pekee baada ya kuhakikisha kwamba amenasa tukio.
"Muda wetu wa kuchukua hatua ni wa mwendopole sana kiasi kwamba iwapo tungebofya kwa kawaida kwenye kitufe cha kupiga video wakati tunafikiria kwamba tukio hilo linafanyika, tukio hilo litakuwa lilishafanyika," anasema Dkt Gonzales-Bellido. Hatuwezo kutumia uwezo wetu pekee kutegemea tutabofya kitufe nzi wakianza kuchukua hatua.
Vita vya nzi
Nzi huyo muuaji na windo lake wakiwa ndani ya kisanduku, mwanzoni nzi huyo muuaji alikaa tu bila kufanya chochote, lakini nzi mla matunda alipopaa umbali wa sentimeta 7 hivi, ghafla bin vuu, nzi muuaji aliruka na kufumba na kufumbua macho nzi akawa amegeuzwa kuwa mlo.
Ni baada ya kuangalia video ya mwendo pole kwenye kompyuta ambapo inakuwa wazi nini kilifanyika.
Nzi huyo muuaji alipaa, akamzunguka nzi huyo mla matunda mara tatu akijaribu kumnasa, na mwisho akafanikiwa kumkamata kwa miguu yake ya mbele.
Hayo yote kuanzia kupaa hadi kutua tenda na windo lake yalitokea kwa sekunde moja pekee.
Kwa macho yetu, hilo linaonekana kama tukio la ghafla.
Kwa kweli basi, kitendo chetu cha kujaribu kumnasa au kumuua nzi kwa mkono basi kwa nzi mkono huonekana ukisonga kwa mwendo wa konokono.
Hilo humuwezesha mbu au nzii kupaa na kutoroka kabla ya mkono wako kumfikia.
Ili kumuwezesha nzi huyu muuaji kufikia kasi hii ya ajabu, ambayo inazidi ya nzi wengine, seli zenye kugundua mwanga kwenye macho ya nzi hao huwa na mitochondria (betri au kiwanda cha nishati ndani ya seli) kwa kiasi cha juu kuliko kwenye seli sawa katika nzi wengine.
Hizi ndizo betri za seli na kwa hivyo basi, jambo ambalo linadokeza kuwa ili kuona kwa haraka lazima mdudu, mnyama au ndege yoyote Yule anahitaji kiasi cha juu cha nishati kuliko wakati anaona kwa mwendopole.
Hii labda inafafanua ni kwa nini macho yote hayana uwezo sawa.
Kwa sababu nzi muuaji hula nyama, nyama hiyo humpa viwango vya juu vya nishati anayoihitaji kutumia kwenye seli hizo za macho.
Hata kama tungekuwa na kiasi sawa cha mitochondria kwenye seli za macho yetu, hatungekuwa na kasi sawa ya kuona sawa nay a nzi hao kwa sababu muundo wa seli za kutambua mwanga ndani ya macho ya nzi bado huwa tofauti na wa viumbe wengine wenye uti wa mgongo.
Asili ya hili imo katika asili ya viumbe wenyewe.
Wadudu na viumbe wenye uti wa mgongo walichipuka kutoka kwenye
Wazazi wa makundi haya mawili ya viumbe walitengana karibu miaka 700-750 milioni iliyopita.
Nzi hutumia viungo vinavyofanana na nyuzi kunasa na kusafirisha mwanga ndani ya jicho. Viungo hivi huchanganyikana na mwanga lakini si kwa ndani kama kemikali. Lakini kwenye viumbe wenye uti wa mgongo, huwa na seli zinazofanana na bomba ndogo ambazo huwa na kemikali kwenye shina lake ambazo huchanganyikana na mwanga.
Kuna baadhi ya viumbe wenye mti wa mgongo ambao wana uwezo wa kuona kwa kasi kuliko binadamu.
Hili mara nyingi huonekana kuwiana na uwezo wa kiumbe husika kupaa au la, na pia iwapo ni kiumbe mdogo au mkubwa.
Hii huenda ni kwa sababu wanaopaa wanahitaji kuchukua hatua upesi kuepuka kugongana na vitu angani.
Viumbe wenye uwezo wa juu zaidi wa kuona huwa ni wale ambao wanaweza kuwanasa nzi wakiwa angani.
Miongoni mwa viumbe wenye uti wa mgongo, watafiti katika chuo kikuu cha Uppsala nchini Sweden waligundua kwamba ndege afahamikaye kama 'pied flycatcher' ambaye huwanasa nzi wakiwa wanapaa, ana uwezo wa kutambua mwanga ukiwashwa na kuzimwa mara 146 kwa sekunde.
Uwezo wao wa kutenganisha mwanga ulikuwa karibu mara mbili zaidi ya uwezo wa binadamu, lakini uwezo wao haukufikia uwezo wa nzi wa kawaida.
Hii ina maana kwamba ndege, sawa na nzi, hutazama mshale wa saa ukisonga kwa mwendo wa pole zaidi kushinda binadamu.
Inaonekana kama njia ya kujinusuru kuhakikisha uhai wa viumbe.
Ndege hao wanahitaji kuona kwa kasi ili kuweza kunasa windo, nzi nao wanahitaji kuona kwa kasi kuweza kuwakwepa wanaowawinda.
Utakapojaribu tena kumuua mbu au nzi ushindwe, usife moyo.
Juhudi zao zinazimwa na mambo ambayo yamekuwepo kutokana na mabadiliko ya mamilioni ya miaka kwenye viumbe kuhakikisha baadhi ya viumbe wanaendelea kuishi.
Ndio maana mbu au nzi atauona mkono wako ukielekea upande wake kwa mwendopole na kumuwezesha kuukwepa!
No comments:
Post a Comment