Sunday, October 29

AMANI HUJENGWA KWA MARIDHIANO


HIVI karibuni Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, aliwataka viongozi wa kisiasa kujenga utamaduni wa kukutana mara wanapogundua kuna matukio yanayoashiria uvunjifu wa amani.
Jaji Warioba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema waasisi wa taifa hili walijenga misingi ya umoja ambao hivi sasa unaelekea kutoweka.
Ushauri huo una mashiko kwa jamii.
Jaji Warioba amesema kuna viashiria vya kutoweka kwa amani na viongozi wa kiserikali na kisiasa wanapaswa kuiga mfano unaofanywa na viongozi wa dini, ambao hukutana mara kwa mara kujadili masuala mbalimbali yakiwamo ya kitaifa.
Jaji Warioba anasema: “Nchi haiwezi kuendeshwa kwa huyu kuongea hiki, huyu naye anamjibu kupitia vyombo vya habari, hapana, hawa watu wakae wazungumze.”
Bila shaka Jaji Warioba amezungumza hayo akiamini kuwa majibizano yenye mtazamo huo aliouzungumza hayawezi kujenga mshikamano, bali ni chanzo cha watu kuibua migogoro hali inayoweza kuhatarisha amani ya taifa.
Linapozungumzwa suala la amani, linajumuisha utulivu na masikilizano miongoni mwa jamii, wakiwamo viongozi wa kisiasa.
Kwa muktadha huo, ili kujenga ushirikiano na amani, ni muhimu viongozi wetu wa kisiasa kujenga utaratibu wa kukutana mara kwa mara na kutazama mwelekeo wa taifa kwa nia ya kujenga umoja wetu ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere.
Wote tunafahamu kuwa amani ni kitu kinachojengwa kwa nguvu kubwa ya pamoja, lakini ikivunjika ni vigumu kuirejesha.
Kwa msingi huo, sisi kama taifa ni muhimu kuutazama ushauri wa Jaji Warioba kwa jicho pana badala ya kutumia nguvu kubwa kujibishana.
Ifahamike kuwa ustawi wa taifa haujengwi kwa misuguano au malumbano yasiyo na tija, bali hujengwa kwa kukaa pamoja kujadiliana kwa hoja hatimaye kukubaliana.
Jaji Warioba ametoa ushauri, ni vema uzae matunda. Naamini watu wazima akiwamo mzee Warioba wakitoa ushauri maana yake wameona jambo.

No comments:

Post a Comment