Monday, October 2

Kuminya demokrasia ndio chanzo wanasiasa kupumulia mitandao ya kijamii


Kinachoonekana dhahiri sasa ni kuwa kanuni mpya za maudhui ya utangazaji na mitandao ya kijamii zinakwenda kuongeza udhibiti katika eneo hilo.
Hili ni eneo ambalo kwa siku za karibuni limegeuka mkombozi na mahali pa wanasiasa na wananchi wengine kupumulia baada ya uhuru wa kujieleza na demokrasia kuonekana inaminywa kwa namna moja au nyingine.
Mathalan, Alhamisi iliyopita wadau wa habari nchini waliinyooshea kidole Serikali kwamba imeweka mazingira ambayo yanasababisha wananchi washindwe kutoa taarifa, na vyombo vya habari vishindwe kutafuta taarifa na kuziripoti kwa mujibu wa sheria na Katiba.
Hali hii kwa mujibu wa wadau hao ni kinyume na Katiba ya nchi, ibara ya 18 (1) inayosema, “bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa”.
Pia, wanasema inapingana na kifungu cha pili cha ibara hiyo kinachotoa haki kwa rais “kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi”, na kuhusu masuala muhimu kwa jamii.
Achilia mbali uhuru wa kujieleza, pia wanasiasa wanaendelea kulia kutokana na kupokwa haki yao ya kufanya mikutano ya hadhara, kuandamana kama inavyoelezwa sheria ya vyama vya siasa na Katiba.
Ni kutokana na mazingira hayo, wanasiasa, wanahabari na wananchi kwa ujumla wameona mitandao ya kijamii kama sehemu mbadala ya kupumulia; huko ndiko wanakotolea maoni yao.
Ndio kisa cha wanasiasa wa chama tawala, wakiwamo viongozi wa kitaifa na wale wa upinzani na hata wananchi, kutumia mitandao kutoa maoni yao.
Hata Rais John Magufuli amekuwa akitumia ukurasa wake wa Twitter kutuma ujumbe kwa jamii, kama ilivyokuwa alipompongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kutetea kiti chakes na kutoa pole kutokana na mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi.
Pia, hatujasahau majibishano ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na wabunge wa upinzani ambao walitoa picha za video kwenye mitandao ya kijamii wakikosoa mwenendo wa Bunge.
Matumizi hayo ya teknolojia ya kisasa katika mawasiliano, yamesababisha wasomi na wanasiasa kueleza bayana kuwa yametokana na kuminywa kwa demokrasia nchini.
Mbali na kuunga mkono matumizi ya mitandao hiyo kutolea dukuduku zao, pia wameeleza wasiwasi wao wa jamii kuchanganyikiwa kutokana na kupata habari za kweli na nyingine zisizo za kweli.
Mfano, Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe anasema kuzuia demokrasia haiwezekani.
“Hata maji yakizuiwa njia, hutafuta pa kupita na yakifanya hivyo wakati mwingine husababisha athari kwa sababu hutafuta njia zisizo rasmi,” anasema.
Anasema wanasiasa sasa ni kama maji yanayofanya kila linalowezekana kutafuta namna ya kupita. Ndiyo maana mitandao ya kijamii inafurika kauli zao.
“Hiyo ndiyo njia pekee iliyobaki kwa wanasiasa, hasa wa upinzani, kutafuta namna ya kuwafikia wananchi ambao ni wanachama wao,” anasema.
Anasema cha kushuruku ni mitandao ya kijamii ambayo ndiyo imekuwa mwokozi pekee kwa wanasiasa wakati huu ambao wamenyimwa haki zao za kisheria na kikatiba za kufanya mikutano.
Kwa mtazamo wake, mitandao ya kijamii ikitumika vema, itawasaidia wananchi kupata taarifa na itawasaidia wanasiasa kutoa kile ambacho wasingeweza kukaa nacho kifuani, ingawa kuna athari kwa kiasi fulani.
“Athari zake ni kuwa wananchi wanachanganyikiwa kwa sababu inachukua muda mrefu kupata ukweli wa nani kasema nini,” anasema.
“Wakati ukweli unatafutwa, mengine yanazidi kutokea. Kibaya zaidi mitandao imevamiwa na wasiokuwa na nia njema na kusambaza mambo wanayoyajua wenyewe kwa kutumia majina ya wanasiasa na kutoa kauli zisizo sahihi.”
Lakini, mtaalamu wa masuala ya kisiasa na kijamii, Dk Peter Bujari anaangalia zaidi athari za zuio hilo kwa wanasiasa.
“Kibaya zaidi (wanasiasa) wanazuiwa bila kujali kuwa wanachokifanya ni haki yao. Kumzuia mtu kuzungumza kunasababisha awe na hasira, ambayo inaweza kumsababishia madhara ya kiafya yeye binafsi na watu wanaomzunguka,” anasema Bunjari ambaye ni daktari wa binadamu.
“Wananchi na wanasiasa hasa wa upinzani wana msongo wa mawazo kutokana na katazo la kutozungumza masuala ya siasa mikutanoni ambayo ni jukumu lao la msingi.
“Niamini mimi, miaka ijayo kutakuwa na watu wengi waliochanganyikiwa. Hili jambo linachukuliwa kirahisi lakini ni baya na lina athari.”
