Tuesday, October 24

DC ILALA AWATIMUA POLISI WANAOPIGA RAIA UKONGA

Siku mbili baada ya polisi kuwatembezea kichapo wakazi wa Ukonga jijini Dar es Salaam kwa madai ya kuuawa kwa askari mwenzao, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amewataka askari hao kuondoka maeneo ya makazi ya watu mara moja.
Mjema ametoa amri hiyo leo Oktoba 24, alipowatembelea na kuongea na wakazi hao kutokana na kadhia waliyoipata ambapo inadaiwa askari hao wamekuwa wakiwapiga baada ya kifo cha askari mwenzao anayedaiwa kuuawa na wananchi.
“Kama askari ameshafariki utaratibu ulikuwa uchunguzi ufanyike wale ambao wamefanya makosa wachukuliwe hatua za kinidhamu lakini huko barabarani sitaki kuona FFU wanasumbua watu, waondoke wakaendelee na kazi waacheni watu wafanye kazi zao za kila siku bila kubughudhiwa.
“Wale wote walioumia jiorodhesheni muende mkapate matibabu kwa sababu mmeumizwa na wale waliokamatwa nitachukua majina yao ili tuweze kuhakikisha wananchi mnaendelea na kazi zenu ili muishi kama wananchi wengine,” amesema Mjema.
Awali wakielezea masikitiko yao mbele ya Mkuu wa Wilaya, baadhi ya wakazi hao walisema kwa muda wa siku mbili hasa nyakati za usiku wamekuwa wakinyanyaswa kwa kupigwa na askari hao hadi kufikia hatua ya kufunga biashara zao na kujifungia ndani.
“Ni kweli wenzetu wamepoteza ndugu yao ni jambo la kuhuzunisha, lakini hatua walizochukua hazikubaliki kwa sababu wanapiga ovyo ovyo kina mama, watoto na vijana, haikubaliki eti wanasema wanalipa kisasi kwa ndugu yao naomba mkuu wa wilaya uchukue hatua,” amesema mkazi mmoja wa wakazi hao aliyejitambulisha kwa jina la William Igogo.
Hata hivyo, wananchi hao ambao walikuwa na hasira walimwambia Mkuu wa Wilaya askari anayewasumbua hapo wakimtaja kwa jina la JJ, huku wakimwonyesha kwa vidole wakisema askari huyo ni jipu na si askari ila mhalifu.

No comments:

Post a Comment