Wanajeshi wa Kenya jana waliwaua wanamgambo watano wa kundi la Al-Shabaab kwenye oparesheni yao katika msitu wa Boni kaunti ya Lamu. Wanajeshi hao pia walipata bunduki sita aina ya AK-47, risasi-321, guruneti tatu na vilipuzi kadhaa baada ya kuwavizia wanamgambo hao katika eneo la Bodhei. Katika taarifa, afisa wa maswala ya umma katika jeshi la KDF, kanali David Obonyo aliwahakikishia wakenya kuwa msako dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabaab utaendelea ili kukomesha visa vyovyote vya mashambulizi ya kigaidi katika eneo hilo. Kanali Obonyo alisema wanamgambo waliouawa ni sehemu ya kundi ambalo limekuwa likitekeleza mashambulizi katika eneo la Pwani. Mnamo Julai mwaka huu, watu tisa waliuawa katika kijiji cha Jima, eneo la Lamu Magharibi ilihali mwezi Agosti watu watatu waliuawa kwenye shambulizi la wanamgambo wa Al-Shabaab dhidi ya basi la abiria katika eneo la Witu, kaunti ya Lamu.
No comments:
Post a Comment