Anasema ukimziba mdomo binadamu, lazima atafute namna ya kuzungumza na wao kama wanadamu wameona hii ya mitandao ya kijamii ndiyo njia sahihi ya wao kuwasiliana na umma.
Anaeleza kuwa njia hiyo ni nzuri na inawafikia zaidi walengwa wa mabadiliko ambao ni vijana, lakini pia mawasiliano hayo yanapunguza gharama.
“Kupitia mtandao unaweza kuwasiliana na watu wengi kwa wakati mmoja na ukitumia gharama nafuu kuliko mkutano utakaokulazimisha kutumia nauli, vifaa vya kupasa sauti na muda,” anasema.
Anasema angalau katika mitandao ya kijamii, wananchi wanapata kile walichokuwa wanakikosa.
“Si kweli kwamba wananchi hawataki kuwasikia wanasiasa, wanataka na ndiyo maana maneno machache wanayoyaandika mitandaoni yanazunguka na kupata sauti, maoni kutoka kwa wananchi,” anasema Bunjari.
Anasema mitandao pia imeonyesha matokeo chanya kwa sababu imeibua kashfa nyingi ambazo zikifuatiliwa zinaonekana zina ukweli.
Hata hivyo, anasema ukweli unabaki palepale kwamba ili wanasiasa wapate ahueni, wanapaswa kufanya mikutano ya hadhara kama sheria ya vyama vya siasa na Katiba inavyoelekeza.
Suala la umuhimu wa mitandao pia lilizungumzwa na Profesa Mohamed Bakari wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Imesaidia ukimya ambao ungetawala wakati huu wa katazo la kufanya mikutano,” anasema.
“Kwa maana hiyo, hata wakiruhusiwa kufanya mikutano, bado wataendelea kuitumia mitandao kwa sababu inawafikia walio wengi kwa wakati mmoja bila kujali muda.
“Mitandao ina nguvu, tofauti na ilivyokuwa inafikiriwa hapo awali. Hakuna anayechukulia kama ni kitu cha kupita, inapewa uzito uleule.”
Anasema tofauti na vyombo vingine vinavyotumika kufikisha ujumbe, ikiwamo magazeti, redio na runinga ambako habari huhaririwa kabla ya kutoka, mitandao ya kijamii hufikisha ujumbe kama ulivyo bila kupunguza na kupata kitu halisi kutoka moyoni mwa aliyekitoa.
“Kwangu njia hii ni sahihi na iendelee kutumika, nchi zilizoendelea zimeitumia sana na imezaa matunda.
“Kuna vitu vilikuwa vinafichwa fichwa, kupitia mitandao ya kijamii vimebainika na kizuri zaidi. Haidhibitiki kirahisi kama vyombo vya habari ambavyo hufungiwa au kupewa onyo kwa kukubali kutoa taarifa kama hizo,”anaongeza Profesa Bakari.
Anasemaa licha ya kuwapo kwa athari kutokana na baadhi kuitumia vibaya, bado tatizo ni dogo ukilinganisha na faida.
Anasema hata kutumia nyumba za ibada kufanya siasa si mbaya, ingawa kumekuwa na katazo la kuhofia kuchanganya dini na siasa.
Anafafanua kuwa hakuna mstari uliopigwa wa kuzuia jambo hilo kwenye nyumba za ibada na imekuwa ikifanyika, kwa mfano wahubiri wanapopinga ufisadi, rushwa na kusisitiza amani.
“Kimtazamo ni mambo ya kawaida, lakini kimsingi ni siasa, hivyo inawezekana kuzitumia nyumba za ibada kwa namna tofauti na ujumbe ukafika,” anasema.
Akijazia mjadala huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda anasema uhuru huu wa kujieleza haujaminywa kwa wanasiasa pekee bali hata kwa wananchi, kwa kuwa hawana nafasi ya kutoa mawazo na ndiyo maana kila mmoja anaeleza kinachomuuma, kinachomkera kuhusu nchi kupitia mitandao.
Anasema ni njia nzuri na imeondoa pengo kati ya wakubwa na wananchi, hivyo waitumie ipasavyo kufikisha kile wanachoona kitasaidia kusonga mbele.
“Hata namna inavyotumika inaonekana kabisa ni kwa hasira kutokana na kuzuiwa kuzungumza kwenye maeneo husika, ndiyo maana hakuna anayetoa elimu zaidi ya kukemea.
“Kama kungekuwa na uhuru wa kutoa maoni, kujieleza, labda wangekuwa wanazungumza mengine badala ya kukemea na kuhoji kila kukicha,” anasema Mbunda.
Anaungana na wasomi wenzake kuonya kuwa mbali na kusaidia kwa kiasi fulani bado kuna athari zinazoweza kutokea ikiwamo upotoshwaji mkubwa wa taarifa kutoka kwa wazoefu wa mitandao.
“Wananchi hasa wanakuwa na wakati mgumu kufahamu ipi ni taarifa sahihi iliyotoka kwa mtu sahihi kutokana na ‘magangwe’ hao kutumia mitandao kupotosha umma.
“Sitaki kuamini kama wanafanya huku wakijua wanachokifanya kina madhara gani, ingawa kwa upande mwingine inaonyesha wazi wanaelewa wanachokifanya,” anaongeza Mbunda.
Mbunda anafafanua kuwa Serikali inatakiwa itathmini na kuona haja ya kuruhusu mikutano ya kisiasa, hii itasaidia kuepuka Taifa kuingia katika sintofahamu ya kupokea maneno ya kweli na uongo kila kukicha.
Anasema wananchi wakikosa taarifa sahihi wanachanganyikiwa na hiyo inaweza kuzaa chuki kwa asiyestahili.

No comments:

Post a Comment