Thursday, October 19

Dk Mahiga aongoza ujumbe wa Tanzania mkutano wa Maziwa Makuu



Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga

Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga 
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Saba wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) akimwakilisha Rais John Magufuli.
Mkutano huo umefanyika leo Oktoba 19,2017 mjini Brazzaville, Jamhuri ya Congo ukitanguliwa na mingine ya awali katika ngazi ya wataalamu wa masuala ya fedha, wakuu wa vyombo vya usalama, wakuu wa majeshi, waratibu wa nchi na mawaziri wa mambo ya nje.
Taarifa kwa vyombo vya habari imesema mkutano huu umehudhuriwa na wakuu wa nchi, Serikali na wawakilishi wao kutoka mataifa ya Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jamhuri ya Kongo, Kenya, Rwanda, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia.
Ajenda kuu ya mkutano huo ilikuwa ni kupitia na kujadili hali ya siasa, ulinzi na usalama katika eneo la Nchi za Maziwa Makuu na hasa katika nchi za Burundi, DRC, Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini. Nyingine ilikuwa kupokea taarifa ya michango ya nchi wanachama.
Kuhusu hali ya usalama katika Nchi za Maziwa Makuu kwa jumla iliripotiwa kuwa inaendelea kuimarika kwa kiwango kikubwa isipokuwa kwa DRC ambako  operesheni zinaendelea kufanywa na Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DRC- Monusco (FIB) dhidi ya vikundi vya waasi vya ndani ya DRC na vile vinavyotoka nje ya nchi hiyo.
Mkutano huu ulifuatiwa na mwingine wa nane wa wakuu wa nchi na Serikali wa Mpango wa Amani na Usalama katika Maziwa Makuu.
Taasisi zingine za kimataifa zilizoalikwa kwenye mikutano hiyo ni Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).
Ujumbe wa Sadc uliongozwa na Katibu Mtendaji wake, Dk Stergomena Tax.

No comments:

Post a Comment