Tuesday, October 31

Aliyedaiwa kuuawa na FFU azikwa


Babati. Hatimaye mwili wa Regina Daniel (23) mwanamke aliyeuawa kwa kupigwa risasi na mzazi mwenzake ambaye ni askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mjini Babati mkoani Manyara, Cosmas James umezikwa. 
Mwili wa marehemu Regina ulizikwa jana Jumatatu kwenye Kijiji cha Mamire wilayani Babati baada ya ndugu wa marehemu kugoma kuzika hadi waelezwe hatima ya mtoto aliyezaa na askari huyo. 
Baada ya ndugu wa marehemu kuzungumza na Inspekta Isack Mahembe walikubali kuzika na ibada ya mazishi ikaongozwa na mchungaji John Sulle wa Kanisa la KKKT usharika wa Mamire. 
Polisi waligharamia usafiri wa kutoa mwili hospitali ya mji wa Babati, gharama za jeneza la marehemu huku gharama za chakula kwenye mazishi hayo zikigharamikiwa na ndugu wa marehemu.
Akizungumza wakati wa mazishi hayo mchungaji Sulle aliwaomba ndugu wa marehemu kusamehe tukio hilo na kumkabidhi Mungu kwani ndiye muweza wa yote. 
"Kitabu kitakatifu tunachokiani cha biblia kinatuambia kuwa kisasi ni cha bwana hivyo tunapaswa kusamehe na kulikabidhi jambo hili kwa mwenyezi Mungu kwani yeye ndiye mwenye kugawa haki," amesema mchungaji Sulle. 
Amesema hata suala la maisha ya mtoto wa marehemu huyo Mathayo Cosmas mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi nane lipo kwenye uwezo wa Mungu mwenyewe kwani ndiye mpangaji wa wote. 
"Waombolezaji wengi nimewasikia wakijiuliza juu ya hatma ya mtoto wa marehemu ambaye mama amefariki na baba yupo mahabusu kwa mauaji ya mama, sisi tusiwe waamuzi wa hilo kwani yupo Mungu ambaye atalisimamia hilo ipasavyo," amesema mchungaji Sulle. 
Kaimu kamanda wa polisi wa mkoa huo, Longinus Tibishubwamu amesema bado wanamshikilia mahabusu askari huyo wa FFU. 

No comments:

Post a Comment