Wananchi wa Kata za Themi, Sekei na Sombetini Wilaya ya Arusha mjini leo wameanza zoezi la Usajili Vitambulisho vya Taifa kwa kishindo; huku baadhi wakihangaika huku na huko kutoa nakala ya viambatisho vyao ili kujisajili kwa wakati.
Akizungumza katika Usajili huo Afisa Usajili wa Wilaya hiyo Bi. Juliet amesema wamepanga kukamilisha usajili wa Kata hizo ndani ya siku 9; na kwamba wananchi wote wanaoishi katika Kata hizo kujitokeza kwa wingi ili wasajiliwe.
Misururu ya wananchi imeonekana katika Kata za Themi na Sekei; huku baadhi wakihangaika kujaza fomu za maombi ya Usajili. Katika hali iliyoonyesha ushirikiano na kujizatiti kwa viongozi katika kuhakikisha wananchi hao wanahudumiwa, ofisi za Mitaa leo zilifungwa kwa muda na huduma zote kuhamia katika makao makuu ya Kata ili kuwaidhinishia wananchi fomu zao pamoja na kuwagongea mihuri kuthibitisha makazi yao.
Zoezi la Usajili kwa Wilaya ya Arusha Mjini linatazamiwa kukamilika ndani ya miezi miwili; ambapo wananchi wataweza kupata namba za Utambulisho (NIN) wakati hatua za uzalishaji Vitambulisho zikiendelea. Wilaya nyingine mkoani humo ambazo usajili unaendelea ni Karatu, Longido, Arumeru na Monduli.
Mmoja wa Wageni Wakaazi mkoani Arusha na mkazi wa Kata ya Sekei akikamilisha Usajili wa Vitambulisho vya Taifa. Zoezi la Usajili kwa mkoa wa Arusha linahusisha wananchi wenye umri wa miaka 18 na kuendelea na Wageni Wakaazi wenye kuishi halali nchini.
Watumishi wa NIDA wakiingiza taarifa za wananchi kwenye mfumo kutumia mashine maalumu ya Usajili ambayo pia inauwezo wa kuhifadhi si tu taarifa za kawaida pia alama za kibaiolojia na picha za waombaji wa Vitambulisho wakati wa Usajili.
Ofisi ya Kata ya Themi ambako zoezi la Usajili limeanza rasmi, na kukutanisha mamia ya wananchi kupata huduma.
Afisa Uhamiaji kutoka Ofisi ya Uhamiaji makao makuu Arusha akihakiki uraia wa mmoja wa wananchi katika Kata ya Themi aliyefika kujiandikisha.
No comments:
Post a Comment